PORT SAID Mzuka wake wa soka usipime!

Muktasari:

Kutoka hapa kwenda Israel ni umbali wa Km300 tu. Ni sawa na mwendo wa kutoka Dar es Salaam kwenda Gairo ama Handeni.

NI umbali wa zaidi ya Km 6,200 kutoka Dar es Salaam hadi hapa Port Said, Misri. Kwa safari ya ndege ni saa karibu sita hewani. Ni mwendo wa maana. Mji huu upo karibu zaidi na Israel. Kutoka hapa kwenda Israel ni umbali wa Km300 tu. Ni sawa na mwendo wa kutoka Dar es Salaam kwenda Gairo ama Handeni.

Umbali huo mrefu wa kutoka Tanzania umesababisha maisha hapa yawe tofauti sana na yale ya Bongo, hasa ya mpira.

Tuliwasili mjini hapa alfajiri ya juzi Alhamisi, lakini picha iliyojionyesha mjini hapa ni ya kipekee.

Wakati tukiingia Mji wa Port Said majira ya saa 12.30 asubuhi tulistaajabu tuliyoanza kuyaona. Kwenye moja ya mitaa ya mji huu kulikuwa na watoto wamefunga mtaa huo wakicheza mpira. Inashangaza sana.

Ilikuwa ni asubuhi sana na baridi ilikuwa kali kama ile ya maeneo ya Mbeya na Songea hivi, lakini watoto hao waliamka kucheza mpira, picha niliyopata inafanana na ile niliyozoea kuiona mtandaoni katika mitaa ya Brazil.

Tena kilichostaajabisha zaidi ni kwamba watoto hao walikuwa wakicheza kwenye barabara ya lami. Waliamka muda huo kwa kuwa wakazi wengi huwa bado wamelala na mitaa mingi imepoa. Wangecheza saa ngapi?

Mji wa Port Said umejaa maghorofa karibu kila mahali. Sehemu nyingi zina makazi ya watu na maeneo ya kucheza soka ni machache. Sehemu nyingi pia zina viwanda.

Viwanja vya kucheza soka hapa ni vichache kwelikweli, sio kama ilivyo Dar es Salaam ama mikoa mingine nchini ambako unaweza kukuta vipo kwa wingi kidogo. Bahati nzuri, watoto wa hapa wanapenda sana soka hivyo hulazimika kutafuta namna ya kucheza ikiwemo kuamka alfajiri hiyo. Inafurahisha sana.

Cha kuvutia zaidi, watoto wanapokwenda sehemu yoyote kwa mtoko hubeba mpira. Kwenye Hotel ya Nora Style ambayo Simba imeshukia mjini hapa watoto walipokuja kwenye chakula cha usiku na wazazi wao walibeba mpira wao pia. Walitumia muda mwingi kucheza nje ya hoteli na hakuna aliyewakataza.

Mwenyeji wangu, Daruwesh ananieleza viwanja ni tatizo kubwa hapa Port Said, hivyo watoto hulazimika kucheza katika maeneo ambayo wanaona kuna nafasi ikiwemo barabarani.

“Hapa mtu akinunua eneo la kujenga nyumba kama hana fedha anafanya tu biashara ya soka. Anatengeneza hapo uwanja mzuri wa soka kisha vijana wakija kucheza wanalipia kwa kila saa moja.

“Mtu anaweza kufanya hivyo kwa muda kisha akawa anakusanya fedha za kujenga. Vijana hapa wanapenda sana soka, utakuta wanapambana kupata muda wa kucheza hapo,” anaeleza Daruwesh.

Kwenye Uwanja wa Al Masry ambako Simba ilikwenda kufanya mazoezi siku ya Alhamisi palikuwa na watu wengi pia. Kuna viwanja vinne vidogo na kimoja kikubwa ambacho ndicho kilitumiwa na Simba.

“Kule kwenye viwanja vidogo watoto wanalipia ili kufanya mazoezi. Kuna ambao wanacheza timu za vijana za Al Masry pia wanatumia hapo kufanya mazoezi.

“Msimu wa joto mambo huwa moto zaidi, watoto hubadilishana tu muda wa kucheza hadi saa 10 alfajiri ndipo uwanja unafungwa,” anaeleza Daruwesh ambaye anazungumza Kiswahili na Kiarabu kwa ufasaha kwani ameishi mjini hapa kwa miaka zaidi ya 15 sasa.

USIKU NDO KUMEKUCHA

Nchi za watu zina mambo. Hapa Port Said watu ni wachache sana mitaani wakati wa mchana, lakini usiku mambo ni moto.

Mwenyeji wangu mwingine hapa Imam ambaye ni Mwandishi wa Habari wa kituo kimoja cha televisheni, anasema mchana watu wanakuwa bize na shughuli zao hivyo usiku ndio wanatoka kufanya manunuzi na kula bata kimtindo.

Tulizunguka mji wa Port Said kuanzia saa4-6 usiku na kustaajabu yale tuliyoyaona. Watu walikuwa ni wengi kweli kweli. Maduka mengi yalifunguliwa muda huo na watu walikuwa bize kufanya manunuzi.

Kinadada walitembea kwa makundi ya watu watatu ama wanne na kuzunguka huku na kule huku wakiwa wamevalia mavazi mazito ili kujikinga na hali ya baridi. Kwenye migahawa ndipo kulikuwa na watu wengi zaidi. Familia nyingi hapa zinapenda mitoko ya usiku na hutoka wote kwa pamoja.

Kinachostaajabisha, ni nadra sana kukuta vijana wa kike na kiume wakiongozana kwa pamoja. Wanaume walikuwa kwenye makundi yao na wanawake nao walitembea kivyao.

Wengi pia wana usafiri hivyo hubebana wanne ama watano kwa ajili ya mitoko kwani usafiri wa daladala upo kwa kiwango cha chini sana hapa Port Said.

Saa 5 usiku ndipo barabara zao zilianza kuwa na foleni. Kulikuwa na magari yaliyobeba maharusi kwenda kwenye sherehe yakipita pia huku wakishangilia.

Watoto wadogo pia walikuwa ni wengi na ni kama hakuna mtu aliyekuwa anataka kulala. Imam ananieleza kuwa, hapa maduka mengi hufungwa kuanzia saa nane usiku lakini kwa Cairo biashara hufanyika kwa saa 24.

Kinachofurahisha zaidi, kwenye maeneo ya wazi tuliyopita muda huo wa usiku kulikuwa na watoto wakicheza soka pia. Kwenye barabara zisizo na pilika pia kulikuwa na watoto wakicheza soka.

AL MASRY YAREJEA

Imam ananieleza Simba itacheza na Al Masry kwa mara ya kwanza leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Port Said tangu ufunguliwe.

Uwanja huo ulifungiwa mwaka 2012 baada ya mashabiki wengi kufariki dunia zilipotokea vurugu wakati zikicheza Al Ahly na Al Masry. Tangu hapo Al Masry ilikuwa ikicheza kwenye viwanja tofauti nje ya mji, lakini uwanja huo sasa umefunguliwa na Simba ndipo atakwenda kusaka ushindi ili kusonga mbele.

“Hapa Port Said kuna timu moja tu, ni Al Masry. Kama ulivyoona tiketi zinagombaniwa sana, mashabiki hapa hawataki kukosa fursa ya kutazama mchezo huo.

“Kama unakumbuka huu uwanja ulifungiwa, hivyo Simba ina bahati mbaya maana umefunguliwa na ndio wanakuja hapa. Kwenye mechi za kimataifa hakuna ukomo wa tiketi, ila kwenye mechi za Ligi Kuu huwa wanapewa idadi ya watu ambao wanaruhusiwa kuingia,” anasema Imam.

Tiketi za mechi ya leo usiku zinauzwa kati ya Dola 7-25 za Kimarekani na ni sawa na Sh15,000-80,000.