MAONI YA MHARIRI: TFF isilete siasa katika suala la viwanja vya Ligi Kuu Bara

Muktasari:

Hata hivyo, ni bahati mbaya suala la viwanja limekuwa likipuuzwa sio na klabu tu ambazo ni chache zinazomiliki viwanja, lakini hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)

ILI mchezo wa soka usonge mbele ni lazima kuwepo na mambo muhimu na mipango madhubuti ya kuwezesha kuleta tija.

Moja ya nyenzo muhimu za kulipeleka mbele soka ni ubora wa viwanja pamoja na uwekezaji kuanzia chini sambamba na usimamizi bora wa mchezo huo.

Kunapokuwapo viwanja vyenye ubora na kukidhi matakwa ya soka kuwawezesha wachezaji kuonyesha uwezo wao, kunasaidia hata kufanya ligi iwe nzuri kwa sababu timu zinaonyeshana kazi na kupata matokeo yanayostahili.

Hata hivyo, ni bahati mbaya suala la viwanja limekuwa likipuuzwa sio na klabu tu ambazo ni chache zinazomiliki viwanja, lakini hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndio wasimamizi wa soka ni kama hilo hawalizingatii sana.

Ni kweli TFF hufanya ukaguzi kila mara kwenye viwanja vinavyotakiwa kutumika kwa michezo ya ligi, lakini kuna wakati ukaguzi huo ni kama unafanywa kiasi ndio maana haishangazi wakati mwingine kushuhudia viwanja vibovu vikiruhusiwa.

Majuzi mara baada ya pambano la Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Njombe Mji, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alinukuliwa akiulalamikia uwanja wa Sabasaba kuwa, haufai kutokana na mazingira yake yalivyo.

Nsajigwa alilalamikia eneo la kuchezea na hata vyumba vya wachezaji kuwa ni vichafu, huku uwanja huo ukiwa na mazingira yasiyovutia kwa mechi ya Ligi Kuu kuchezwa pale na kushangaa ilikuwaje hata Sabasaba ukaruhusiwa kwa ligi.

Mwanaspoti linaamini Nsajigwa ni mzoefu wa viwanja vya soka kwani amecheza kwa muda mrefu na kwa mafanikio ndani na nje ya nchi, hivyo kile alichokisema kimetokana na jinsi alivyouona uwanja huo. Lakini kinachoshangaz, siku chache zilizopita TFF ilikaririwa kuwa wanaweza kuvifungia viwanja vya Manungu Complex na Mabatini Mlandizi kama wamiliki wake watashindwa kukamilisha majukwaa ya kuruhusu mashabiki kukaa.

Ni kauli inayoshangaza kwa sababu, mtu ambaye ni mgeni angedhani alichokuwa akikiangalia kupitia runinga angehisi ni mechi ya mchangani ama Ligi Daraja la chini na sio mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Eneo la kuchezea lilikuwa sio rafiki kwa wachezaji pia mashabiki waliokosa kuingia uwanjani walikuwa wana uwezo wa kuufuatilia mchezo huo wakiwa nje kutokana na uwanja huo wa shule kuzungukwa na majumba na miti iliyoruhusu watu kupanda juu na kufuatilia mchezo huo bila tatizo.

Achana na uwanja kustahili kuchezwa kwa mechi za madaraja ya chini, lakini TFF ndio iliyohuruhusu kwa mechi za ligi, hapo ndipo unmapoweza kuona tatizo lipo wapi na shirikisho ni kama linaendesha mambo kisiasa.

Siasa hizo hizo ndizo zilizokwamisha kwa muda mrefu Azam kuutumia uwanja wake wa kisasa kucheza dhidi ya klabu zisizo na viwanja vyao vya Simba na Yanga kwa visababu ambavyo hazikuwa na maana. Simba wameenda kucheza Chamazi wikiendi iliyopita na mechi kumalizika salama wa salimini bila lolote kutokea tofauti na watu walivyoaminishwa awali na TFF kuzuia mechi za vigogo kupigwa uwanjani hapo.

Ndio maana tunasema wazi imefika wakati TFF iache kufanya mambo kwa mazoea na kukumbatia siasa badala yake ifanye mambo kisasa kwa manufaa ya soka la Tanzania. Viwanja visivyokidhi matakwa visiruhusiwe kwa mechi za ligi kwa sababu ya kisiasa na urafiki kwa sababu ni chanzo ha kudidimiza soka na kuifanya Tanzania lidumae na kuachwa na mataifa yaliyokuja nyuma yetu.

Ligi Kuu ni daraja la juu la mashindano ya soka na lazima iwe na heshima yake, ni kweli tuna uhaba wa viwanja, lakini bado haivutii kuona mechi ya ligi hiyo ikichezwa kwenye mazingira yanayozidiwa hata michuano ya ndondo.

Viwanja vibovu licha ya kuhatarisha usalama wa wachezaji, viongozi na mashabiki, pia vinachangia kukwamisha kuwapa nafasi wachezaji kuonyesha viwango vyao kama ambavyo mechi ya Njombe Mji na Yanga ulivyokuwa.

Tunaamini uongozi wa TFF chini ya Wallace Karia na Michael Wambura ni wasikivu na watafanyia kazi ushauri huu juu ya umuhimu wa mechi za Ligi Kuu kuchezwa viwanja vyenye ubora, kwa manufaa ya soka la Tanzania.