TFF inatengeneza matatizo mengi halafu haiyatatui

Raisi wa TFF Wallace Karia

Muktasari:

Wakati wa mkutano na wahariri kwenye Hoteli ya Seaeacape, alisema TFF imefanya makubwa katika kipindi kifupi tangu kuingia madarakani Agosti 12, 2017.

TANGU kuingia madarakani kwa uongozi wa awamu ya nane wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Agosti 2017 chini ya Rais Wallace Karia, soka la limeshuhudia madudu mengi kuliko mazuri ambayo uongozi huu unayafanya mpaka sasa.

Wakati wa mkutano na wahariri kwenye Hoteli ya Seaeacape, alisema TFF imefanya makubwa katika kipindi kifupi tangu kuingia madarakani Agosti 12, 2017.

Kila mtu anajua kilichotokea kwa Abajalo na Mvuvumwa kwenye Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Timu hizi zilikuwa na mechi za raundi ya pili ya mashindano hayo dhidi ya Prisons na JKT Tanzania mtawalia, lakini baadhi ya wachezaji wao hawakuwa na leseni, hivyo wakashindwa kucheza mechi zao. Timu hizo zikatolewa kwenye mashindano.

Kwa utaratibu wa Tanzania, usajili hukamilika halafu kunakuwa na kipindi cha mapingamizi na mambo mengine yanayofanana na hayo halafu ndio wachezaji waidhinishwe na kupewa leseni zao ili waanze kuzitumikia timu zao mpya.

Utaratibu huu ni wa ovyo kupita maelezo kwa sababu wakati timu zinasubiri TFF wakae na kuidhinisha wachezaji, mashindano yanaendelea na timu hizo hizo zinazosubiri, zinatakiwa kucheza. Sasa zitachezaje ilhali wachezaji wao wapya hawajaidhinishwa na wale wa zamani wamehama? Hiki ndicho kilichowatokea Abajalo na Mvuvumwa.

Wakati unatafakari hilo, liangalie hili la viwanja vitakavyotumika kwa raundi ya nne ya Kombe la FA. Timu za JKT ya Dar es Salaam, Kiluvya United ya Pwani, KMC ya Dar es Salaam pia na Buseresere ya Geita zimehamishwa kutoka viwanja vyao kwa sababu mbalimbali.

Kuna zilizoridhia lakini JKT imesikika ikilalamika kuchaguliwa uwanja wa kutumia.

Hoja yao ni kwamba uwanja wao una sifa stahili, lakini kama hauna hizo sifa kwa nini hawakuambiwa ni sifa gani zinazotakiwa ili warekebishe? Wanasema hatua za awali zote wamecheza hapo, kimebadilika nini wakati huu?

JKT wanazuiwa kutumia uwanja wao na kuchaguliwa uwanja mwingine, Kiluvya United nao wanahamishwa kutoka Uwanja wa Filbert Bayi na kupelekwa Mabatini, uwanja ambao una sifa za chini kulinganisha na Uwanja wa JKT Tanzania.

KUBWA KULIKO YOTE

Hayo yote ni tisa, 10 ni haya madudu ya Ligi Daraja la Pili (SDL). Timu ya AFC ya Arusha inalalamika kudhulumiwa haki yao na African Sports ya Tanga, pia na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Malalamiko ya AFC ni mchezo wao dhidi ya African Sports ya Tanga ulimalizika kwa kipigo cha 2-0. Katika mchezo huo, wenyeji African Sports waliwachezesha wachezaji wawili waliotumia leseni ambazo sio zao, mmoja alitumia leseni ya Athuman Mwile na mwingine akitumia Emmanuel Mpungumoto.

Wachezaji halisi wenye leseni hizi hawakuwepo siku ya mchezo huo, hivyo African Sports wanatakiwa kupokonywa pointi zote walizozivuna wakiwa na wachezaji hawa. AFC walikata rufaa lakini rufaa yao ikatupiliwa mbali.

Mzee wa Upupu nimebahatika kuongea na mmoja wa wachezaji halisi wenye leseni hizi, Emmanuel Mpungumoto ambaye anasema yeye alishangaa kuona kikosi cha African Sports kikiwa na mchezaji mwenye jina lake.

Emmanuel mwenyewe anasema yeye alikaribia kusajiliwa na AFC, lakini dili likakwama na akaangukia African Sports lakini aliondoka timu hiyo baada ya kucheza mechi mbili tu kutokana na kutoelewana kwenye masilahi.

Akiwa nyumbani Morogoro, akashangaa kujiona kwenye kikosi cha African Sports Mkwakwani Tanga. Hili ndilo suala ambalo AFC wanalilalamikia, lakini TFF ya Karia haitaki kulisikia. Kwa mwenendo huu, mpaka atoke madarakani, Karia inawezekana akauacha mpira wetu njia panda.

Kinachotakiwa kwa TFF ni kuhakikisha mpira unachezwa tena kwa kufuata sheria, kanuni na misingi inayosimamia soka. Vinginevyo itakuwa vurugu tu.