Mwakinyo apongezwe, asaidiwe maandalizi ya kusaka taji la IBF

Muktasari:

  • Mwakinyo ambaye amerejea nchini juzi na moja kwa moja kupelekwa bungeni mjini Dodoma ambako licha ya kupongezwa na kumwagiwa sifa lukuki, pia wabunge waliamua kumchangia fedha kama shukrani kwa alichokifanya.

BONDIA Hassan Mwakinyo ghafla tu amekuwa maarufu na gumzo kubwa ndani na nje ya nchi, hii ikiwa ni baada ya kumtwanga bondia Mwingereza Sam Eggington wiki iliyopita kwa TKO katika raundi ya pili ya pambano lililofanyika nchini Uingereza.

Mwakinyo ambaye amerejea nchini juzi na moja kwa moja kupelekwa bungeni mjini Dodoma ambako licha ya kupongezwa na kumwagiwa sifa lukuki, pia wabunge waliamua kumchangia fedha kama shukrani kwa alichokifanya.

Mwanaspoti kama wadau wa michezo, tulishampongeza mapema Mwakinyo kwa alichokifanya na kumtakia kila la heri katika safari yake ya kuendeleza kipaji chake na hasa kujiandaa vyema kwa pambano lake ujao dhidi ya Wanik Awdijan.

Tulitanguliza mapema kumtahadharisha Mwakinyo kwa kutambua, kwa kufanikiwa kumpiga kwa TKO Eggington tena kwenye ardhi ya kwao, itawafanya wapinzani wake wengine wa nje ya nchi kumfuatilia na kujiandaa vikali.

Pambano lake litalochezwa Oktoba 20 halipo mbali na ni wajibu wa bondia huyo kuanza kujipanga mapema ili kwenda Ujerumani na kuthibitisha hakubahatisha kumtwanga Muingereza.

Kitu cha muhimu kwa sasa kwa Mwakinyo mbali na kumwagiwa sifa na kupokea pongezi kila kona ya nchi, wale wanaojitokeza sasa kumkumbatia bondia huyo watambue wana dhima kubwa ya kufanikisha safari yake. Safari ya kwenda kwenye mafanikio zaidi katika mchezo huo na kuendeleza kipaji chake.

Tunalisema hivi kwa kutambua, kuna baadhi ya wadau na hata wanasiasa wanaweza kuitumia nafasi ya mafanikio ya Mwakinyo ya kumtwanga Eggington kama mtaji wao kisiasa na hata kwa mambo mengine.

Ndio, hakuna aliyekuwa anajua Mwakinyo aliweza kusafiri vipi kwenda Uingereza na kumpiga mpinzani wake, lakini leo kila mmoja anajitokeza kujifanya yupo karibu na bondia huyo.

Huu ni utamaduni wa siku zote nchini kwa watu kujitokeza kwenye mafanikio tu na kusahau kujitokeza wakati wa maandalizi ya safari ya mafanikio husika.

Tumekuwa tukiyaona hayo mara kadhaa kwenye soka, timu ya taifa iwe Taifa Stars ama zile za vijana na wanawake ama klabu zikipata mafanikio kwenye mashindano inayoshiriki, ndipo watu hujitoteza na hasa wanasiasa.

Hujifanya wameguswa sana na mafanikio ya timu hizo, lakini pale wawakilishi hao wanapokuwa wakiomba kupigwa tafu ili kufanikisha mipango yao, kila mmoja huziba pamba masikioni.

Pia kujitokeza dakika za mwisho za kwenda kwenye mafanikio kwa timu zetu wakiwamo wanaojitolea ahadi ya fedha na nyingine kemkem, wamekuwa wakitibulia timu husika na ambao kama Mwakinyo hatakuwa makini watamtibulia hata yeye kwenye safari yake ya kwenda kupigana na Wanik.

Tuliona kwa Taifa Stars ilipokaribia kwenda fainali za Afcon 2008 namna ilivyopata ushindi wa 1-0 dhidi ya Burkina Faso nyumbani kwao, ulivyowatia kiburi nyota wa timu hiyo na kujikuta wakipotezwa na Msumbiji nyumbani.

Serengeti Boys iliyokuwa ikikaribia kwenye fainali za Afcon U17 za mwaka jana, wadau walijitokeza mwishoni ilipokata rufaa na kufuzu, lakini mapema hakuna aliyekuwa anajua timu hiyo ya Vijana ilikuwa inajiandaa vipi kama sio juhudi binafsi za aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Hata Mwakinyo amekaririwa namna alivyosafiri kwa kuungaunga hadi kwenda Uingereza na kuitoa kimasomaso Tanzania, lakini ushindi wake umewatoa watu mafichoni na kujitokeza kumuunga mkono sasa.

Ni jambo zuri na linalotia moyo, lakini tahadhari yetu wanaompongeza sasa washiriki kumsaidia katika maandalizi na safari yake ya Ujerumani ili aende kubeba taji la IBF kwa Vijana. Wasisubiri arudi na taji ndipo tujitoe kimasomaso.

Hata hivyo, hata kwa bondia mwenyewe, hakumbuke ya Uingereza yameisha na sasa ni wajibu wake kujipanga kwa mchezo wake ujao dhidi ya Wanik, Oktoba 20 sio mbali, afanye maandalizi mazuri ili aenda kufanya kweli tena. Hili ndilo muhimu.

Watanzania tuko nyuma yako, tunakutakia maandalizi mema ya pambano lako hilo ili uzidi kuiletea sifa nchi yako na kuwapa hamasa mabondia wengine wa nchini kuthubutu kama ulivyothubutu.