MAONI YA MHARIRI: Ratiba ya Kombe la Mapinduzi inaumiza, ni vizuri ikatazamwa

MASHINDANO ya Kombe la Mapinduzi yanaendelea visiwani Zanzibar kwa mechi za hatua ya makundi kuchezwa.

Mechi hizo zinachezwa kuanzia saa nane mchana hadi saa nne usiku. Kila siku inachezwa michezo mitatu ikiwa ni juhudi za kumaliza mashindano hayo mapema.

Mwaka huu Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kimezipa nafasi timu 11 ambazo zimegawanywa katika makundi mawili. Kundi moja lina timu sita wakati jingine lina tano.

Kwa upande wa Bara, mbali na Simba na Singida United, tumewakilishwa pia na timu za Azam na Yanga.

Simba pekee ndiyo iliyoshindwa kuanza vizuri mashindano hayo baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwenge ya kule Wete, Pemba lakini jana Alhamisi usiku ilirejea uwanjani kujaribu bahati yake tena dhidi ya Jamhuri.

Yanga iliifunga Mlandege mabao 2-0 na ilikuwa ikicheza na JKU huku Singida United na Azam zikianza kwa kishindo zaidi kwa kushinda mechi za mwanzo tena kwa ushindi mnono. Azam imeendeleza ubabe wake wa safu ya ulinzi kwa kutoruhusu bao kwenye mechi zake mbili za kwanza.

Hakuna shaka mwaka huu timu za Bara zitaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kwa kucheza nusu fainali pamoja na kutwaa ubingwa huo.

Ushindani wa timu hizo zinazopambania taji la Ligi Kuu Bara unaonekana kuwa mkubwa tofauti na zile za Zanzibar ambazo zimekuwa vibonde kwao na mara nyingi kuishia katika hatua ya makundi.

Ukiachana na matokeo ya uwanjani, kuna tatizo moja ambalo limejitokeza katika mashindano ya mwaka huu. Ratiba ya michuano hiyo imekuwa mbovu kulinganisha na miaka mingine yote.

Kipindi cha nyuma mechi za Mapinduzi zilikuwa zikichezwa kila baada ya siku mbili, lakini mwaka huu timu zimekuwa zikicheza kila baada ya siku moja.

Mfano Simba ilicheza na Mwenge siku ya Jumanne lakini wapinzani wao hao wakarejea tena Uwanjani juzi Jumatano kucheza na URA. Yaani timu hiyo ilicheza mechi mbili ndani ya masaa 24. Ni hatari sana.

Jamhuri ya Pemba ilicheza na Azam juzi Jumatano na jana ikarejea tena uwanjani kucheza na Simba. Yanga ilicheza jana jioni na JKU na leo inacheza tena na Taifa Jang’ombe. Hatufahamu watu wa ZFA waliwaza nini, ila inasikitisha sana kuona mashindano hayo ya Mapinduzi yamefikia hatua hii ya michezo kuchezwa kila siku.

Hivi majuzi tumeona makocha wa Ligi Kuu ya England (EPL) hasa wa vinara Manchester City, Pep Gurdiola akilalamikia ratiba ya wakati wa sikukuu ambayo hutoa mapumziko ya siku mbili tu kwa kila mchezo.

Tukimnukuu alisema: “Ratiba hii inawaumiza wachezaji. Sote tuko hapa kwa ajili ya wachezaji hawa lakini tunashindwa kuwajali. Mchezaji hawezi kuwa fiti kwa kucheza kila baada ya siku mbili. Wachezaji wanapata majeraha, wanaumia,” mwisho wa kumnukuu.

 Kitaalamu, imekuwa ikishauriwa michezo ya ushindani inatakiwa kupishana angalau saa 72 (siku tatu) ili kutoa fursa kwa wachezaji kupumua. Ili kulinda pia afya za wachezaji hao ambao ndiyo injini ya mpira wenyewe wa soka.

Misuli inachoka na hata utimamu wa mwili wake unapungua.

Kwa kifupi, ratiba ya mashindano ya Mapinduzi inawaumiza wachezaji na haikupaswa kuwa kama ilivyo. Inashangaza kuona makocha wa timu shiriki waliikubali ilihali wanajua madhara yake.

Ni wazi Kamati ya Ufundi ya ZFA haikufanya kazi yake ipasavyo kwa kushauri maboresho ya ratiba hiyo.

Kama ni lazima mashindano hayo yamalizike Januari 12, ni vizuri wakapunguza idadi ya timu shiriki au kuongeza siku za kuanza mashindano kuliko kuweka timu nyingi ambazo zinawaumiza wachezaji.

Kwa upande wa timu za Ligi Kuu Bara ambayo itaendelea siku nne tu baada ya kutoka kwenye mashindano hayo, zitakumbana na changamoto kubwa ya kuupata ubora wa nyota wake ambao watakuwa wamechoshwa na mashindano hayo. Tunapenda kuikumbusha ZFA kuwa pamoja na wao ndio wenye haki na michuano hiyo, watengeneze ratiba ambayo itaendana na uhalisia na siyo kuziumiza timu na wachezaji wake. Isifikie hatua timu zikaona mashindano hayo ni ya kupoteza muda au adhabu kwao na kukosa msisimko.