MAONI YA MHARIRI: Ni wakati sasa klabu kuwaza namna ya kufanya biashara

Muktasari:

  • Miaka 30 iliyopita, soka kwa hapa Tanzania lilikuwa sehemu tu ya kujiweka fiti na kushindana bila kujali kinapatikana kitu gani.

SOKA linazidi kupita katika nyakati tofauti na kuwa na mabadiliko mengi. Hii ni kuanzia dunia ya kwanza hadi ile ya tatu ambayo tunaishi.

Katika nchi za Ulaya, tayari wamehama kutoka katika nyakati za soka kuwa burudani na kulifanya kuwa biashara tena yenye mapato makubwa. Kwa Tanzania bado tupo katika kipindi cha mpito kujaribu kufanya mageuzi ya soka na kulifanya kuwa biashara.

Miaka 30 iliyopita, soka kwa hapa Tanzania lilikuwa sehemu tu ya kujiweka fiti na kushindana bila kujali kinapatikana kitu gani. Wachezaji wengi walihama kutoka timu moja kwenda nyingine bure, wengi hawakuwa na mikataba huku wengine wakitegemea kupata tu posho bila kuwa na mishahara inayoeleweka.

Kwa sasa hali haiko hivyo tena. Soka limebadilika na kuwa biashara japo bado kumekuwa na changamoto kubwa ya namna ya kuzifanya biashara hizo.

Ni wazi nchini kuna mashabiki wengi wenye wazimu na soka lakini bado hawajatumiwa vizuri kuwa sehemu ya kipato kwa klabu pamoja na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na soka. Biashara ya soka iko tofauti kidogo, inahitaji akili pana, uthubutu na usimamizi mkubwa.

Katika soka, biashara ya kwanza ni ya mechi, ziwe za mashindano ama za kirafiki. Huzalisha mapato ambayo baadaye hugawanywa kwa mujibu wa kanuni. Kwa Ligi Kuu Bara baada ya kukatwa kodi, timu mwenyeji hupata asilimia 40 wakati mgeni hupata asilimia 20.

Hii ina maana, timu zinatakiwa kuifanya mechi yao kuwa bidhaa kwa kuitangaza na kufanya harakati zote kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi uwanjani.

Bahati mbaya klabu hazioni hilo. Zinachukulia mechi zake kawaida na hakuna hamasa yoyote inayofanyika kuhimiza watu wakatazame mechi zao. Matokeo yake mechi zinachezwa na mashabiki hawafiki hata nusu uwanja.

Kwa timu kama Simba yenye mashabiki zaidi ya milioni moja jijini Dar es Salaam, inashindwaje kujaza Uwanja wa Uhuru unaobeba watu 20,000 kila wikiendi? Yanga nayo inashindwaje? Mbona kwenye tamasha la Simba Day watu zaidi ya 40,000 hujitokeza? Kuna kitu cha ziada huwa kinafanyika.

Biashara ya pili katika soka ni mauzo ya wachezaji na mpaka sasa hapa nchini inafanywa na Mtibwa Sugar pekee. Nyingine ziko wapi?

Katika kipindi cha miaka miwili, Mtibwa imewauza Shiza Kichuya, Mzamiru  Yassin, Mohammed Ibrahim, Said Mohammed ‘Nduda’ na wengineo kwenda Simba.

Biashara ya wachezaji ina pesa nyingi. Timu ikiweza kuuza wachezaji wawili ama watatu kila msimu itakuwa na uhakika wa kutengeneza zaidi ya Sh100 milioni. Kwa nini zinashindwa? Bado kuna tatizo mahali.

Biashara ya tatu katika soka ni ile inayotokana na bidhaa za klabu. Hapa ndipo linakuja suala la jezi orijino za klabu, skafu, viatu na vitu vingine vinavyoweza kuuzwa na timu ya soka. Mauzo ya jezi hufanyika kulingana na ukubwa wa mastaa. Timu inapofanya usajili wa mchezaji staa, inatengeneza jezi nyingi zenye jina lake na kuziuza kwa mashabiki wake. Biashara hii bado haifanyiki ipasavyo hapa nchini.

Simba, Azam na Mbeya City zinajaribu lakini bado hazijapata njia sahihi. Bado kumekuwa na walanguzi wengi kwenye bidhaa hizi.

Mfano leo hii Yanga ingekuwa inauza jezi nyingi zenye majina ya Papy Kabamba Tshishimbi na Ibrahim Ajibu. Simba ingekuwa inauza jezi za Emmanuel Okwi na John Bocco.

Biashara ya mwisho kwenye soka ni haki za matangazo. Hizi huanza na haki ya kuweka matangazo katika jezi za timu. Hapa ndipo linapokuja suala la udhamini. Mfano Simba na Yanga zimeuza haki hiyo kwa SportPesa.

Timu nyingine zinakuwa na wadhamini wengi zaidi na zaidi. Zipo timu zenye wadhamini hadi 15.

Kama timu ina uwanja wake huwa inauza haki za jina pamoja na kuweka mabango uwanjani. Klabu kama TP Mazembe inapata pesa nyingi tu kwa kuweka mabango uwanjani. Kwa nini timu za hapa nchini zimeshindwa?

Biashara hizo ni njia sahihi za kuzipatia klabu fedha nyingi, endapo tu zitafanyika kwa uhakika.

Tunapenda kuzishauri klabu kujifunza namna ya kufanya biashara za soka ili kusaidia kukua kwa uchumi wao na taifa kwa jumla. Enzi za kucheza soka kwa mazoea zimekwisha.