NJE YA BOKSI: Pesa za usajili Ulaya klabu zinatisha

Muktasari:

Takwimu zilizotolewa na FIFA mwaka 2008 zilionyesha watu million 226 wameshawahi au wanacheza soka la ridhaa(Amateur) ama kwa kulipwa(professional).

Umaarufu wa soka duniani umekua kwa kasi sana na hili limesaidiwa zaidi na mchezo huo kutumiwa kama njia ya kutangaza biashara za makampuni makubwa yenye ushawishi.

Takwimu zilizotolewa na FIFA mwaka 2008 zilionyesha watu million 226 wameshawahi au wanacheza soka la ridhaa(Amateur) ama kwa kulipwa(professional). Ligi kubwa kule Ulaya kama lEPL imezigharimu kampuni za kurusha matangazo ya televisheni ya Sky Sports na BT Sport pauni bilioni 5 ili kupata haki ya kurusha matangazo kwa miaka mitatu tu.

Kwa pesa ya namna hiyo timu ilioshika mkia na kushuka daraja msimu wa 2016-17 (Sunderland) iliingiza Pauni milioni 93.5, kiasi hicho ni kikubwa kuliko zawadi anayopata bingwa wa Bundesliga, La Liga au Serie A kule Italia.

Mastori leo yanaelezea wachezaji ambao ingekua pesa zao za uhamisho zinapokelewa na nchi zao moja kwa moja basi gawio kwa kila raia lingeleta faida zaidi.

Uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham hotspurs kuelekea Real Madrid kwa takribani $122m, pesa hizo zingegawanywa kwa kila raia wa Wales basi kila mtu angepata angalau $39 yaani Sh. 85,000 kila raia wa Wales.

Usajili wa $3m wa mchezaji raia wa Liechtenstein Maro Frick kutoka klabu ya Arezzo kwenda Hellas Verona mwaka 2002.

Kama kiasi hicho kingegawanywa kwa raia takribani 36,200 wa nchini kwake basi kila mmoja angepata $83 (Sh. 183,000). Mastori yanadai pia uhamisho wa $10.8m wa mchezaji mzaliwa wa Greenland, Jesper Gronkjaer(Alichezea Denmark) kuelekea Chelsea. Kiasi hicho kingegawanya kwa raia 57,000 wa Greenland kila mmoja angepata angalau $189 (Sh. 415,000).

Hapa kwetu Afrika wapo wachezaji waliouzwa bei ghali sana ila kutokana na idadi kubwa ya raia katika nchi zetu bado mgawanyo wa fedha hizo hautakua wa tija sana, ila kama tukiangalia mchango wa pato la mtu mmoja mmoja (Per Capita GDP) huko nchini Togo mwaka 2009, kwa wastani mtu mmoja alikua akiishi kwa $1,100 kwa mwaka, hio ni sawa na $3 kwa siku.

Uhamisho wa mchezaji Emmanuel Adebayor kutoka arsenal kwenda Man city kwa $25m ungefanya kila raia 7.6 millioni wa Togo kupata $3, yaani hela ya kujikimu kwa siku inayotambulika na Serikali ya Togo.