NINACHOKIAMINI: Mbeya City hawakutaka kupata heshima kwa Yanga

Muktasari:

Nidhamu ya mchezo huifanya timu kuwa makini na lango lao, hulinda zaidi lango huku wakishambulia kwa umakini mkubwa.

KAMA kuna kitu ambacho makocha na wachezaji wa timu mbalimbali wameshindwa kukifanya na kukitekeleza ni nidhamu ya mchezo.

Nidhamu ya mchezo huifanya timu kuwa makini na lango lao, hulinda zaidi lango huku wakishambulia kwa umakini mkubwa.

Wakati timu inaposhambulia, wachezaji wanapaswa kujua kuwa wana kazi ya kulinda lango lao lisiwe katika hatari.

Hilo ni jambo la kawaida katika mchezo wa soka, bahati mbaya ni kuwa makocha wengi na wachezaji wao wamekuwa wakidharau hilo.

Ingawa mashabiki wa soka wamekuwa wakimlaumu Jose Mourinho kwa kucheza mpira wa kujihami zaidi kuliko kushambulia, binafsi naikubali nidhamu yake ya mchezo katika kujilinda.

Mourinho anaujua uwezo wa timu yake, hivyo akiamua kujihami anafanya hivyo kwa sababu anajua hana uwezo wa ‘kupishana’ na ‘kushambuliana’ na timu pinzani, hivyo anaamua kujihami zaidi.

Unapokuwa kocha lazima ujue uwezo wa timu yako dhidi ya wapinzani unaocheza nao. Jambo la msingi kuliko yote ni kuangalia uwezo wa timu yako na wa timu pinzani.

Hilo litamfanya kocha kuamua aina ya mchezo na wachezaji wa kuwatumia, vinginevyo atajikuta katika matatizo makubwa.

Sidhani kama kocha wa Mbeya City, Nsanzurwimo Ramadhani aliyafanya yote hayo. Sidhani kama aliangalia uwezo wa timu yake, na sina uhakika kama aliujua uwezo wa Yanga.

Kwa mtazamo wangu kocha wa Mbeya City alifanya makosa matatu katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika juzi Jumapili.

Kwanza, hakutaka kujua uwezo wa Yanga na ndio maana aliamua kucheza mchezo wa kujiachia na kufunguka mwanzo mwisho wa mchezo. Alikosa nidhamu na wachezaji wake wakakosa nidhamu. Ukiona unacheza na timu kama Yanga halafu unashindwa kuonyesha heshima unastahili kuadhibiwa.

Jambo la pili ambalo lilinishangaza ni kumuona kocha wa Mbeya City na timu yake wakicheza kama wapo katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Hawakujua kuwa wapo ugenini, walitaka kucheza kama wapo nyumbani. Kwa Mbeya City ya sasa haina uwezo huo wa kusumbua timu nyingine ugenini. Nidhamu ya kujihami ingewasaidia zaidi uwanjani badala ya kujiachia.

Jambo la tatu, nililoliona ni Mbeya City ambayo inaundwa na wachezaji wengi wasio na uzoefu kujaribu kucheza na kukaba kwa nafasi, badala ya kucheza na kukaba mtu kwa mtu. Unapocheza kwa nafasi dhidi ya Obrey Chirwa, lazima utapewa adhabu inayostahili.

Huwezi kusafiri kilometa 900 zaidi ya saa 15 kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, halafu unacheza na Yanga ukadhani unacheza na timu ya sokoni Kariakoo.

Mourinho licha ya kuwa na timu kubwa ya Manchester United, kuna wakati huwa anakuwa ana heshima anapocheza na timu ambazo anadhani zina uwezo mkubwa.

Kufungwa mabao matano ni jambo la kawaida katika mchezo wa soka, tatizo ni umefungwa vipi? Nidhamu ilichangia kwa kiasi kikubwa kufungwa kwa Mbeya City.

Tupende tusipende, huwezi kucheza mchezo wako tu katika kila mechi bila kujua uwezo wa timu nyingine. Mbeya City walipaswa kujua wanacheza na timu kubwa, yenye mashabiki wengi, yenye uwezo kuliko wao, kwa hiyo walistahili kipigo hicho kwa sababu hawakuwa na nidhamu.