Simba, Yanga, Azam zinapowagombea wachezaji wa Mbao

KICHWA kinauma unapoona Simba, Yanga na Azam zinakesha usiku kucha kuwagombania wachezaji wa klabu ya Mbao. Inaacha maswali mengi nyuma yake. Kiasi inachekesha, lakini kuna ukweli unaofichwa.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara iliyomalizika, Mbao ilishika nafasi ya 12. Katika fainali za FA Mbao ilifika fainali. Mbao walikuwa wazuri au? Ni swali la kujiuliza.

Upande mmoja walinusurika kushuka daraja, upande mwingine wakafika fainali.

Huwa inatokea sana. Hata kwa wazungu huwa inatokea. Wakati mwingine kuna timu au makocha ni wazuri kwa mechi za michuano. Mara nyingi michuano ni kama mbio fupi (short sprint). Ligi ni kama mbio ndefu (marathon).

Kwa mtazamo wangu niliwaona Mbao wakicheza kitimu zaidi. Sikuwa najali sana uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Nilikuwa najali zaidi muunganiko wao wa kitimu na walinikosha jinsi walivyocheza na Simba katika pambano lao la raundi ya kwanza ya ligi. Wakaruhusu bao la jioni kabisa la Mzamiru Yassin.

Kama tunakubaliana kwamba Mbao walikuwa wazuri na walicheza vema, ilikuwaje wakashika nafasi ya 12 wakinusurika kushuka daraja? Kama walikuwa na wachezaji mastaa, ilikuwaje wakafika nafasi hiyo? Hapa ndipo tunapoanza kujipa majibu.

Kwanza, inawezekana wachezaji wa Kitanzania ni wale wale tu isipokuwa hali ya kiuchumi ndio ambayo inawatofautisha kati yao na wale wa Yanga, Simba na Azam.

Kwamba kama wachezaji wa Mbao wangekuwa na huduma zilezile za wachezaji wa timu kubwa za Dar es Salaam, basi si ajabu wangechukua ubingwa wa ligi.

Halafu pili, ni wakati wa kujiuliza kama ligi yetu inachezeshwa kwa usawa. Si ajabu Mbao walikuwa wanakutana na dhuluma nyingi kutoka kwa watu wa mpira na hivyo kujikuta wakifanya vibaya. Si ajabu tulikuwa hatuzitupii macho mechi zao. Labda walikuwa wanacheza vema katika mechi nyingi za mikoani lakini wakawa wanakumbana na dhuluma.

Lakini vile vile kuna hofu kubwa huwa inaingia. Wakati mwingine wachezaji kama wa Mbao wanaweza kuwa wazuri kitimu kuliko uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Labda klabu zetu zimefanya uchunguzi wa kina kugundua kuwa mastaa wa Mbao wanaweza kung’ara nje ya klabu yao.

Imewahi kutokea mara nyingi kuona wachezaji wanaotoka katika timu ambayo ilikuwa na uchezaji wa umoja zaidi kupwaya wanapokwenda katika timu ambazo wachezaji wake wanategemewa kutoa vitu vingi binafsi kuliko kucheza kitimu zaidi.

Halafu kuna swali la tatu. Inawezekana Mbao imeingia katika mkumbo wa kijinga wa kucheza kwa kukamia katika mechi kubwa halafu hawajiandai kwa mechi za kawaida. Labda ndio maana tabia hii imewapelekea kuwa wa 12.

Iangalie safari yao ya FA walipocheza mechi ya nusu fainali na Yanga, kisha fainali na Simba, mechi zote walikamia. Kama wangekuwa wanacheza vile kila mechi ya ligi si wangekuwa wanawania ubingwa? Hili ndio tatizo la timu zetu.

Hata hivyo, pamoja na yote haya bado inastaajabisha pia kuona Azam, Simba na Yanga zikiwawania kwa kasi wachezaji wa Mbao pengine kuliko timu ambazo zimemaliza ligi zikiwa juu ya Mbao katika msimamo, tena kwa mbali.

Inawezekana ni kitu kipya kwangu kwa sababu chukulia tu mfano wa timu zinazoshuka daraja katika Ligi Kuu England. Ni ngumu kwa wachezaji wa timu hizo kwenda katika klabu kubwa.

Wanaweza kuwaniwa na timu za mitaa ya kati kama West Ham, Newcastle, Everton lakini hawawezi kwenda Manchester United, Chelsea, Liverpool au Arsenal.

Hili pia linaashiria kwamba tunajitoa katika mbio za ubingwa za michuano mbalimbali ya kimataifa msimu ujao. Hawa akina Al Ahly, TP Mazembe, Etoile Du Sahel na wengineo watasajili mastaa kutoka katika klabu kubwa za Afrika kwa ajili ya kujiandaa vema na michuano ya kimataifa.

Wakati utaamua kuhusu kila kitu, lakini kwa sasa naendelea kutazama vita ya Yanga, Simba na Azam kugombania wachezaji wa Mbao na hata Toto Afrika kila kukicha. Mpira wetu una siri nyingi ambazo zimeendelea kujikita nyuma ya mapazia.

Nakumbuka wachezaji wa Tukuyu Stars walikimbiliwa baada ya kutwaa ubingwa mwaka 1986, hawa wa Mbao hadithi ni tofauti kidogo.