Maoni: Nidhamu kwa wachezaji ni silaha ya mafanikio uwanjani

Muktasari:

  • Kwa wachezaji wa soka na michezo mingine, vitu hivyo ni muhimu kwa sababu vinawasaidia kufika mbali katika maisha yao.

ILI mtu afikie mafanikio ya kila jambo ni muhimu kuzingatia vitu vya msingi kama nidhamu, juhudi na uvumilivu.

Kwa wachezaji wa soka na michezo mingine, vitu hivyo ni muhimu kwa sababu vinawasaidia kufika mbali katika maisha yao.

Mchezaji asiye na nidhamu, uvumilivu na kujituma kwa bidii ni nadra kufika mbali kwa sababu, msingi wa soka umejengwa katika nguzo hizo.

Fuatilia hata kwa wachezaji wenye vipaji, kama watakosa nidhamu, kujituma na uvumilivu mwisho wao huwa vipi? Wengi hushindwa kufikia ndoto walizojiwekea ama zile ambazo walitabiriwa na watu wanaowafuatilia. Mifano ipo mingi ndani na nje ya nchi.

Nidhamu sio suala la mchezaji kumwamkia kocha mkuu ama watu wa benchi na viongozi ama wachezaji waliomzidi umri. Ni namna mtu anavyofuata taratibu za soka ndani na nje ya uwanja, ikihusisha ratiba yake ya mazoezi, mlo, muda wa kupumzika, kulala, aina ya marafiki na mengine ambayo yanachangia kwa namna moja au nyingine.

Kama mchezaji anafanya mambo yake bila kuzingatia nidhamu ni vigumu kusonga mbele na kama hapendi kujituma nao ni mtihani mwingine na iwapo hana uvumilivu ni jambo jingine linaloweza kumwangusha mapema kisoka.

Bahati mbaya ni wachezaji wachache nchini wanaotambua misingi hiyo na kuizingatia. Miongoni mwa wachezaji hao wachache ni Mbwana Samatta na kwa sasa Simon Msuva. Wapo wengine, lakini tunawatumia hawa kwa namna ambavyo safari zao kisoka zilivyopitia changamoto mbalimbali mpaka kufika walipo sasa.

Samatta asingekuwa Ubelgiji kwa sasa kama asingezingatia nidhamu, kujituma na kuvumilia. Ni sawasawa na Msuva ambaye amepitia katika safari ndefu mpaka kufika Morocco akicheza soka la kulipwa klabu ya Difaa El Jadida.

Wapo baadhi ya wachezaji wenye vipaji vikubwa kuliko wawili hawa, lakini wameshindwa kufika walipofikia wenzao, sio kwa sababu ya kukosa bahati au kubaniwa. Hapana ni kwa sababu wameshindwa kuzingatia mambo hayo matatu na kujikwamisha wenyewe bila kutarajia.

Kama mchezaji hana nidhamu ndani na nje ya uwanja ni vigumu kufika mbali. Kama mchezaji hajitumi kwa bidii na kuvumilia changamoto anazokutana nazo ni nadra kufika mbali kwa sababu hukata tamaa na kuridhika mapema.

Mchezaji asiyependa mazoezi, anayeendesha mambo yake kwa mtindo wa bora liende na kutegemea kipaji tu, ni vigumu kufika mbali kwa sababu adui mkubwa wa mchezaji ni utovu wa nidhamu.

Mwanaspoti linawakumbusha wachezaji wetu, kujikita kwenye misingi hiyo kama kweli wanataka kufika walipofikia wenzao wanaotamba kimataifa.

Hakuna siri Tanzania ina hazina ya vipaji vingi vya soka na hata michezo mingine, lakini vipaji hivyo vinashindwa kuleta manufaa kwao na taifa kwa jumla kwa sababu ya kupuuza misingi hiyo mitatu.

Ndio maana tunawakumbusha wachezaji wetu, wasijidanganye kuwa wataweza kufika walipofikia kina Didier Drogba ama Sadio Mane kama hawatakubali kupita katika njia hizo tulizoziainisha hapo juu. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amekuwa akipata mafanikio ndani ya soka la Tanzania kwa sababu ya kuzingatia vitu hivyo. Tshabalala ana nidhamu ndani na nje ya uwanja. Anajituma mazoezini na uwanjani na pia ni mvumilivu kwa kufuatilia historia yake kisoka tangu alipoibuka.

Wachezaji wetu wasiishi maisha ya kuku wa kienyeji, lazima wazingatie misingi hiyo na kujengwa tangu ngazi za chini. Kuanzia kwa wazazi, makocha na viongozi wa klabu wanapaswa kuujenga msingi nzuri wa mchezaji ili wakue nao na kumfikisha kule kunakotakiwa.

Lakini kubwa zaidi ni kwa wachezaji wenyewe kjitambua kuwa soka ni ajira zao, ni maisha yao na kuyumba kwao kisoka kutakwamisha kila kitu kwao, hivyo ni muhimu kwao kujikita katika misingi hiyo mikuu ya kuyafikia mafanikio.

Wachezaji wasisubiri kungozwa na mtu, wajiongoze kwa kila jambo kwa sababu wanapoharibu wanajiharibia wenyewe na ifahamike majuto ni mjukuu.