ROHO NYEUPE: Hivi jamani, tutazibeba Simba na Yanga hadi lini?

Friday December 8 2017Gift  Macha

Gift  Macha 

By GIFT MACHA

SOKA la Tanzania limekaa kiupendeleo sana. Simba na Yanga zimekuwa kama watoto wa baba na hawaguswi ovyo, hata kama wanakosea. Tumezigeuza timu hizi miungu watu. Kwanini tunaukosea heshima mpira wa miguu?

Kanuni za Ligi Kuu zimekuwa zikipindishwa kisa Simba na Yanga. Watu wenye akili timamu wamekuwa wakiongea ujinga kisa Simba na Yanga. Tutazibeba timu hizi mpaka lini? Kwanini tunaweka akili zetu mfukoni kwa ajili ya timu hizo ambazo hazina hata viwanja vya mazoezi?

Nimekuwa nikifuatilia Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu sasa. Kuna dalili za upendeleo kila siku. Tukio likifanywa na mchezaji wa Simba ama Yanga linaonekana la kawaida, lakini mchezaji wa timu nyingine ataonekana shetani.

Kumekuwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu kwa wachezaji wa Simba na Yanga lakini hayachukuliwi hatua ila yakitokea kwa wachezaji wa timu nyingine adhabu kali zimekuwa zikitolewa.

Ni lini mchezaji wa Simba ama Yanga alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya timu nyingine za kawaida? Unafikiri hawafanyi makosa? Hapana, wanafanya ila ndiyo hivyo.

Hivi majuzi Yanga ilicheza na Prisons ya Mbeya na kilichotokea Mungu ndiye anayejua. Kwanza mchezaji wa Prisons, Lambert Sabiyanka alimpiga kiwiko beki wa Yanga, Juma Abdul, mwamuzi akamtoka kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja. Mwamuzi alifanya hivyo japo lilikuwa ni tukio ‘jepesi’ ambalo lilistahili tu kadi ya njano.

Hilo halikuwa tatizo sana. Baada ya muda kidogo, mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa alimpiga kiwiko mchezaji mmoja wa Prisons, tena kwa makusudi lakini mwamuzi akakausha. Marudio ya picha za video yanaonyesha mwamuzi hakuwa mbali sana na tukio hilo lakini alichofanya ni kwenda kuuliza kwa mwamuzi wa akiba.

Mwamuzi wa akiba naye akasema hajaona licha ya kwamba alikuwa karibu pia. Yawezekana ni kweli mwamuzi hakuona tukio hilo, lakini inatia wasiwasi hasa kwa namna picha za marudio zinavyoonyesha.

Hilo pia siyo tatizo kubwa sana. Tatizo zaidi ni kwamba mpaka sasa Chirwa hajachukuliwa hatua yoyote licha ya kwamba tukio lake limeonekana kuwa la kawaida. Watendaji wote wa ligi wana picha hizi za marudio nilizoziona mimi pale Azam TV.

Tukio la Chirwa linafanana na lile la kipa wa Mbeya City, Owen Chaima ambaye amesimamishwa. Chaima alimpiga kibao aliyekuwa straika wa Azam, Yahya Mohammed. Mwamuzi hakuona tukio hilo lakini picha za marudio ya TV zilionyesha.

Chaima alisimamishwa siku chache tu baada ya tukio lake na sasa anasubiri hukumu ya kamati ya nidhamu. Kwanini Chirwa hajaadhibiwa mpaka sasa? Pengine kwa kuwa anacheza Yanga.

Yawezekana Kamati ya Saa 72 haijakaa mpaka sasa, lakini kadiri muda unavyokwenda, napata mashaka juu ya uamuzi wa kamati hiyo iliyoshikilia hatma ya soka letu.

Mapema msimu huu beki wa Majimaji, Juma Salamba alimpiga kiwiko mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Martins kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo uliochezwa Uwanja wa Majimaji Songea. Tukio hilo halikuonwa na mwamuzi.

Picha za marudio zilionyesha namna Salamba alivyotenda tukio hilo la utovu wa nidhamu. Ni kama tu Chirwa alivyomfanyia mchezaji wa Prisons. Salamba alisimamishwa na baadaye kuhukumiwa na Kamati ya Nidhamu. Kwanini kwa Chirwa inachelewa?

Salamba alihukumiwa kwa marudio ya picha za video. Chaima alihukumiwa kwa marudio ya picha za video. Kwanini siyo Chirwa? Pengine kwa kuwa anaichezea Yanga.

Msimu uliopita aliyekuwa beki wa Simba, Abdi Banda alimpiga kiwiko nahodha wa Kagera Sugar, George Kavila. Kanuni ilikuwa inasema wazi kosa la kupiga adhabu yake ni kufungiwa mechi zisizopungua tano. Hata hivyo, suala la Banda lilimalizwa kisiasa tu eti kisa anacheza timu ya Taifa ya Tanzania.

Msimu huohuo tena wachezaji wa Yanga, Obrey Chirwa, Deus Kaseka na Saimon Msuva walifanya makosa ya utovu wa nidhamu kwenye mchezo dhidi ya Mbao FC. Walimsukuma mwamuzi kama vile wanataka kumpiga.

Adhabu yao ilikuja kutolewa miezi mitatu baadaye, tena kwa kuungaunga.  Matukio mengi ya wachezaji wa Simba na Yanga ndivyo yanavyomalizwa.

Ninasubiri kuona Chirwa akiadhibiwa.

Nasubiri kuona wachezaji wa Simba na Yanga wakiadhibiwa kila wanapovunja kanuni. Haki ndivyo ilivyo. Ina kawaida ya kuchomachoma pande zote.