STRAIKA WA MWANASPOTI: Serikali zetu zisaidie kukuza sekta ya michezo

Muktasari:

Mwanasoka siridhishwi kabisa kwa jinsi serikali hizo zinavyochukulia poa hali hii kwani zinaonekana kutulia tu huku tukishuhudia soka letu likizidi kudorora bila ya wao kujali.

Ndugu zangu, serikali ndio kila kitu katika nchi yoyote ile.

NDUGU msomaji, Jumanne ya leo nimeamua kuitumia kwa makusudi maalumu katika kushusha shoka langu la machungu kwa serikali zetu za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwanasoka siridhishwi kabisa kwa jinsi serikali hizo zinavyochukulia poa hali hii kwani zinaonekana kutulia tu huku tukishuhudia soka letu likizidi kudorora bila ya wao kujali.

Ndugu zangu, serikali ndio kila kitu katika nchi yoyote ile. Hivyo, kama viongozi wake hawafahamu chochote kuhusu michezo na hawatilii maanani fani hiyo, maana yake ni sawa na kusema katika nchi hiyo michezo ni kama imekufa.

Katika hali ya kawaida, michezo kwa asilimia kubwa hushirikisha vijana kwa maana ya uchezaji, na kwa hali ya sasa ya kidunia, michezo imegeuka kuwa ajira kubwa ikiwafaidisha wengi kitaifa na kimataifa pia. Hivyo, kwa kuzigatia kuwa katika nchi zetu hizi vijana ndio wengi zaidi, maana yake kujali michezo ni kuisaidia jamii.

Nina hakika kama serikali zetu zingejali michezo kwa kiwango kinachotakiwa, kwa utajiri wa vijana na vipaji tulivyonavyo, hakika si Kenya au Tanzania tu, bali ukanda mzima huu tungekuwa mbali sana kimichezo.

Na kwa kuwa nina uzoefu zaidi katika soka, hapa ningependa kuzungumzia zaidi mchezo huu. Ninasema hivi kwa kuwa ninapoona mtu au serikali inapuuzia soka, huwa inaniudhi sana.

Soka la sasa ni biashara, linahitaji wafadhili na wadhamini. Na hao wataingia katika soka iwapo watapata nguvu kutoka kwa serikali zetu.

Sasa angalia kichekesho cha Kenya. Sijui inakoelekea kisoka, wakati wenzetu wanayakumbatia makampuni yanayofadhili michezo, sisi ndio kwanza tunayakimbiza yasifanye hayo kwetu, halafu tunataka mafanikio ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Nikiwa ni mchezaji mstaafu nilikerwa sana na kuondoka kwa SuperSport katika kuifadhili Ligi Kuu Kenya. Kwani ni kampuni ya kurusha matangazo na kuonyesha soka katika runinga zetu.

Kuondoka kwake niliona kama wametuacha uchi wa mnyama. Wachezaji wetu wengi walikuwa wameanza kupata soko katika nchi nyingine kutoka na kuonekana katika runinga duniani kote. Kwa sasa imekuwa kikwazo kikubwa.

Ni kama wachezaji wametelekezwa baada ya SuperSport kukusanya virago vyake na kuondoka. Iwapo tungekuwa na serikali au wakuu wake wanaopenda soka, naamini mambo yasingekuwa yalivyotokea.

Haya kabla hatujakaa sawa, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilitunyang’anya haki ya kuandaa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) ambazo kwa sasa zinaendelea Morocco baada ya kupewa haki hiyo.

Ndio tumeukosa uhondo huo kwani yangetufaa kimichezo, kijamii na hata kiuchumi, lakini ndio hivyo tena.

Kama ilivyo kawaida yetu, Serikali ya Kenya iliahidi itajenga viwanja vitano vya kisasa katika awamu yake iliyopita, lakini mpaka unapoisoma makala hii hakuna hata uwanja mmoja uliojengwa, ndio maana hata Caf haikuwa na kigugumizi ilipotunyang’anya Chan.

Hivi unataka kuniambia tungekuwa na mkuu wa nchi ambaye hapati usingizi linapokuja suala la soka, mashindano hayo yangeota mbawa kwetu? Ah wapi nakwambia sasa hivi tungekuwa tunafurika katika viwanja vyetu kuangalia vipaji vya Afrika.

Kabla hata hatujapumua, wafadhali wengine wa Ligi Kuu Kenya SportPesa nao hao wanaondoka. Majuzi wamethibitisha hilo la kuachana na udhamini wao kutokana na serikali kuwapandishia kodi.

Ukiangalia kwa undani kabisa utabaini klabu nyingi nchini zimekuwa zikitegemea ufadhali wa SportPesa. Klabu za Gor Mahia na AFC Leopards zilikuwa zinaneemika zaidi kwa kulipiwa mishahara ya wachezaji wao kila mwezi. Klabu nyingi zimekuwa pia zikipata ufadhili wa kiasi fulani kutoka SportPesa. Hela ambazo Kwa kweli zimekuwa zikizisaidia klabu hizo kwa ukubwa sana. Serikali imewaweka kodi ya asilimia 35 ambayo Kwa wafadhili wanasema inawaangamiza kimaslahi. Ndugu zanguni. Tunaua soka letu ama vipi? Kama michezo isipoimarishwa, pale vijana wetu watakapokosa ajira nyingine tulizozizoea, watageuka kuwa wezi mitaani.