Neymar ametukumbusha hakuna mchezaji asiyeuzwa

Tuesday August 8 2017

 

HAIJALISHI wewe ni mchezaji wa aina gani, hakuna mchezaji asiyeuzwa hapa duniani. Inategemea tu una kiasi gani cha pesa katika kumnunua. Rais wa Real Madrid, Florentino Perez aliwahi kusema hivyo wakati akimtaka Zinedine Zidane huku Rais wa Juve, Luciano Moggi akiendelea kuropoka kuwa Zidane hauzwi.

Kwa hapa Tanzania rafiki zetu hawauziani wachezaji. Simba, Yanga na Azam wamekuwa wagumu kuuziana wachezaji. Hii yote inatokana na ujinga na wachezaji pamoja na viongozi wa klabu. Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani.

Hapa Tanzania ukienda kwa mtani kutaka kumnunua mchezaji unaambiwa kuwa ana mkataba. Inadhaniwa kuwa mkataba ni ndio tija ya kumzuia mchezaji asiuzwe. Uongo ulioje! Mkataba ndio sababu ya mchezaji kuuzwa katika klabu nyingine.

Wanachokosea wachezaji wetu ni kusaini mikataba ya upande mmoja. Mikataba yao inatokana na akili za viongozi wa klabu zao. Haitokani na akili za wanasheria wao. Mikataba yao ilipaswa kutengenezwa kwa mahafikiano baina ya pande mbili lakini hapa kwetu mikataba inatengenezwa na viongozi.

Kwa mfano, Neymar ameondoka kwa kutumia kipengele ambacho kiliwekwa katika mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote mbili kwamba kama kuna klabu ikifika dau la Pauni 196 milioni, basi anaweza kuuzwa kama Neymar akijisikia kuhama.

Uhamisho wa Luis Figo kwenda Real Madrid kutoka Barcelona ulitumia kipengele hicho. Uhamisho wa Zidane kutoka Juve kwenda Real Madrid ulitumia kipengele hicho. Inapofikia hatua klabu ipo tayari kutoa kiasi cha mauzo kilichopo katika mkataba kunakuwa hakuna mazungumzo zaidi ya kupeleka hundi tu.

Hapa Tanzania wachezaji hawaingii vipengele hivi. Kwa mfano, kila siku Simba walikuwa wanamtamani Simon Msuva wakati akiwa Yanga lakini katika mkataba wake pale Jangwani hakukuwa na kipengele chochote ambacho kilikuwa kipo wazi kikionyesha kuwa klabu ikifika dau Fulani, basi inaweza kumbeba Msuva.

Mikataba ya wachezaji wetu yote iko sawa. Wameidurufu kila sentesi. Sehemu ambayo ipo wazi ni ile ya jina la mchezaji, pesa atakapewa akisaini pamoja na sehemu ya saini yake. Hakuna vipengele vinavyomtofautisha mchezaji mmoja na mwingine. Kila mchezaji amepewa masharti ya mwenzake.

Wachezaji waamke kwa sasa na wasiwe wafungwa wa mikataba. Kwa mfano, katika mkataba mpya wa Raphael Daud wa Yanga kupitia mwanasheria wake alipaswa kuandika wazi kwamba kama klabu ya ndani ya nchi ikiweka milioni 80 kwa ajili ya kumchukua, basi Yanga imuuze na itie kibindoni pesa hizo.

Angeweza pia kuandika kuwa kama kuna klabu ya nje ikifika Shilingi100 milioni kwa ajili ya kumnunua, basi Yanga ichukue pesa hizo na kumruhusu kuondoka. Hata hivyo, hakuna kipengele kama hicho na ndio maana klabu zetu zimewageuza wachezaji kuwa watumwa. Zinawanyanyasa kupitia mikataba kama vile ndio kigezo cha kukaa nao bila ya ruhusa ya kuondoka.

Kitu kingine ambacho hata klabu zenyewe zinakosea ni kwamba zinashindwa kuweka kipengele cha manunuzi ya mchezaji ambaye wamemuuza (Buy back clause). Kwa mfano, Simba na Azam zinakuza sana makinda. Makinda hawa wanaweza kukosa nafasi na hivyo kuruhusiwa kwenda kwingineko.

Hata hivyo, kuna uwezekano huko wanakokwenda wakapata nafasi na kuwa mastaa wakubwa.

Klabu yake ya zamani inaweza kumrudisha tena kwa Shilingi 20 milioni tu kama iliingia mkataba na klabu ndogo ambayo mchezaji alikwenda.

Kwa mfano, Simba ingeweza kumuuza Mbaraka Yusuf kwenda Kagera Sugar kwa bei ndogo kabisa. Hapo hapo wakaweka kipengele inaweza kumnunua tena mchezaji huyo kwa Shilingi 20 milioni endapo watajisikia kufanya hivyo.

Leo Mbaraka angekuwa amerudi tena Simba kwa mujibu wa kipengele hiki cha manunuzi ya baadaye. Hivi ndivyo ambavyo Real Madrid ilifanya kwa Alvaro Morata ilipomuuza kwenda Juventus kisha ikamnunua tena baada ya misimu miwili. Ilimnunua kwa pesa ndogo tu.

Wachezaji wetu wajikite katika kutafuta wanasheria wa kuwasimamia. Wasijiendeshe tu wenyewe. Wanageuzwa kuwa watumwa wa mikataba yao kwa sababu wanataka kujisimamia wenyewe au wanasimamiwa na watu ambao wanashindwa kuelewa mikataba ya mpira.

Neymar ametukumbusha tu hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani. Hata Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanauzwa. Inategemea tu kama umefika dau lililowekwa katika mikataba yao.