Simba kusajili dirisha dogo ni kuchezea tu pesa

Muktasari:

  • Simba imetimia kila idara. Imsajili mchezaji akacheze nafasi gani? Wakati mwingine pesa huwa zinawasha, lakini mabosi wa Simba watulie tu na fedha zao kwa sasa.

SIMBA inahitaji kufanya usajili wowote wakati huu wa dirisha dogo? Hapana, hakuna haja hiyo. Kama ikifanya usajili katika dirisha hili lililofunguliwa juzi na litakalokuwa wazi hadi Desemba 15, itakuwa ni kuharibu tu pesa zao.

Simba imetimia kila idara. Imsajili mchezaji akacheze nafasi gani? Wakati mwingine pesa huwa zinawasha, lakini mabosi wa Simba watulie tu na fedha zao kwa sasa.

Ukifanya tathimini ya ubora wa kikosi cha Simba kwa sasa, huoni sehemu ambayo wanahitaji kurekebisha. Kama umeiona niambie.

Tuanze na golini. Simba ina kipa bora zaidi mzawa, Aishi Manula. Amekuwa na makosa machache msimu huu, lakini bado anaendelea kuwa bora.

Kwa mechi alizocheza ni wazi nafasi yake haina shaka.

Manula anasaidiwa na Emmanuel Mseja katika benchi, lakini kipa mwingine wa viwango, Said Mohammed ‘Nduda’ yupo mbioni kupona na atarejea uwanjani. Simba inahitaji kusajili kipa? Hapana, iache matumizi mabaya ya pesa.

Tuwatazame mabeki wake. Upande wa kulia wana Erasto Nyoni na Ally Shomary. Wanaye pia Shomary Kapombe ambaye wameanza kumuundia zengwe. Upande wa kushoto wana Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Jamal Mwambeleko.

Beki ya kati ya Simba ina Juuko Murshid, Method Mwanjali, Yusuf Mlipili na Salim Mbonde ambaye ni majeruhi kwa sasa, lakini atarejea siku si nyingi. Wanaye pia James Kotei anayemudu kucheza nafasi hiyo.

Simba inahitaji kusajili beki? Hapana, wakimsajili atakwenda kucheza wapi? Mpaka sasa Mwambeleko hajacheza mechi yoyote. Mlipili amecheza mechi moja tu. Ally Shomary naye amekuwa hapati nafasi katika siku za karibuni. Kwa kifupi beki ya Simba imetimia.

Twende katika nafasi ya kiungo. Wana Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Haruna Niyonzima, Mwinyi Kazimoto na Said Ndemla ambaye wamemuweka sokoni.

Hapo bado hujamtaja Mohammed Ibrahim ‘MO’ ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa viwango vya juu nchini.

Mpaka sasa kuna mgogoro mkubwa katika nafasi ya kiungo, nani aanze kati ya Mkude na Kotei. Nani aanze kati ya Niyonzima na MO Ibrahim? Nyota wengine kama Kazimoto na Ndemla nafasi zao za kucheza ni finyu mno.

Simba inahitaji kusajili kiungo akacheze wapi? Kwanini tunakuwa na matumizi mabaya ya fedha kiasi hicho?

Kwanini tunataka kutumia pesa vibaya wakati huu ambao vyuma vimekaza? Simba tulizeni akili kwanza.

Ni kweli kwamba pesa ni ya kwenu na hatuwezi kuwapangia namna ya kuitumia, lakini si kwa kufanya usajili usio na tija.

Nafasi ya ushambuliaji ndiyo imesheheni mno. Una Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, John Bocco, Laudit Mavugo, Nicholas Gyan na Juma Liuzio, unasajili mchezaji mwingine akacheze wapi?

Tuacheni masikhara na pesa jamani. Unataka kusajili straika Simba akacheze wapi?

Ni kweli kwamba Bocco hajafunga sana, Mavugo hajafunga sana kama ilivyo kwa Liuzio na Gyan lakini siyo tatizo lao.

Simba inavyocheza sasa hata ikiletewa Romelu Lukaku na Harry Kane hawawezi kufunga mabao mengi.

Mfumo unaotumiwa na kocha, Joseph Omog, ndiyo unawabana mastraika. Timu yake inacheza na viungo wengi kwenye kila mchezo na kujikuta ikishindwa kutengeneza nafasi za kutosha kwa mastraika wake.

Simba inacheza na viungo wawili wakabaji hadi mchezo dhidi ya Njombe Mji, mastraika watafungaje?

Simba ni timu kubwa. Inatakiwa kucheza soka la kushambulia ikiwa nyumbani na siyo kujaza viungo wengi wasio na tija.

Kocha Omog aache kupanga kikosi cha kuwaridhisha watu fulani. Anahitaji kubadilika ili kuwapa mastraika wake kila mmoja nafasi ya kung’ara.

Kitu pekee ninachokiona kwa sasa ni Omog kubadilika, vinginevyo itabidi abadilishwe. Huwezi kuwa kocha wa Simba unapanga kikosi cha kujilinda dhidi ya Lipuli ama Majimaji, tena ukiwa nyumbani.

Simba haina haja ya kufanya usajili wakati huu wa dirisha dogo, labda kama wana pesa za kuchezea.

Yanga hakuna ubishi kwamba inahitaji kusajili mastraika wawili na beki mmoja wa kati. Azam hakuna ubishi inahitaji kusajili mastraika wawili. Ila kwa Simba hapana, waache kutumia pesa vibaya.

Nitashangaa kama Simba itafanya usajili kwenye dirisha hili, labda kama kuna watu wananufaika na usajili huo nyuma ya timu.