Nasi tujiandae kuamua mechi zetu kwa video

Saturday December 2 2017

 

MALALAMIKO dhidi ya waamuzi wa soka nchini yameendelea kushika kasi katika mechi za Ligi Kuu Bara na hata Ligi Daraja la Kwanza zinazoendelea kuchezwa nchini.

Kadiri siku zinavyokwenda ndio makosa ya kibinadamu yanavyozidi kuonekana, hii nayo haipo hapa kwetu tu, hata kwa wenzetu kama kule barani Ulaya hali ni hivyo hivyo tu.

Kwa kiwango fulani, makosa ya kibinadamu yanayofanywa na waamuzi huongeza ladha ya mchezo wenyewe kwani makosa ni sehemu ya mchezo. Kukosea ni sifa ya binadamu, hivyo makosa hubeba uanadamu.

Nakumbuka kocha wangu mmoja alipokuwa akitufundisha masuala ya nidhamu ndani ya uwanja, alituambia kuwa kama mchezaji anaweza kukosea kwa kumpasia mpinzani badala ya mchezaji wa timu yake, basi hata mwamuzi naye anaweza kukosea, kwani ni binadamu hivyo naye ana haki ya kukosea kama akoseavyo mchezaji.

Wiki iliyopita tulishuhudia matukio kadhaa katika mechi za hapa kwetu Bongo, lakini hayo yalihitimishwa na tukio lililotokea Jumapili barani Ulaya katika mechi ya Ligi Kuu Hispania iliyozikutanisha Barcelona na Valencia iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo, mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi alipiga mpira kwenda langoni mwa Valencia na kipa aliucheza kisha ukadunda nyuma yake na hatimaye kuuokoa tena kwa mara ya pili kitendo ambacho watazamaji tuliokuwa tukiifuatilia mechi hiyo kupitia televisheni, tuliweza kuona kuwa mpira ule ulidunda ndani ya goli.

Hata hivyo, kwa kuwa mwamuzi, Ignacio Iglesias na wasaidizi wake walikuwa uwanjani hawakuweza kuona kama mpira ule ulikuwa tayari umeshavuka mstari wa goli, hivyo walilikataa kuwa sio bao.

Matukio kama hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na hivyo kuchukiliwa uamuzi wa kuanzisha teknolojia hiyo ili iwe rahisi kuamua iwapo mpira umeingia golini au la.

Wakati hayo yakitokea huko, Jumatatu Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), ilikutana jijini Cairo, Misri na kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya teknolojia katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika mwaka 2018 kule Morocco.

Katika mkutano huo, kamati hiyo ilipitisha matumizi ya rekodi za video kama mwamuzi msaidizi (VAR) yatakayoanza kutumika katika fainali hizo kuanzia hatua ya robo fainali.

Kutokana na hatua hiyo, CAF imewaita pia waamuzi wa Afrika walioteuliwa kuchezesha fainali za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Urusi ili nao waendelee kujifunza matumizi hayo ya video.

Hivyo ukiona CAF imepitisha maamuzi hayo tena kwa shindano la wachezaji wa ndani, maana yake ni kwamba muda si mrefu matumizi hayo yatatakiwa kushuka chini hadi kwa wanachama wake, sisi Tanzania tukiwa miongoni mwao.

Nayasema haya kwa kuwa maendeleo katika dunia ya sasa yanakwenda kwa kasi zaidi. Dunia ya sasa haina msamiati unaoitwa subira. Hivyo ni vyema kujiandaa ili maendeleo yatakapokuhitaji uwe tayari umekwishaanza na upo njiani ukiendelea.

Bahati nzuri wiki iliyopita hapa kwetu Bongo waamuzi takribani 18 walipata beji za Fifa, hivyo ni imani yetu kuwa pamoja na kuwa ligi zetu bado hazijaanza kutumia teknolojia hiyo ya video katika kufanya maamuzi ya uwanjani, lakini waamuzi hao wanayo nafasi ya kujifunza kabla ya muda rasmi wa matumizi kufika hapa kwetu.

Hivyo tutarajie katika miaka ya hivi karibuni kwenye mashindano mathalani haya ya Kombe la Chalenji yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuona matumizi ya video kutumika kwa kuwa tayari CAF imeshaanza utaratibu huo.

Pamoja na yote hayo, bado waamuzi wetu wanatakiwa kujipanga na kujiandaa kupokea mabadiliko haya tena kwa kasi ili yaendane na mabadiliko yaliyopo katika soka la dunia.

Kwa leo naomba kuishia hapa, nasubiri mrejesho kutoka kwenu.