MAONI YA MHARIRI: Simba sasa iusimamie vyema mfumo mpya iwe mfano chanya

HATIMAYE klabu ya Simba imeingia kwenye mfumo wa hisa na kuachana na ule wa wanachama uliodumu klabuni hapo kwa zaidi ya miaka 80.

Kamati ya Zabuni ya klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, imemtangaza bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ kuwa mshindi wa tenda ya kuwekeza klabuni hapo, hivyo sasa atamiliki asilimia 49 ya hisa za klabu hiyo.

Awali, MO alihitaji asilimia 51 ya hisa huzo za klabu, lakini wanachama waliamua kuwa apewe asilimia 50 kabla ya Serikali kuweka kanuni kuwa mwekezaji mmoja haruhusiwi kuwa na zaidi ya asilimia 49 ya hisa.

Bila shaka kumekuwa na maridhiano baina ya MO, Simba na Serikali juu ya mfumo huo mpya ambao klabu hiyo sasa inauendea.

Mabadiliko hayo yanamaanisha kuwa Simba sasa itakuwa kampuni na siyo klabu tu kama ilivyokuwa zamani.

MO ameweka kiasi cha Sh20 bilioni ambazo zitawekezwa na kuanza kuzalisha faida kwa kila mwaka, fedha ambazo zitapatikana ndizo zitakuwa zikiendesha klabu hiyo.

Kwa upande wa wanachama, watamiliki asilimia 51 ya hisa za klabu, lakini hawajaweka fedha zozote. Katika hizo asilimia 51 za hisa, wanachama wamepewa mgawo wa asilimia 10 na nyingine zimewekwa akiba.

Ni wazi haya ni mageuzi makubwa katika soka la Tanzania, kwani wadau wengi wa mchezo huo nchini walikuwa wakiomba jambo hili litokee na hatimaye limefanikiwa.

Simba sasa inakwenda kujibadilisha na kuwa timu inayolenga zaidi kwenda kibiashara, huku ikitengeneza faida tofauti na kipindi cha nyuma ambapo kila mwaka ilikuwa ikipata hasara tu.

Hii inadhihirisha ni jinsi gani klabu hii imekuwa na uchu wa mafanikio na kujifananisha na klabu kubwa za Afrika ambazo zinajiendesha kitajiri na kupata mafanikio kisoka.

Simba ikiwa chini ya mfumo wa wanachama, ilishindwa kusimamia biashara zake, hivyo kuhitaji mfumo mpya ambao utaleta mabadiliko.

Klabu hiyo pia ilishindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, hivyo sasa uwekezaji huu unatarajiwa kuleta mabadiliko ambayo yataifanya timu hiyo iweze kushindana na klabu kubwa za Afrika.

Akizungumza baada ya kutajwa kuwa mshindi wa tenda hiyo, MO alisema anatamani kuifanyia mageuzi makubwa klabu hiyo, huku akiweka ahadi ya matumizi makubwa ya fedha ili kusimamia mageuzi hayo.

MO ameahidi ujenzi wa uwanja, hosteli, gym, mgahawa na vinginevyo ambavyo sasa vitaifanya timu hiyo iwe katika kiwango cha juu na kushindana na timu vigogo wa Afrika kama TP Mazembe, Esperance De Tunis na nyinginezo.

Hii ni nyota njema kwa Simba ambayo imekuwa na kiu ya kufikia kilele cha mafanikio hasa nje ya nchi.

Hili limedhihirika hata katika mapambano ambayo klabu hiyo imewahi kuonyesha katika mashindano ya kimataifa.

Pamoja na yote, hili ni jambo jipya kwenye soka la Tanzania hivyo tunahitaji kuwa watulivu kuona Simba itakwendaje katika mfumo  mpya.

Kitu kipya chochote huwa na changamoto zake, hivyo lolote ambalo litaikuta Simba lisitazamwe kwa jicho hasi, bali sehemu ya kufanyia marekebisho ili kuwa na mfumo bora zaidi.

Kila mdau wa soka na hasa mashabiki wa Simba wanatamani kuona mfumo huo mpya unaanza kwa kasi kwani wanaamini ni mfumo wa kisasa na unaoruhusu timu kuingiza pesa nyingi na hivyo kuweza kujihudumia kwa urahisi.

Hiyo itasaidia timu kujiimarisha katika kila idara kuanzia uongozi hadi timu na hivyo kuweza kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya nchini na kimataifa.

Tunaishauri klabu ya Simba kusimamia kwa misingi imara kile walichokubaliana, ili kutoa darasa kwa timu nyingine nchini nazo kwenda katika mfumo kama wao.

Tunatazamia Simba itakuwa kioo cha timu za ndani na nje, kuingia katika mabadiliko ambayo yatakuwa na tija kibiashara na kuongeza ajira nchini.

Mfumo huu pia utasaidia kukuza viwango vya mchezo wa soka nchini endapo utasimamiwa vizuri.

Tunawapongeza pia Simba kwa hatua hiyo kubwa katika klabu yao na tunawataki kheri katika utekelezaji.

Wapenda maendeleo ya kweli wapo nguma yao.