ROHO NYEUPE: Usajili umeipa Simba kikosi kipana, Yanga kikosi cha ushindani

Friday August 4 2017

By GIFT MACHA

SIMBA na Yanga, kama ilivyo kwa timu nyingine za Ligi Kuu Bara, nazo ndio zipo mwishoni kabisa katika harakati za usajili kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano. Dirisha la usajili kwa wachezaji wa ndani litafungwa keshokutwa Jumapili. Usajili uliofanyika mpaka sasa umezipa Simba na Yanga makali tofauti. Simba imepata kikosi kipana wakati Yanga imepata kikosi bora cha kwanza. Unajua ni kwa nini? Twende pamoja.

Tuanze na Yanga. Usajili wa awamu hii kwa wana Jangwani hao umewaimarisha zaidi katika kikosi cha kwanza. Unataka kubisha? Usiwe na papara.

Yanga sasa inakuwa timu yenye kikosi imara zaidi cha kwanza kuliko timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu. Unaweza kukipanga kikosi chao kama ifuatavyo.

Kipa atakuwa Youthe Rostand, mtu mmoja makini na anayeifanya kazi yake kwa utulivu wa hali ya juu. Amesajiliwa kutoka African Lyon iliyoshuka daraja.

Beki ya kulia itakuwa chini ya Juma Abdul na kushoto ni Mwinyi Haji, wote uwezo wao unafahamika. Wakiwa katika ubora wao ni wachezaji makini.

Beki ya kati kama ataongezwa Mnigeria Herry Tony Okoh basi atacheza yeye sambamba na Kelvin Yondani. Kama hataongezwa, basi Yondani atacheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Ni wachezaji wenye uzoefu mkubwa.

Katika safu ya kiungo ni wazi sasa itakuwa chini ya Thaban Kamusoko, Tshishimbi Kabamba na Raphael Daudi ambao wote ni wa viwango ya juu.

Kwenye ushambuliaji watakuwa Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma na Amissi Tambwe, wote hao ni hatari wanapocheza eneo la mwisho. Bila shaka unaweza kuona kikosi cha kwanza cha Yanga kina nguvu kubwa mno. Tatizo ni Yanga haina kikosi kipana cha kuhimili mashindano mengi. Kuna tofauti kubwa sana ya viwango vya wachezaji wanaoanza na wale wa benchi.

Mfano katika beki ya kati unaweza kuona kuna tofauti kubwa ya viwango vya Cannavaro na Yondani dhidi ya Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’. Ikitokea mmoja anaumia ni pengo la wazi.

Dante ana uzoefu, lakini amekuwa na makosa katika hesabu zake. Anashindwa kujua hesabu za adui vizuri na ndiyo sababu mara nyingi akicheza Yanga huwa inaruhusu bao. Ninja bado hana uzoefu na Ligi Kuu Bara na hajatengeneza kombinesheni na mtu yeyote katika beki hiyo ya kati. Hana uzoefu na mechi za kimataifa pia. Kwenye kiungo bado kuna tofauti kubwa kati ya Said Juma ‘Makapu’ na wale wanaoanza. Ikitokea Kamusoko ameumia ni wazi safu ya kiungo itapwaya hasa kama mechi inayofuata itakuwa ngumu. Kwa upande wa washambuliaji wa pembeni Kocha George Lwandamina, bado ana kazi kubwa ya kuwaimarisha Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi.

Nyota hawa wamekuwa na viwango vya kawaida. Hakuna anayeweza kufikia makali ya Simon Msuva ama Deus Kaseke (wote hao wameondoka).

Ibrahim Akilimali bado si mchezaji wa kumtegemea sana. Hajawahi kucheza Ligi Kuu katika nchi yoyote na ndiyo anaanzia hapo Yanga.

Kwa roho nyeupe kabisa Yanga ina kikosi imara cha kwanza ila kwa waliopo benchi bado si wa daraja la juu sawa na wale wanaoanza. Kutabiri kikosi cha kwanza cha Yanga ni rahisi kama kutafuna mkate.

Kwa Simba kazi ipo. Simba haina kikosi imara cha kwanza, ni tofauti na Yanga lakini ina kikosi kipana kweli kweli. Simba inaweza kubadili kikosi kizima na bado ikafanya vizuri. Kwenye nafasi ya kipa akianza Aishi Manula ama Said Mohammed ‘Nduda’ ni sawa tu. Wote ni makipa wa kiwango cha juu.

Wote ni makipa wa Taifa Stars. Kwenye beki yao ndipo kwenye chaguo pana zaidi. Upande wa kulia anaweza kuanza Ally Shomary, Erasto Nyoni ama Shomary Kapombe. Wote ni mabeki wazuri.

Kwa upande wa kushoto anaweza kuanza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ama Jamal Mwambeleko, wote ni mabeki mahiri.

Beki ya kati anaweza kuanza Method Mwanjali na Juuko Murshid na nje wakawa Salim Mbonde na Yufus Mlipili. Nyoni na James Kotei wana uwezo wa kucheza nafasi hii pia.

Ina upana wa kutosha. Kwenye kiungo wote wapo vizuri. Yupo Kotei, Jonas Mkude, Said Ndemla, Mzamiru Yassin na Haruna Niyonzima. Kocha ana chaguo pana mpaka anapata mchecheto. Akianza yeyote ni sawa tu.

Eneo la mbele lina Nicholas Gyan, John Bocco, Emmanuel Okwi, Mohammed Ibrahim, Shiza Kichuya na Laudit Mavugo. Wote ni wachezaji wa viwango vya juu. Akianza yeyote ni poa tu.

Simba inaweza kubadili hata kikosi kizima na bado ikapata matokeo mazuri, Yanga haiwezi kufanya hivyo. Ila Yanga ina kikosi cha kucheza mechi kubwa na kupata matokeo, cha Simba bado.

Mwishowe mbinu za makocha Joseph Omog na Lwandamina zitakuwa na maana kubwa. Omog ana kazi ya kuchagua wa kuanza, Lwandamina ana kazi ya kuhakikisha wachezaji wanaoanza wanakuwa fiti wakati wote.