SPOTI DOKTA: Hatua za mchezaji kufuzu vipimo

Friday July 20 2018

 

NI kawaida kwa wapenda soka kujiuliza wachezaji walioshiriki fainali za Kombe la Dunia kule Russia watakuwa wanaafanya nini kwa sasa.

Ikumbukwe wachezaji wengi walioshriki fainali hizo wanacheza katika ligi kubwa zenye ushindani wa hali ya juu ikiwamo Ligi Kuu ya England (EPL), La liga, Ligi One, Bundesliga na Seria A.

Baadhi ya wachezaji walitolewa mapema katika fainali za Kombe la Dunia wengi wako mapumzikoni na kutuliza miili na akili ili kujiweka tayari na ligi hizo ambazo nyingi zinaanza mwanzoni mwa Agosti.

Wakati wakiwa mapumziko mawakala wa wachezaji wao wanakwea mapipa kukutana na Marais wa klabu ambazo zimeonyesha nia ya kuwanunua.

Wengine wakiwa mapumzikoni baada ya kununuliwa na klabu zao mpya wanatambulishwa na kupewa mikataba mipya na kusaini na hapo baaadaye wanarudi kuendela na mapumziko.

Kwa wale walionunuliwa kutoka klabu moja kwenda nyingine hutambulishwa katika klabu zao mpya, lakini mpaka kufikia hatua hii upo mchakato wa upimwaji wa afya wanapofaulu vipimo ndipo hapo baadaye hutambulishwa rasmi.

Mfano ni usajili uliotikisa ni wa Mchezaji Bora wa Dunia Cristiano Ronaldo alipohamia Juventus ya Italia kwa dau la Pauni 105 milioni.

Straika huyo aliyenunuliwa kutoka Real Madrid alifaulu vipimo vya afya na tayari ameisha tambulishwa kama mchezaji mpya wa Juventus.

Kwa kawaida kipindi hiki wachezaji wapya wanaponunuliwa ni lazima wafaulu vipimo vya afya ili biashara iweze kufanyika.

Leo nitawapa mchakato mzima wa upimaji wa afya za wachezaji wapya mpaka kufuzu vipimo na kununuliwa.

Kwa kawaida uchunguzi hufanyika katika vituo maalumu vya kisasa vyenye vifaa vya kisasa na unaweza kuchukua saa 12-24 iwapo taratibu zitafuatwa.

Uchunguzi huu hutegemeana na umri, afya kwa jumla na historia ya familia na mienendo na mitindo ya kimaisha ikiwamo kama mwanamichezo anatumia tumbaku au kilevi chochote.

Uchunguzi hujikita zaidi matatizo ya mfumo wa moyo na mzunguko wa damu, mfumo wa upumuaji, mfumo wa fahamu, mfumo wa mifupa na misuli na mengineyo. Pia, unaweza ukaanzia katika historia ya mwanamichezo kama ana dalili zozote au historia ya magonjwa sugu au ya kurithi katika familia yake.

Vilevile uchunguzi wa kimwili ikiwamo upimaji wa shinikizo la damu, kasi ya upumuaji, joto la mwili, mdundisho wa damu katika mshipa. Vipimo vya uzito, urefu, na upimaji wa ukubwa wa misuli na mwili pia hufanywa kubaini uzito mkubwa au mdogo.

Vipimo vya kisasa huweza kutumika kuweza kubaini matatizo ya kiafya yaliyojikita kwa ndani zaidi ikiwamo vipimo vya picha za CT na MRI. Kwa upande wa uchunguzi wa mwili unaweza ukahusisha maabara na vipimo vya picha.

Vipimo kama vya wingi wa damu na kundi lake, kipimo cha picha nzima ya damu, kiwango cha sukari ya mwili, vipimo vya maambukizi ya magonjwa ya kujamiana na VVU.

Vilevile uchunguzi wa picha za mwili ikiwamo picha ya kifua ya X-ray, vipimo vya uchunguzi vya moyo ikiwamo kipimo cha picha ya moyo na kipimo cha kuona ufanyaji kazi wa moyo.

Fifa iliweka mwongozo wa uchunguzi wa kiafya wa kina wa moyo hasa baada ya matukio ya wanasoka kufariki viwanjani.

Uchunguzi wa moyo ni muhimu sana, kwani inahofiwa endapo mchezaji atakuwa anashiriki michezo matatizo katika mfumo wa damu na moyo unaweza kumsababishia moyo kusimama na kupata kifo cha ghafla.

Majaribio mbalimbali ambayo hufanyika katika maabara maalumu ambazo huwa na mashine za kukimbilia huweza kubaini kasi ya mwanamichezo huyo kama anakidhi kasi inayotakiwa awe nayo.

Vilevile hufanyiwa majaribio ya mazoezi ya viungo kuona uimara wa mwili kwa jumla, majaribio kuona uwezo wake wa kuona, kutumia akili na kufanya maamuzi.

Wataalamu wa afya za wanamichezo ndio wanawagundua wanamichezo kama kasi na viwango vimepungua. Hivyo, hatua huweza kuchukuliwa kuikabili hali hiyo na kumsaidia mwanamichezo kurudisha kiwango.

Uchunguzi hubaini uwepo wa majeraha ya mara kwa mara yasiyopona, hivyo kumpunguzia ufanisi na kiwango mchezaji.

Ugunduzi wa hili unasaidia kumpa ushauri na matibabu ya majeraha yake. Uchunguzi wa kiafya ndio huweza kubaini mchezaji kama ana uzito mkubwa au uzito na uimara wa misuli unapungua katika eneo fulani la mwili.

Mambo kama haya yanapogundulika ndipo wanamichezo wanapoweza kupewa msaada wa ushauri ikiwamo mazoezi ya ‘gym’ ya kujenga mwili kwa wale ambao misuli imekuwa dhaifu huweza kupewa mazoezi maalumu.

Kwa wale wenye uzito mkubwa hupewa ushauri wa kuudhibiti ikiwamo kuacha kula vyakula vya mafuta mengi, wanga na sukari kwa wingi. Uchunguzi huu huweza pia kubaini kasoro za kimaumbile ya mwilini ambazo zinaweza kumfanya mchezaji kuwa wa kiwango cha kimataifa.

Wataalamu wa afya huwa na uwezo wa kugundua matatizo ya kisaikolojia na kitabia kwa wachezaji ikiwamo ulevi wa kupindukia, uvutaji sigara na mifarakano ya kifamilia.

Uchunguzi wa kiafya hubaini mchoko hasa baada ya mchezaji kutumika kupita kiasi. Wanasoka wanaposhiriki michezo mikubwa hukabiliwa na matatizo haya ikiwamo majeraha ya misuli.

Uchunguzi wa kiafya wanaofanyiwa wanasoka ndiyo unatoa mustakabali wa mwanasoka kununuliwa na klabu, hivyo unapoona mchezaji ametambulishwa jua tayari amefaulu vipimo vya afya kama ilivyo kwa Ronaldo na wengineo.