Mwakinyo anafurahia ushindi na watanzania au anatusuta

Muktasari:

  • Kama mipango ya binadamu peke yake ingekuwa inatosha kutimiza mambo na maazimio, Dolores asingeweza kuwa mwanamke maarufu duniani. Asingeitwa mama wa kijana gwiji wa soka ulimwenguni, anayeichezea Klabu ya Juventus na Timu ya Taifa ya Ureno.

DOLORES Aveiro ni mama wa staa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anaitwa mama wa stadi huyo wa mpira wa miguu kwa kudura za Mungu. Matunda anayokula kupitia mwanaye hakika hakuyastahili. Maana anakula raha alizojaribu kuzihujumu.

Kama mipango ya binadamu peke yake ingekuwa inatosha kutimiza mambo na maazimio, Dolores asingeweza kuwa mwanamke maarufu duniani. Asingeitwa mama wa kijana gwiji wa soka ulimwenguni, anayeichezea Klabu ya Juventus na Timu ya Taifa ya Ureno.

Dolores hakumtaka Ronaldo wakati ikiwa mimba, lakini sasa hivi anatamba huku na huko kwamba yeye ndiye mama mzaa nyota. Mungu alimlinda Ronaldo.

Mama huyo, alikusudia hasa kukatisha maisha ya Ronaldo akiwa bado mimba, kwani hata madaktari walipomshauri asifanye hivyo, alitumia mpaka njia za kienyeji.

Dolores ameandika kitabu na kukiita kwa Lugha ya Kireno, Mae Coragem (Mother Courage), maana yake ikiwa ni Ujasiri wa Mama. Ndani ya kitabu hicho Dolores anasema: “Nililenga kutoa mimba ya Ronaldo. Nilitumia njia nyingi bila mafanikio.”

Anaongeza: “Madaktari waligoma kunisaidia kutoa mimba, uamuzi uliofuata baada ya hapo ikawa ni kunywa pombe kali ili kuitoa. Lakini sikupata matokeo niliyohitaji.

“Nilitumia kila njia nikashindwa. Sikutaka kumzaa Ronaldo. Sikujua kama atakuja kuwa huyu anayenifanya nijivunie kuwa mama.”

Ronaldo anajua hila za mama yake, na siku moja alimrudi, akamwambia: “Mama angalia, ulitaka kunitoa nikiwa mimba na sasa mimi ndiye kinara wa nyumba yetu. Unanitegemea na familia yetu yote inanitazama mimi.

“Tazama jinsi ambavyo dunia inanitazama. Naitwa mchezaji mkubwa duniani. Kila klabu kubwa ya soka duniani ingependa kupata huduma yangu. Unadhani hii ni fahari yangu peke yangu? Inakuhusu na wewe mama yangu. Unapaswa kujivunia sana kuwa na mtoto kama mimi.

“Hata hivyo, usingenipata kama ungefanikiwa kutoa mimba. Unaweza kuona somo unaloweza kutoa kwa wanawake wengine kuhakikisha wanatunza mimba na kuwalea watoto wao ili waje kujivunia uwepo wao. Pengine wakawa watoto wenye umashuhuri mkubwa duniani.”

Mume wa Dolores, Dinis Aveiro ambaye ni baba wa Ronaldo, alishatangulia mbele za haki kwa maradhi ya kuharibika kwa ini, ikiwa ni matokeo ya kuathirika na unywaji pombe kupita kiasi.

Je, Dolores ana uhakika gani? Jinsi Ronaldo anavyofurahia naye mafanikio ya kimaisha, inakuwa ni furaha isiyo na mawaa au anamsuta, kwamba angefanikiwa kuitoa mimba yake yote anayopata sasa asingeyapata.

VIPI KUHUSU MWAKINYO

Septemba 8, mwaka huu, bondia Mtanzania kutoka Tanga, Hassan Mwakinyo, aliushangaza ulimwengu, alipomchapa Muingereza Sam Eggington, kwa technical knockout (TKO), raundi ya pili. Pambano lilifanyika kwenye Uwanja wa Birmingham, jijini Birmingham, Uingereza.

Usongo wa Mwakinyo umemharibia Eggington rekodi yake. Kabla Eggington hajakutana na Mwakinyo, alikuwa ameshacheza mapambano 27, akishinda 22, KO 15, alipoteza manne. Na yote hiyo aliyopigwa, yote ni kwa pointi, yaani kwa uamuzi wa marefa.

Maana yake ni kuwa Eggington alikuwa hajawahi kupigwa kwa KO. Pambano lake la 28, dhidi ya Mwakinyo, likamchafulia gazeti. Raundi ya pili tu akawa amekaa. Mpaka hapo inatosha kuonesha namna Mtoto wa Kitanga alivyofanya kazi ya heshima. Alichokifanya Mwakinyo kwa Eggington ndiyo tafsiri halisi ya Kibanga kumpa kichapo Mkoloni.

Unadhani Mwakinyo amefanya kazi nyepesi? Tulia uambiwe. Kwanza jinsi Birmingham Arena ilivyotapika watu, ilitosha kuonyesha kwamba usiku ule haukuwa wa watoto. Watu waliingia kuona ndonga. Bahati mbaya, wengi walisubiri Eggington ampe kichapo Mwakinyo. Hawakujua Mwakinyo ndiyo Kibanga mwenyewe, huwa hachekicheki na Wakoloni.

Kikubwa ni rekodi. Pambano lilikuwa uzito wa welterweight. Yaani juu ya kg63.5 na pungufu ya kg66.7. Na Eggington ameshavalishwa nyota nyingi katika mapambano ya uzito huo, hivyo wasiwasi ulikuwa mdogo sana upande wake. Alijua Mwakinyo angepokea ndonga za kutosha na kurudi Bongo na nundu kadhaa za usoni.

Eggington amewahi kuwa bingwa wa Ulaya (bara zima la Ulaya) uzito huo wa welterweight. Alishakuwa bingwa wa Uingereza na Jumuiya ya Madola uzito huo huo. Alikuwa akimiliki taji la fedha la Baraza la Boxing Duniani (WBC) Kimataifa, yaani WBC International.

Bodi ya Usimamizi na Boxing Uingereza (BBBofC), imeigawa nchi hiyo katika kanda nane ambazo zinaitwa halmashauri. Halmashauri ya Midlands, taji la British Masters Silver, lilikuwa likimilikiwa na Eggington. Kama unatumia njia ya kawaida kuwaza, ile ya kutumia akili, utabaini kwamba Eggington ni bondia ‘sirias’, hivyo Mwakinyo amemchapa bondia sirias.

Ni sababu hiyo, Mwakinyo amepaa daraja kutoka nafasi ya 174 mpaka ya 16 duniani. Amepaa hivyo kwa sababu amemdunda kirahisi bondia aliyekuwa nafasi ya nane. Na kwa mshangao alioutengeneza, amefanya wadau wa Boxing kutamani pambano kati ya Mwakinyo na bondia mkubwa duniani, Kell Brook.

Hapa achana na stori za kupindisha za mkalimani Rashid Nassor ‘Chidy Mzee wa Mbele’, hii ni kweli kabisa kuwa wadau wa Boxing Uingereza wamemshauri promota wa Brook, Eddie Hearn wa taasisi ya Matchroom Boxing, kwamba kama anataka mshindani wa kweli dhidi ya bondia wake, basi Mwakinyo anafaa.

Matchroom Boxing wanashughulikia uwezekano wa Brook kutifuana na supastaa Amir Khan Desemba mwaka huu. Wanashauri kwamba ikitokea pambano hilo limeshindikana, basi ni fursa kwao kumtazama Mwakinyo. Ukimtazama Brook yupo nafasi ya tano. Unataka uambiweje kuwa Mwakinyo ameshakwea ‘levo’ za mbali?

Wikiendi iliyopita Khan alisema anatambua shauku kubwa ya wadau wa Boxing kuona anapigana na Brook. Amesema yupo tayari kupigana naye, lakini uwanja lazima uwe Wembley, vilevile pambano lifanyike mwakani. Hivyo, mipango ya Desemba haiwezekani. Vipi Mwakinyo akipata shavu hiyo Desemba? Anaweza kufanya maajabu mengine na mwakani akamvaa Khan. Ndoto iliyoje?

TUSIACHE KUJIULIZA

Pambano la Mwakinyo na Eggington lilikuwa la utangulizi. Shughuli kamili ilichezwa kati ya Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas. Khan alishinda kwa pointi. Mwakinyo alipata mchongo wa kupigana Birmingham Arena ndani ya wiki mbili kabla ya pambano. Muda huohuo akautumia kujiandaa kwa safari pamoja na mchezo.

Maelezo ni kwamba Eggington alikuwa apigane na bondia kutoka Ghana. Baada ya kushindikana kwa Mghana ndipo video ya Mwakinyo akijifua kwa kutumia tairi la gari badala ya punching bag ilipoonwa na waandaaji wa pambano. Akapewa mchongo, akasafiri kwenda Uingereza kukichafua dhidi ya Eggington. Mazingira hayo ya zimamoto ni sababu iliyowapa imani Waingereza kwamba, Mwakinyo angenyooshwa kirahisi.

Eneo la kujiuliza linakuja kwenye taarifa ya namna Mwakinyo alivyosafiri kwenda Uingereza. Hakuwa na fedha. Mwenyewe anasema ni mtoto wa kimaskini ndiyo maana hana uwezo hata wa kununua punching bag na kuishia kufanya mazoezi kwa kutumia tairi. Hivyo alihitaji msaada kusafiri.

Mwakinyo alisema alikutana na mizengwe mingi kupata viza. Fedha ya nauli na ya kulipia viza ilibidi aazime kwa mwanafunzi ambaye hakumtaja. Alisimulia kwamba kama si kutokata tamaa na kutumia mpaka njia ambazo si halali, asingeweza kwenda Uingereza kupambana.

Hapo ni kusema kwamba Mwakinyo alikuwa hana wa kumshika ili kufanikisha safari yake. Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lipo wapi? Vyama na mashirikisho ya masumbwi yaliyojaa nchini yalikuwa wapi? Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, milango yake inafunguliwa kwa funguo zipi mpaka Mwakinyo akashindwa kuingia kuomba msaada aweze kusafiri? Aliondoka kwa kujipigania mwenyewe. Leo hii Mwakinyo ameshinda kila mmoja anafurahia ushindi wake. Naye anafurahi na Watanzania. Hapa tunapaswa kujihoji; Mwakinyo anafurahi na Watanzania kutoka moyoni au anawasuta kwamba, pamoja na kumyima sapoti bado ameweza kutoboa?

Ijumaa iliyopita Mwakinyo alipewa Sh7.8 milioni bungeni. Alikutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa faragha, nyumbani kwake Dodoma. Haya yote ni heri, ila ilitakiwa hizi pesa azipate wakati wa kujiandaa. Angeshindwa ingekuwaje? Uwekezaji unapaswa kufanyika wakati wa maandalizi, sio kipindi cha kusherehekea ushindi.