Ngassa noma, mastaa wote hawa wamechemsha

WINGA matata aliyetikisa vilivyo soka la Bongo, Mrisho Ngasa amerudi Yanga kwa mara nyingine. Wenyewe wanasema amerudi nyumbani, klabu ambayo ameichezea kwa muda mrefu zaidi kuliko nyingine katika maisha yake ya soka.

Ngassa kabla ya kuondoka Yanga kwa mara ya mwisho mwaka 2015, aliwahi kuweka rekodi moja ambayo hadi anaondoka na kurudi hakuna aliyeivunja na sasa amerejea ili kuilinda kama atakuwa na nguvu ya kutosha kupigania nafasi katika kikosi hicho.

Rekodi hiyo ya Ngassa ni kufunga mabao sita Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014. Rekodi hiyo kuanzia alipoondoka hadi sasa hakuna aliyefanikiwa kuivunja ndani ya klabu hiyo na hawa ni mastaa ambao licha ya kufurukuta na kuonekana wangeibeba Yanga kimataifa, lakini wamechemsha na kuliacha jina la Ngassa kuendelea kukaa kileleni.

Mbali na Yanga, Ngassa kwa nyakati tofauti pia amezichezea Azam FC na Simba.

Donald Ngoma

Pamoja na uongozi wa Yanga kuamua kuvunja mkataba na mchezaji huyo kutokana na kukabiliwa na majeraha ya muda mrefu, lakini Ngoma anabaki kuwa mmoja wa mastaa waliobeba ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA wakiwa na Yanga. Pia, aliiwezesh Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016.

Alijiunga na Yanga mwaka 2015 akitokea Platinum’s ya Zimbabwe na kuonyesha kiwango kizuri tangu amejiunga na timu hiyo hadi pale walipoamua kuvunja mkataba wake kutokana na majeraha.

Pamoja na sifa za Ngoma katika kufumania nyavu, idadi kubwa ya mabao aliyofunga kwenye awamu moja ya mashindano ya kimataifa ni matatu ambayo alipachika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016 ambayo ni nusu ya mabao yaliyofungwa na Ngassa mwaka 2014.

Obrey Chirwa

Ni straika aliyefanya vizuri sana katika mashindano ya ndani kwa kuisaidia Yanga kupachika mabao mengi zaidi misimu miwili mfululizo, pamoja na kuwa na rekodi hiyo nzuri, ameshindwa kuonyesha makali yake kimataifa. Pia, Chirwa hakuweza kufurukuta kabisa kuvunja rekodi ya Ngassa.

Ameichezea Yanga misimu miwili na kuibuka mfungaji bora wa timu hiyo akipachika idadi kubwa ya mabao klabuni hapo, lakini pamoja na uwezo wa kuwaonea mabeki wa timu za Ligi Kuu, Chirwa ameshindwa kupenya kwenye anga za kimataifa.

Hata hivyo, mbele ya rekodi ya Ngassa kimataifa, Chirwa si lolote kwani idadi kubwa ya mabao aliyofung kwenye mashindano ya kimataifa ni moja ambalo alilifunga dhidi ya Township Rollers kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Amiss Tambwe

Anashikilia historia ya washambuliaji wa kigeni waliofunga idadi kubwa ya mabao na kufanikiwa kutwaa kiatu cha dhahabu na alifunga mabao 21 Ligi Kuu Bara, ambayo mpaka sasa hakuna aliyemfikia.

Hata hivyo, Tambwe ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Jangwani, ameshindwa kuvunja rekodi ya Ngassa pamoja na kushiriki mashindano ya kimataifa mara tatu mfululizo akiwa Yanga.

Ni miongoni mwa wachezaji ambao wameisaidia Yanga kuingia katika hatua ya makundi mara mbili mfululizo na amekuwa na msaada mkubwa katika michuano mbalimbali.

Tambwe naye ni miongoni mwa wanaoteswa na mafanikio ya Ngassa kwani, idadi kubwa ya mabao aliyowahi kufunga kwenye msimu mmoja wa mashindano ya kimataifa ni mawili ambayo yalipatikana kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016.

Saimon Msuva

Misimu mitano nyuma kabla ya kuamua kwenda nje kujaribu soka la kulipwa katika timu ya Difaa Hassan El Jadida, ndiye mchezaji aliyechukua kiatu cha dhahabu mara mbili mfululizo na alikuwepo katika kikosi cha Yanga kuingia katika hatua ya makundi msimu wa 2015/16.

Pamoja na kuwa na jicho kali la kuona nyavu, lakini jamaa naye ameshindwa kuvunja rekodi hiyo.

Msuva pamoja na kutimka Yanga na kujiunga na miamba hiyo ya Morocco ambayo pia inashiriki mashindano ya kimataifa, bado hajafikia rekodi ya Ngassa japo kuna uwezekano mkubwa wa kuifikia au kuivunja kama ataendelea kupata nafasi ya kucheza na kufunga.

Kwa sasa Msuva ana mabao matano kwenye anga za kimataifa.

Alipokuwa Yanga, kwenye mashindano ya Afrika alifunga bao moja tu ikiwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia akafunga idadi kama hiyo kwenye Kombe la Shirikisho mwaka 2016.

Ibrahim Ajibu

Alijiunga na Yanga akitokea Simba na kuingia kwenye anga za kimataifa akiwa na Yanga, lakini ameshindwa kuonyesha makali yake.

Japo Ajibu aliingia wakati tayari Yanga ikianza kukabiliwa na majanga na haikuwa vizuri ndani ya uwanja, hivyo kumfanya kushindwa kuonyesha makali kama ilivyotarajiwa.

Ajibu amecheza mashindano hayo na kuisaidia timu yake kuingia hatua ya makundi japo hadi sasa hawana dalili za kusonga mbele kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Wana pointi moja kwenye mechi nne walizocheza mpaka sasa. Tangu amejiunga Yanga, ameifungia bao moja tu kwenye mashindano ya Afrika.