Neymar na Sure Boy, wazazi katika dunia tofauti

Muktasari:

Mfano ulio wazi ni baba yake, Neymar. Anaitwa Neymar Snr. Tangu ajue mwanae ana kipaji ameacha kila kazi kwa ajili ya kula pesa za mwanae.

HUWA nina wivu na namna ambavyo wazungu wanatengeneza pesa. Wivu unanipata sana jinsi wanavyotengeneza pesa kupitia vipaji vyao.

Mfano ulio wazi ni baba yake, Neymar. Anaitwa Neymar Snr. Tangu ajue mwanae ana kipaji ameacha kila kazi kwa ajili ya kula pesa za mwanae.

Alianza maandalizi ya kula pesa hizo tangu akiwa kwao Brazil. Alisimamia kipaji chake kwa kumpeleka mazoezini kila siku na kumsisitizia awe na nidhamu. Leo, baba yake Neymar amekula zaidi ya pauni 20 milioni za halali kwa uhamisho wa Neymar kutoka Barcelona kwenda PSG.

Kabla ya hapo alikula pesa halali za uhamisho wa Neymar kutoka Santos kwenda Barcelona. Wale Barcelona walimpa chake mapema kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Neymar haendi Real Madrid. Baba yake Neymar ana kampuni yake ya kijanja.

Baba yake Neymar alikuwa mchezaji mzuri wa kawaida. Hata hivyo, alijua kuishi maisha ya soka baada ya soka. Alipobarikiwa kuwa na mtoto mwenye kipaji kama Neymar basi akaiona fursa na kuitumia. Mpaka leo sidhani kama ana kazi nyingine zaidi ya kuishi dunia ya Neymar.

Siku hizi wachezaji wengi Ulaya wanasimamiwa na wazazi wao ingawa wana mawakala zao. Hawa wazazi wanaowasimamia watoto wanafungua kampuni zao za kijanjajanja. Watu wanaofaidika zaidi kwa kuelewa kinachoendelea katika dunia ya soka ni wachezaji wa zamani.

Kwa mfano, Patrick Kluivert anawasimamia watoto wake. Cristiano Ronaldo atakuja kumsimamia mwanae akiwa mkubwa. Wote wanajua mirija ya utamu inavyokwenda na hawataki pesa iende mbali na mkondo wa familia.

Tunaishi katika dunia tofauti kidogo. Wachezaji wetu wa sasa inabidi wajifunze jinsi maisha ya soka yalivyo. Wasichukue pesa na kwenda kununua magari tu. Wanahitaji kutumia fursa hizi kwa kujifunza. Kuna siku na wao wanaweza kuwa na watoto wanaocheza soka la kulipwa.

Nachukulia mfano wa Aboubakar Salum ‘Sure Boy’. Staa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa. Hauwezi kumlaumu kwa kutosimamia vema kipaji cha mwanae. Angeweza kuchuma pesa zaidi kama angejifunza usimamizi wa mtoto wake na mikataba yake. Tatizo yeye mwenyewe wakati anacheza zamani hakukulia katika mazingira ya sasa.

Sure Boy orijino hakukulia katika masuala ya mikataba na usimamizi wa mawakala au mameneja. Labda kama angekulia huko angeweza kujua namna gani ya kuchuma pesa pale tu alipogundua kuwa mwanae ana kipaji kikubwa.

Lakini, leo tunaishi katika dunia ya Sure Boy mtoto. Amekulia katika mikataba ya Azam. Ameona pia wachezaji wengi wa kigeni wakija na kuondoka Azam. Ameona baadhi ya mameneja wa wachezaji wa kigeni waliofika Azam. Anajifunza kitu ili asifanye makosa ya baba yake? Hili ndio swali la msingi.

Mara nyingi nimekuwa nikisisitiza umuhimu wa wachezaji wetu kujifunza kuwa wachezaji mahiri na wanadamu mahiri. Kwa mfano, hawa wachezaji wetu wa kigeni ni mahiri na pia ni wanadamu mahiri. Miaka 10 ijayo unaweza kukutana na Emmanuel Okwi akiwa ameachana na soka, lakini anaishi katika maisha ya soka akipiga dili. Anaweza kuwa anasimamia baadhi ya wachezaji makinda pale Uganda au kwingineko na anajua jinsi ya kusaini mikataba, kuwatafutia timu, kuwauza. Sioni kama tuna wachezaji wengi wa kileo ambao wanaweza kuwa wapiga dili nje ya soka katika miaka inayokuja. Jonas Mkude ana usimamizi wa wakala wake. Je anajifunza chochote kwa namna ambayo anaweza kumlea mwanae kama yeye alivyolelewa na wakala wake?

Wakati mwingine ni rahisi kusingizia suala la elimu, elimu, elimu, lakini mwisho wa siku ni namna ya kutengeneza ujanja wa maisha tu. Namna ya kujaribu kuiga kile kinachokutokea kwa matumizi ya siku za baadaye na kwa ushirikiano wa watu unaowaamini. Tangu enzi na enzi, soka letu halizalishi wachezaji ambao baadaye wanaweza kuwa wachambuzi, mawakala, mameneja, au mabosi. Inatokea nadra sana kwa mtu kama vile, Wilfried Kidau kuwa Katibu Mkuu wa TFF halafu bado kijana halafu ametoka kucheza soka moja kwa moja.

Itazame dunia ya Neymar na baba yake halafu itazame dunia ya Sure Boy na baba yake. Vitu viwili tofauti.