Siioni timu ya kuipa upinzani Man City

Muktasari:

Katika dirisha kubwa la uhamisho vilabu vingi vilijipanga vizuri sana. Na vilabu kama Manchester United, Chelsea na Manchester City wote walikuwa na timu katika karatasi yenye uwezo wa kushinda Ligi Kuu.

MSOMAJI, kabla msimu huu wa Ligi Kuu ya England kuanza wengi waliamini kwamba itakuwa ngumu kutabiri mshindi.

Katika dirisha kubwa la uhamisho vilabu vingi vilijipanga vizuri sana. Na vilabu kama Manchester United, Chelsea na Manchester City wote walikuwa na timu katika karatasi yenye uwezo wa kushinda Ligi Kuu.

Lakini, kutoka mwanzo wa msimu Manchester City ni timu pekee ambayo imeweza kutawala Ligi Kuu ya England.

Wikiendi iliyopita walikutana na watani wao wa jadi Manchester United na walishinda mchezo huu wakiwa ugenini. Tena kirahisi kabisa. Manchester City bado hawajapoteza mchezo katika Ligi Kuu na wameshawafunga Arsenal, Manchester United, Chelsea na Liverpool.

Na hivi sasa sioni timu yenye uwezo wa kuwafunga Man City. Man United bado wameshika nafasi ya pili lakini Man City wamewazidi pointi kumi na moja.

Katika msimu wowote pointi kumi na moja ni nyingi katika Ligi Kuu ya England lakini hususan katika msimu huu itakuwa ngumu kwa klabu vingine kuwafukuza Manchester City kwa kuwa timu hiyo haipotezi pointi hata dhidi ya vilabu bora kabisa nchini England.

Imebaki wiki mbili tu mpaka Krismasi na katika takriban kila msimu katika miaka 10 timu ambayo inaongoza Ligi Kuu baada ya Krismasi pia imeshinda Ligi mwisho wa msimu.

Na ni wazi kwamba Man City wataongoza Ligi baada ya Sikukuu ya Krismasi.

Manchester City chini ya uongozi wa Pep Guardiola wameonyesha mara kwa mara msimu huu kwamba wana uwezo wa kutawala mchezo kwa namna ya kipekee na kufunga magoli mengi sana dhidi ya timu yoyote ile.

Pep Guardiola alipoifundisha Barcelona nchini Hispania, Barcelona walifunga magoli mengi pia kwa sababu timu nyingi katika Ligi hiyo hazina uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa kujihami.

Lakini, kwa kweli Guardiola ameonyesha ubunifu wake kama kocha msimu huu kutokana na timu yake kufunga magoli mengi katika Ligi Kuu ya England ambayo ni ligi yenye timu nyingi zenye uwezo mkubwa wa kukaba na yenye kiwango kikubwa kuliko vilabu nchini Hispania.

Kwa namna moja au nyingine ninaamini kwamba Ligi Kuu ya England sasa itakosa ladha nzuri kutokana na kutokuwa na timu nyingine yenye uwezo mkubwa wa kuwapa Manchester City upinzani katika Ligi Kuu.

Lakini, pia itakuwa burudani kuona kama Manchester City wataweza kuchukua hata hatua nyingine kimpira na kama wataweza kushinda Ligi bila kupoteza hata mechi moja.

Timu hiyo ina nafasi kutengeneza historia kwa kuwa mpaka sasa ni timu ya Arsenal ya 2004 tu ambayo imeweza kushinda Ligi Kuu bila kufungwa.