Ndikumana ameondoka, kaiacha Stand mahututi

Muktasari:

  • Kwa wapenzi wa burudani tukio kubwa lililoteka hisia zao na pengine kuwaacha na masikitiko ni lile la muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake Steven Kanumba mwaka 2012.

NI wiki iliyojaa majonzi na simanzi kwa wapenzi wa michezo na burudani kutokana na matukio kadhaa ya kuhuzunisha yaliyotokea ambayo kwa namna moja au nyingine yaliwagusa wadau wa sekta hizo nchini.

Kwa wapenzi wa burudani tukio kubwa lililoteka hisia zao na pengine kuwaacha na masikitiko ni lile la muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake Steven Kanumba mwaka 2012.

Kifungo cha Lulu ni pigo kubwa kwa wadau wa sanaa na burudani kwani kinakwamisha na kurudisha nyuma harakati na mipango ambayo alitaka kuifanyia kazi katika kipindi hicho cha miaka miwili.

Wakati kabla hata tukio la Lulu halijapoa, medani ya soka Afrika Mashariki na Kati imejikuta ikimpoteza aliyewahi kuwa mmoja kati ya viungo mahiri kuwahi kutokea katika ukanda huu, Hamad Ndikumana aliyefariki nchini Rwanda usiku wa kuamkia juzi.

Ndikumana ambaye hadi anafikwa na umauti alikuwa ni kocha msaidizi wa mabingwa wa Ligi Kuu Rwanda, Rayon Sports, mbali na kuwahi kuwa mume wa Mtanzania mwenzetu, muigizaji Irene Uwoya pia aliwahi kucheza soka la kulipwa hapa nchini katika klabu ya Stand United iliyopo mkoani Shinyanga pamoja na Yanga.

Usajili wa Ndikumana katika kikosi cha Stand United ulikuwa ni miongoni mwa habari iliyoshtua maelfu ya wadau wa soka nchini hasa kutokana na kutotegemea klabu kama hiyo ambayo ndio kwanza ilikuwa na misimu miwili kwenye Ligi Kuu tangu ipande, imsajili staa kama huyo ambaye alijijengea jina kubwa katika ukanda huu.

Kwa nchi ambayo usajili wa wachezaji mastaa wa ndani na kigeni umekuwa ukifanywa na klabu za Yanga, Simba na Azam, ni wazi mashabiki walikuwa na haki ya kushtuka hasa pale wanapoona nyota aliyechezea timu kubwa kama Anderlecht, Mechelen na KAA Gent zinazoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji au Anorthosis Famagusta na AEL Limassol za nchini Cyprus anasajiliwa na wapiga debe wa Stand United.

Hata hivyo ndani ya Stand United ilikuwa ni jambo la kawaida kufanya usajili wa namna hiyo kutokana na misuli ya kiuchumi ambayo klabu hiyo ilikuwa nayo kwa wakati huo ikichagizwa na udhamini mnono waliokuwa nao kutoka kampuni ya kuchimba madini ya Acacia.

Hakuwa Ndikumana tu bali klabu hiyo iliweza kuvuta nyota kama Haruna Chanongo, Elias Maguli, Seleman Kassim ‘Selembe’, Amri Kiemba, Joseph Owino pamoja na kumuajiri kocha Mfaransa aliyewahi kuinoa Simba, Patrick Liewig.

Haikuwa usajili wa bei mbaya tu, Stand United ililala pazuri, walilipwa mishahara na posho kwa wakati pamoja na kupewa huduma zote stahiki bila kuwepo na changamoto za hapa na pale kama ambazo idadi kubwa ya timu za soka hapa nchini zimekuwa zikikumbana nazo.

Ujeuri huu wote wa Stand United ulitokana na udhamini wa zaidi ya Sh1 bilioni mabao walikuwa wakipata kutoka Acacia ambao ni wazi walionyesha nia ya dhati ya kutaka kuifanya timu hiyo iwe tishio katika medani ya soka ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya udhamini huo kutoka kampuni ya Acacia uligeuka moto kwenye klabu hiyo baada ya kusababisha mgogoro mkubwa uliopelekea uongozi na wanachama wa Stand United kugawanyika hali iliyopelekea kampuni hiyo ya uchimbaji madini kuachana na klabu hiyo kutokana suluhu baina ya pande hasimu kushindwa kupatikana.

Kujiondoa huko kwa Acacia kuliirudisha Stand United kwenye zama za giza ambapo idadi kubwa ya mastaa iliowasajili kama akina Ndikumana, walitimkia kwenye timu nyingine, maisha ya wachezaji yakaanza kuwa magumu kutokana na kucheleweshewa posho na mishahara yao huku klabu hiyo ikishindwa kufanya usajili wa maana kutokana na ukata.

Ni jambo la kusikitisha kuona Ndikumana anafariki katika kipindi ambacho moja ya klabu zake alizowahi kuitumikia ipo kwenye hali mbaya kiuchumi huku siku zake za kubakia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara zikiwa zinahesabika kutokana na matokeo mabovu ambayo imekuwa ikiyapata kwenye mechi zake za Ligi Kuu.

Pengine kifo chake kingemkuta akiwa ameiwezesha Stand United kutamba kwenye Ligi Kuu na mashindano mengine inayoshiriki lakini kutokana na upuuzi wa watu wachache, aliamua kutimkia kwao ambako ameacha alama kwa kuisaidia Rayon Sports kutwaa ubingwa akiwa kama kocha msaidizi.

Kifo cha Hamad Ndikumana ni pigo kubwa kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati lakini kwa Stand United ni msiba mkubwa zaidi kwa sababu ameondoka katika kipindi ambacho timu hiyo inapumulia mashine.

Tumuombee Ndikumana huko aendako, akapumzishwe kwa amani na apatiwe mema mbele za Mungu.

Mchezaji huyo alizikwa juzi jioni kwenye Makaburi ya Nyamirambo, na mamia ya wanamichezo walishiriki maziko yake wakiwemo viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa michezo.