Nani atakayevaa viatu vya Usain Bolt?

Tuesday August 8 2017

 

By BONFACE AMBANI

SIJAWAHI kuandika makala yoyote kuhusu riadha lakini kwa leo mtanisamehe wasomaji wa makala yangu ya soka.

Leo nazama ndani ya makala ya riadha nikiwa na sababu kubwa. Nina sababu kubwa ya kuandika makala kuhusu riadha. Kisa na maana kuna mwanariadha alistaafu juzi kutoka kwa mbio za mita 100 kwa jina Usain Bolt.

Mwanariadha huyu kutoka Jamaica juzi katika Jiji la London alistaafu rasmi kushiriki mbio hizo. Takriban ya zaidi ya miaka 10 ameweza kunawiri katika mbio hizo. Kijana mrefu kutoka nchi ya Jamaica kwa kweli alikuwa amegusa nyoyo za binadamu wengi sana duniani. Usain Bolt rafiki wa karibu sana wa Cristiano Ronaldo alistaafu baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu katika mbio za IAAF zinazofanyika London.

Katika fainali hizo Bolt alishindwa na Mmerikani, Justin Gatlin. Kushindwa kwake kwa kweli haikuwa ishu kubwa hata kidogo. Heshima ambayo alipewa ndani ya uwanja baada ya kuachana na mbio za mita 100 ndugu zanguni ndio lilikuwa jambo kubwa kuliko. Mashabiki ndani ya uwanja wote walisimama kumpa heshima zake za mwisho jambo ambalo kwa kweli lilinivutia sana. Bolt alizaliwa mwaka1986 Jamaica. Kwa sasa ndiye mwanadamu ambaye anashikilia rekodi ya kukimbia mita 100 duniani na sijui kama itakuja kuvunjwa hivi karibuni. Bolt ndiye anayeshikilia rekodi za dunia za mita 100,200 na pia mita 100 ya kupokezana vijiti. Rekodi yake ya kukimbia mita 100 ndani ya sekunde 9 nukta 58 bado imesimama hadi wakati alipoamua kustaafu. Bolt ameshinda nishani za dhahabu ya Olympiki mara nane. umaarufu wake wa mbio ulianza mwaka wa 2008 jijini Beijing China baada ya kuvunja rekodi mbili mtawalia ya mita 100 na mita 200.

Bolt anabakia kuwa mwanariadha wa kipekee duniani kuweza kushinda nishani za dhabu mfululizo katika mbio za olimpiki ikiwa alishinda mwaka wa 2008, 2012 na 2016.

Mwanariadha huyo alinifanya nibubujikwe na machozi baada tu ya kutangaza kuwa anastaafu kutoka. Ilikuwa ni wakati mgumu kwangu. Ningekuwa na uwezo ningemsihi aendelee kukimbia mbio hizo kisa na maana alikuwa anafanya kazi yake kwa kujitolea na alikuwa anaipenda sana kazi yake.

Hakuna kitu ambacho hunifurahisha duniani kama kumuona mwanamichezo anayeupenda mchezo anaoshiriki. Kwa kweli nahisi itakuwa pia vigumu sana kwa mshambuliaji wa Real Madrid, Ronaldo kuweza kustahimili kipigo hicho popote aliko. Kwa wale ambao hawafahamu, Ronaldo ni rafiki mkubwa wa Bolt. Muda ambao Ronaldo alikuwepo Manchester United wawili hao walikuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia pamoja.

Hizo mbio Ronaldo hukimbia ndugu zanguni ni zoezi ambalo alikuwa akipewa na Bolt. Ni marafiki wa karibu. Ikumbukwe Bolt pia ni sahabiki sugu wa Manchester United na alianza kushakibia klabu hiyo enzi za Ruud Van Nielstroy.

Baada ya mbio hizo za London, Bolt alibusu kiwanja na kuinuka na kuinama mbele ya mashabiki kwa ishara ya kuwa anaacha rasmi mashindano. Alizunguka uwanja wote akipiga picha na mashabiki wake akitoa heshima zake za mwisho.

Ilikuwa ni wakati mgumu kwa maafisa wa polisi kumtoa uwanjani kwani kila mtu alikuwa anataka apigwe naye picha za kumbukumbu. Ni wengi wamebaki na kumbukumbu zake jijini London na ni wengi ambao hawatamsahau.

Dunia nzima ilisimama kwa heshima zake. Kilichofurahisha ni kuwa na mapenzi na kila mtu na hana dharau hata kidogo. Ni mcheshi, ana heshima, roho yake safi. Hauwezi kumlinganisha na Gatlin ambaye kwa kweli uwanja wote ulimkataa licha ya yeye kushinda mbio hizo.

Hata hivyo, kulingana na habari za karibu Bolt anaweza kulaumu kushindwa kwake kwa kutokuwa na mazoezi ya kutosha baada ya kumpoteza rafiki wake wa karibu, Germaine Mason aliyefariki dunia kupitia ajali ya gari, kifo ambacho kilimsimamisha Bolt kufanya mazoezi kwa muda wa wiki tatu. Jeraha pia alilo nalo la uti wa mgongo, pia limechangia kwa kushindwa katika mashindano hayo. Kulikuwa na wakati wa heshima kati yake Bolt na Gatlin wakati Gatlin alionyensha ishara ya heshima zake kwa Bolt. Kilichonigusa ni wakati hao wawili walipokumbatiana.

Ni wakati hautaonekana tena popote pale. London itabakia kuwa katika historia ya wawili hao. Majogoo wa riadha.

Hata hivyo, Bolt atabakia kuwa mwanariadha bora duniani baada ya kustaafu kwake. Kwa kweli nitamkosa. Ningesimamisha shughli zangu zote ili kuchukua muda kuangalia shughli zake uwanjani.

Michael Jordan alipostaafu kutoka kwa mchezo wa vikapu ilinichukua muda kabla Kobe Bryant kunishawishi kurudi kutazama mpira wa vikapu. Kwa kweli itanichukua muda tena kabla niweze kufurahishwa na mwanariadha mwingine wa mita 100.

Kumbuka kabla Bolt, kulikuwa na Ben Johnson wa mita 100.Kila mchezo huwa na gwiji wake. Kwa hivyo acha tungojee tuone ni nani mwingine ataweza kuvaa viatu vya Bolt. Namtakia maisha mema.