Sio ajabu Yanga kukiri uhaba wa fedha

Muktasari:

Jambo la pili ambalo ni vigumu kulikiri hadharani ni anapokumbana na kipigo kutoka kwa mwanamke. Mwanaume hata awe dhaifu vipi, akipigwa na mwanamke huwa hasemi, labda awe amekaribia kufa. Hakuna aibu kubwa kwa mwanaume kama hii.

KATIKA maisha ya kawaida, kuna mambo mawili tu ambayo mwanaume hupata aibu kubwa kuyazungumza hadharani. Kwanza ni pale anapokuwa na matatizo ya nguvu za kiume, hili anaweza kulisema kwa daktari tu, akibanwa zaidi atamweleza na rafiki yake wa karibu.

Jambo la pili ambalo ni vigumu kulikiri hadharani ni anapokumbana na kipigo kutoka kwa mwanamke. Mwanaume hata awe dhaifu vipi, akipigwa na mwanamke huwa hasemi, labda awe amekaribia kufa. Hakuna aibu kubwa kwa mwanaume kama hii.

Hata hivyo, mambo mengine kwa mwanaume ni ya kawaida tu. Mwanaume asipokuwa na fedha atasema ili apate msaada. Mwanaume akiwa na njaa husema ili apate chakula. Mwanaume wa kweli haoni aibu kueleza matatizo yake ili apate msaada.

Hakuna heshima kufa na matatizo yako moyoni, hasa ambayo yangeweza kupatiwa msaada. Hapa ndipo ninapotofautiana na Yanga kila siku.

Si jambo la ajabu kwa klabu ya Yanga kusema kuwa ina matatizo ya fedha. Ni jambo la kawaida kabisa kwenye taasisi kuwa na uhaba wa fedha. Yanga haijiendeshi kwa faida, hivyo tunatarajia kuona wakiwa na matatizo ya kifedha kila wakati. Si jambo kipya wala si la aibu.

Katika hali ya kawaida, mahitaji ya fedha ndani ya Yanga ni makubwa kuliko fedha zilizopo. Hata SportPesa wakiwapa fedha zote za udhamini, Vodacom na Azam TV wakawapa pia, bado hazitatosha.

Yanga ni klabu kubwa na ili kuendesha shughuli zake inahitaji fedha nyingi. Kulipa mishahara tu ya wachezaji, benchi la ufundi na sekretarieti inahitajika fedha ya maana. Si chini ya Sh1.5 bilioni kwa mwaka. Zinapatikana wapi fedha hizi?

Kugharimia shughuli nyingine za uendeshaji, maandalizi ya mechi, kambi, viwanja vya mazoezi na mengineyo inahitajika fedha nyingi pia. Si chini ya Sh1 bilioni kwa mwaka. Zinapatikana wapi fedha hizi?

Kuendesha Yanga sio jambo la mchezo mchezo. Yanga ni timu ya kimataifa na ina mahitaji makubwa. Kwa hapa Tanzania angalau Simba inakaribia gharama zake.

Ukizitazama gharama zote za kuendesha Yanga, utagundua klabu yao ina uhitaji mkubwa wa fedha. Mapato yote ya Yanga kwa mwaka hayafiki Sh2 bilioni, lakini inahitaji zaidi ya Sh3 bilioni kuendesha shughuli zake. Fedha za kujazia hapo zinatoka wapi? Uhaba lazima utakuwepo.

Ni nani anatoa fedha hizo? Wanajua wenyewe. Awali alikuwa anatoa aliyekuwa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, lakini sasa amejiweka pembeni. Ni nani amevaa viatu vya Manji? Hakuna.

Yanga kwa sasa inahitaji fedha, tena siyo kidogo. Lakini tatizo ni kwamba hawataki kusema ukweli. Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, anafahamu wanahitaji fedha nyingi tu. Katibu Mkuu, Charles Mkwasa, anafahamu wanahitaji fedha, lakini kwanini hawataki kuwaambia wanachama wao ukweli? Wanajua wenyewe.

Niwaambie tu sio jambo la ajabu kusema Yanga inahitaji fedha. Si ajabu kusema Yanga inadaiwa. Ni kawaida katika taasisi yoyote.

Tanzania tu kama nchi inadaiwa zaidi ya Trilioni 40. Nani anajali? Hakuna. Nchi ama taasisi kudaiwa si kitu cha ajabu.

Muhimu ni kusema ukweli na kuandaa mikakati ya kupata fedha, hicho ndiyo wanapaswa kufanya Yanga kwa sasa. Wakae na wanachama na mashabiki wao na kuwaambia ukweli kuwa timu yao haina fedha kwa sasa.

Kwa namna ninavyowafahamu wanachama na mashabiki wa Yanga, kuichangia timu yao haiwezi kuwa tatizo. Wapo watu wa Yanga ambao wako radhi kulala njaa lakini waipe timu yao fedha.

Hakuna anayetaka kuona timu yao ikiwa chini ya Simba, ni bora walale njaa. Kwanini viongozi wa Yanga hawataki kuwaambia wanachama na mashabiki wao ukweli? Wanajua wenyewe.

Hakuna ufahari kusimama na kusema Yanga haina tatizo la kifedha wakati uhalisia uko tofauti. Kwanini tunazidanganya nafsi zetu? Kwanini tunaficha matatizo ambayo yanaweza kupatiwa suluhu?

Tuache kuishi katika dunia ya kuogopana. Viongozi wa Yanga wasimame na kuwaambia wanachama wao ukweli, watapata msaada.