Sura hizi zikitua England itakuwa freshi kinoma

Muktasari:

  • Fainali hizo zimeondoka na kuachana kumbukumbu tamu kutoka kwa wachezaji walioonyesha viwango vikubwa na kuwafanya mashabiki kutamani kuwaona wakicheza kila wiki.

LONDON, ENGLAND. HADI kufikia jana Jumapili ilikuwa wiki moja imeshakatika tangu fainali za Kombe la Dunia 2018 zilipomalizika huko Russia na Ufaransa kuibuka mabingwa ilipoichapa Croatia katika mechi ya fainali.

Fainali hizo zimeondoka na kuachana kumbukumbu tamu kutoka kwa wachezaji walioonyesha viwango vikubwa na kuwafanya mashabiki kutamani kuwaona wakicheza kila wiki.

Kutokana na hilo, kuna mastaa ambao walitamba kwenye fainali hizo za Russia wanaowafanya mashabiki wanaopenda soka la Ligi Kuu England kutamani kuwaona wakijiunga na timu za ligi hiyo ili wapate nafasi ya kuwaona kwenye mchakamchaka wa michuano hiyo kila wiki.

Kylian Mbappe

Fowadi huyo wa Paris Saint-Germain ni mmoja kati ya wachezaji bora kabisa kwa sasa na anakoelekea anakwenda kuwa bora zaidi. Staa huyo wa Ufaransa alikuwa kwenye moto mkali katika fainali za Kombe la Dunia 2018 akifunga mabao matamu ikiwamo moja kwenye mechi ya fainali timu yake ilipoichapa Croatia 4-2 na kubeba taji hilo la dunia kwa mara ya pili katika historia yake. Mbappe ni mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wangependa kuwaona wakitua kwenye Ligi Kuu England.

Aleksandr Golovin

Kiungo matata kabisa wa Russia. Aleksandr Golovin ni mchezaji mwingine kijana mwenye mwonekano wa kuwa na maisha mazuri ya soka kwa siku za baadaye. Halitakuwa jambo la kushangaza kama atabamba uhamisho wa kujiunga na moja ya klabu za Ligi Kuu England katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Kama kinachoelezwa ni kweli, basi staa huyo ameripotiwa kukaribia kabisa kujiunga na Chelsea na hilo litaondoa kiu ya mashabiki kumwona kwenye Ligi Kuu England.

Benjamin Pavard

Kama ilivyo kwa Mbappe, kinda mwingine mwenye kiwango bora kabisa aliyeibeba Ufaransa katika fainali za Kombe la Dunia huko Russia ni Benjamin Pavard.

Umri wake ni miaka 22 tu na Pavard anacheza nafasi ya beki wa kati kwenye klabu yake ya Stuttgart msimu uliopita, lakini kwenye Kombe la Dunia alitumika kwenye beki ya kulia na Les Bleus. Pavard alishawahi kuhusishwa na Arsenal, lakini ni mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki watafurahi kuwaona kwenye Ligi Kuu England.

Ivan Perisic

Mfungaji wa bao matata kwenye fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa, hata hivyo, timu yake ya Croatia ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 4-2. Supastaa, Ivan Perisic alionyesha kiwango kikubwa kwenye fainali hizo zilizofanyika Russia.

Anatamba pia kwenye kikosi cha Inter Milan na Manchester United inahusishwa na mpango wa kuinasa huduma yake, ilijaribu kufanya hivyo kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana na inajaribu kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Utakuwa usajili bora akitua kwenye Ligi Kuu England.

Diego Godin

Mmoja kati ya mabeki bora kabisa wa kati duniani kwa sasa na pengine kuna nafasi finyu sana ya kumwona Diego Godin akiondoka kwenye kikosi cha Atletico Madrid, lakini kama hilo likitokea na akatua kwenye Ligi Kuu England, basi utakuwa usajili unaosubiriwa kwa hamu kubwa. Staa huyo wa kimataifa wa Uruguay ni mmoja kati ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia na utashangaa kwamba ni beki wa kati wa aina yake lakini hayupo Ligi Kuu England.

Hirving Lozano

Kinda mwingine matata kabisa anayesubiriwa kwenye Ligi Kuu England.

Hirving Lozano alionyesha kiwango kikubwa wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2018 alipokuwa katika kikosi cha Mexico.

Klabu za Ligi Kuu England ziliona uwezo wake kwenye fainali hizo na kumtolea macho zikitaka ajiunge kwenye timu zao, huku Arsenal na Man United zikiwahi kuripotiwa kuhitaji saini yake.

Ni mchezaji anayemudu kucheza ama winga au mshambuliaji kwenye kikosi chake cha PSV ya Uholanzi.

Mario Mandzukic

Kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, Mandzukic alikuwa na sura mbili.

Kwanza alijifunga kisha akafunga, huku timu yake ya Croatia ikichapwa na Ufaransa na hivyo kukosa ubingwa. Lakini, mshambuliaji huyo wa Juventus ni mmoja kati ya wachezaji wanaosubiriwa kwa hamu kubwa kwenye Ligi Kuu England.

Kuna kipindi aliwahi kuhusishwa na Man United na sasa baada ya ujio wa Cristiano Ronaldo huku Juventus, basi kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo akaondoka na kutafuta timu nyingine huku mashabiki wakisubiri kuona anatua kwenye Ligi Kuu England.