TFF iache kuzibebesha klabu Ligi Kuu mzigo wa gharama

Muktasari:

Kabla ya uongozi wa Wallace Karia kuingia madarakani, TFF ya Leodegar Tenga na Jamal Malinzi ilikuwa ikilalamikiwa kwa sababu ya panga pangua ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Bara.

MTU hujifunza kutokana na makosa, lakini kinachoendelea ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni kama sikio la kufa ambalo daima huwa halisikii dawa.

Kabla ya uongozi wa Wallace Karia kuingia madarakani, TFF ya Leodegar Tenga na Jamal Malinzi ilikuwa ikilalamikiwa kwa sababu ya panga pangua ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Bara.

Hata wakati wa Uchaguzi Mkuu wa TFF uliofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma, wadau wengi wa soka walikuwa na imani kubwa kuwa, uongozi mpya utaleta mabadiliko na kukomesha tatizo hilo la mabadiliko ya ratiba kila mara.

Hata hivyo hata mwezi haujapita tangu uongozi mpya uingie madarakani tatizo hilo limejitokeza, japo kina Karia na wenzake hawawezi kubeba lawama ya moja kwa moja kwa sababu ratiba ilitengenezwa kabla hawajaingia madarakani.

Lakini bado hiyo haiwezi kuufanya uongozi huo kulaumiwa kwa kitendo cha Bodi ya Ligi (TPLB) kuamua kuziahirisha mechi zilizokuwa zimepangwa kuchezwa katikati ya wiki hii na kuzipeleka tena wikiendi.

Hakuna sababu ya maana iliyofanya mechi hizo zisogezwe mbele tena wakati klabu zikiwa kwenye maandalizi ya safari na michezo yao baada ya kuahirishiwa Jumamosi iliyopita kupisha pambano la timu za taifa za Tanzania na Bostwana.

Mwanaspoti linafahamu mechi moja tu ya Yanga dhidi ya Njombe Mji iliyokuwa ichezwe mjini Njombe, ndiyo pekee ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la uwanja, lakini mechi nyingine zilipaswa zichezwe wakati ratiba nzima ikiendelea kurekebishwa. Kwa hakika kuna mkanganyiko mkubwa wa ratiba nzima ya msimu huu na wiki iliyopita tuliligusa hapa na kutaka TFF na Bodi ya Ligi kufanyia marekebisho mapema ili kusaidia kuifanya ligi na ushindani na kuleta usawa.

Lakini bado inakuwa ngumu kuamini imekuwaje zikaahirishwa mechi za katikati ya wiki na kupelekwa mwishoni mwa wiki wakati klabu zikiwa zimeshaanza maandalizi ya mechi hizo ama safari kufuata wapinzani wao?

Huku ni kuzibebesha mzigo mkubwa klabu shiriki bila sababu ya maana kwani kama wasimamizi wa ligi walijua zisingechezwa, wala wasingezipangia tarehe ya katikati ya wiki badala yake wangeacha mechi zilizokuwa zimepangwa katika ratiba ya awali kwa wikiendi ya Septemba 9 zichezwe hizo.

Na mechi hizo zilizokwama kuchezwa wiki iliyopita kuangalia namna ya kupangwa upya katika tarehe nyingine na klabu zingeridhika kwa sababu zingejua zinacheza lini na hata maandalizi yao yangelenga kwenye mechi hizo.

Hata hivyo, kwa kuwa Bodi ya Ligi inaendesha mambo yake kwa mazoea na kwa vile klabu zimekuwa zikikubalizikiridhika na mzigo wa gharama wanaobebeshwa kila mara bila kufidiwa, ndio maana haya yanatokea na yataendelea kutokea.

Kwa hakika suala hili linaziumiza klabu nyingi hasa zenye uchumi mdogo na pia kupunguza morali ya wachezaji wa timu shiriki za ligi hiyo. Mbaya zaidi ni kwamba kitendo hiki kinatokea mwanzoni kabisa kwa msimu na Mwanaspoti linaamini uongozi wa Karia utaliangalia jambo hili kwa jicho pana na kuchukua hatua kuzipunguzia mzigo klabu.

Ni bora kungekuwa na utaratibu wa klabu kufidiwa pale mechi zinapoahirishwa bila sababu za maana, lakini kwa kuwa hakuna kitu kama hicho ni vema uongozi wa TFF ujipange na kukomesha uhuni huu. Soka letu hjaliwezi kusonga mbele kama makosa haya yanajirudia kila mara licha ya ahadi tamu tamu za kulikomesha. Soka letu haliwezi kwenda na kasi ya dunia ilivyo kama kila uchao kunatokea mambo yanayowavunja moyo wachezaji na kuvuruga mipango ya walimu wa timu shiriki katika kujiandaa na mechi zao. Kadhalika waliopo ndani ya Bodi na hata Kamati ya Mashindano inashindwa kupanga ratiba ya ligi kwa kuangalia kalenda ya mashindano ya Fifa na ile ya Caf ili kuepukana na aibu ya mara kwa mara wakati zinaongozwa na wasomi?

Kufanya kosa sio kosa, ila kurudia ndio kosa na wahusika ni kama wamekuwa sugu katika kuvuruga soka la Tanzania kwa kushindwa kuwa makini kila msimu katika upangaji wa ratiba.