INAWEZEKANA: Ni sahihi Wenger kuamua hivi

Muktasari:

Kumbukumbu za mashabiki wa soka ni fupi na miaka 14 ni mingi katika dunia ya soka. Mara ya mwisho Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa mwaka 2004.

MSOMAJI, wiki iliyopita kocha mkongwe wa Arsenal, Arsene Wenger, alitangaza kuwa huu ni msimu wake wa mwisho wa kuifundisha Arsenal.

Hakika Wenger ni kati ya makocha bora kuwahi kufundisha katika Ligi Kuu England na yeye ni sababu kubwa ya Arsenal kufika hatua ya kuwa miongoni mwa klabu bora zaidi barani Ulaya, lakini yeye pia ni sababu kubwa ya klabu hiyo kupoteza nafasi katika ulimwengu wa soka hivi sasa.

Kumbukumbu za mashabiki wa soka ni fupi na miaka 14 ni mingi katika dunia ya soka. Mara ya mwisho Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa mwaka 2004.

Katika msimu huo, kikosi cha Wenger kilicheza soka la kutisha na kwa mtazamo wa wengi, Wenger alikuwa kocha bora zaidi duniani wakati huo.

Timu yake ilifanya kile ambacho wengi walifikiri walidhani hakiwezekani, yaani kushinda Ligi Kuu England bila kupoteza hata mechi moja. Yeye alifanya.

Lakini sasa ni wakati mwingine na mambo mengi yamebadilika katika dunia ya soka katika muda huo wa miaka 14.

Wakati Arsenal ilipoamua kuvunja uwanja wake wa zamani, Highburry, na kuujenga mpya wa kisasa, Emirates, klabu hiyo ilikuwa inapata kipato kikubwa kutoka mauzo ya tiketi za mechi za nyumbani.

Kwa kujenga uwanja mpya, Arsenal iliamini itaongeza kipato hicho ambacho kingeisaidia kuwa hata klabu kubwa zaidi England na barani Ulaya pia.

Bahati mbaya haikuwa hivyo. Kutokana na kujenga uwanja mkubwa, Arsenal ilijikuta kwenye madeni mengi kwa misimu mingi iliyofuata, hali iliyosababisha Wenger kukosa fedha nyingi za kufanya usajili mkubwa wa wachezaji.

Kwa dunia ya sasa, kipato kikubwa cha klabu nyingi ikiwamo Arsenal, kinatokea mikataba minene ya televisheni, hivyo bajeti ya Arsenal haizidi sana bajeti ya klabu nyingine kubwa England hata kama uwanja wake unachukua takribani mashabiki 60,000.

Naamini kuwa mashabiki wa Arsenal walielewa Wenger hakuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wengi wakati klabu hiyo ilikuwa katika madeni, hivyo kwa mtazamo wangu kocha huyu alifanya kazi nzuri kuhakikisha Arsenal inabaki ‘Top Four’ katika miaka hiyo.

Lakini katika misimu ya hivi karibuni, uchumi wa Arsenal umekuwa mzuri, madeni ya Emirates hayaiathiri klabu hiyo tena na Arsenal ni klabu yenye kipato kikubwa.

Hivyo mashabiki wake wanategemea kuiona klabu yao ikisajili wachezaji wazuri ili wafikie kiwango walichokuwa nacho mwanzoni mwa karne hii.

Bila shaka, usajili wa Mesut Ozil na Alexis Sanchez katika miaka ya hivi karibuni ulikuwa uamuzi mzuri, hata hivyo Wenger sasa ameshindwa kusajili wachezaji wengine wenye kiwango kikubwa hali iliyosababisha Manchester United, Chelsea na Manchester City kuiacha Arsenal mbali.

Msimu huu Arsenal imekuwa katika hali mbaya kimpira.

Katika mechi nyingi, idadi kubwa ya wachezaji wamecheza bila kujiamini. Kazi ya ukocha si tu kuwa mwanaharakati mzuri, lakini pia unahitaji kuwa na uwezo wa kuhamasisha wachezaji.

Msimu huu Wenger ameonekana hata kuanza kupotea chumba cha kubadilishia nguo wachezaji na wachezaji wengi wameonekana kutokuwa na hamu kucheza chini ya uongozi wake.

Kwa mtazamo wangu, hii ni ishara kubwa kwamba Arsenal inahitaji kocha mpya. Hivyo uamuzi wa Wenger kuachia ngazi klabuni hapo baada ya msimu huu ni uamuzi sahihi.