Mourinho aongoza kura za kufutwa kazi England

Thursday August 9 2018

 

MATOKEO ya hovyo hovyo kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya zimeibua mengi huko Manchester United.

Kocha wake, Jose Mourinho amekuwa akibwabwaja tu hovyo, kulalamikia usajili kwamba bosi wake anayehusika na mambo hayo, Ed Woodward hajafanya mambo anayoyataka. Kutokana na timu kutibua kwenye mechi za kirafiki, Man United ikishinda mara moja tu kati ya sita na Mourinho kuripotiwa kutibuana na Woodward, imefanya jambo hilo limfanye Mreno huyo kuwekwa kwenye jopo la kuwa kocha wa kwanza kufutwa kazi kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2018/19.

Kwenye Top Six ya Ligi Kuu England hivi ndivyo kura zinavyofichua ni kocha gani atakumbana na fagio la kufutwa kazi mapema zaidi kwa mujibu wa mashabiki.

6.Pep Guardiola - kura 57

Chama la Pep Guardiola, Manchester City ndilo linalopewa nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Kama hilo litatokea basi litakuwa limetetea ubingwa huo ambao iliubeba msimu uliopita.

Kwa ubora wa kikosi chake huwezi kuona kama Guardiola kuna nafasi ya kufutwa kazi mapema huko Etihad na ndio maana kuna kura 57 tu zinazosema Mhispaniola huyo anaweza kufukuzwa kazi mwaka huu. Kura 390 zinafichua Guardiola atabaki Man City hadi mwisho wa msimu.

5. Maurizio Sarri - kura 58

Kocha Mtaliano, Maurizio Sarri ametua Chelsea kuchukua mikoba ya Antonio Conte, lakini shida amekwenda kwenye timu ambayo suala la kufukuzwa kocha halijawahi kuwa tatizo. Maisha ya Stamford Bridge hayajawahi kuwa matamu kwa makocha kutokana na mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich kuwa na kawaida ya kuwafukuza makocha bwake mara kwa mara.

Sarri kutokana na hilo, kuna kura 58 zimepigwa zinazosema Mtaliano huyo hawezi kumaliza msimu na atafutwa kazi. Kwa upande wa kura ambazo zinaamini Sarri atamaliza msimu wote akiwa Chelsea ni 52 tu.

4.Mauricio Pochettino - kura 71

Tottenham imeonyesha kukiamini zaidi kikosi chake ilichonacho na kuamua kutokuwa bize kwenye suala la usajili kwenye majira haya ya kiangazi huko Ulaya. Kutokana na hali ya mambo ilivyo, Kocha Pochettino haonekani kuwa kwenye hatari ya kufukuzwa kazi kwenye kikosi hicho msimu huu. Kuna kura 330 zinazosema kocha huyo raia wa Argentina abaki kwenye kikosi cha Spurs hadi mwishoni mwa msimu, huku kuna nyingine 71 ndizo zinafichua uwezekano wa kocha huyo kufutwa kazi ndani ya msimu huu. Kwa kura hizo unaona bayana Pochettino atamaliza msimu akiwa bado na Spurs.

3.Jurgen Klopp - kura 110

Maisha ya Mjerumani Jurgen Klopp huko Liverpool hayaonekani kuwa magumu sana kwa upande wake na ni kocha ambaye mashabiki wanamini ataendelea kubaki kwenye kikosi cha Anfield.

Klopp amepigiwa kura 443 za kubaki kwenye timu hiyo, lakini kwa upande wa kura zinazodai hatamaliza msimu na atafukuzwa kazi ni 110. Hivyo kwenye Top Six, Klopp ni kocha namba tatu kwenye ile orodha ya waliopigiwa kura nyingi kuwa huenda wakafungashiwa virago vyao kwenye kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

2.Unai Emery - kura 117

Kurithi mikoba ya kocha maarufu kama Arsene Wenger halijawahi kuwa jambo jepesi na ndiyo maana Unai Emery anakuwa kocha namba mbili kwa wale waliopigiwa kura nyingi za kuweza kufutwa kazi kwenye Ligi Kuu England kabla ya msimu kumalizika.

Kocha huyo mpya wa Arsenal, amepigiwa kura 117 zinazofichua anaweza kufukuzwa kazi kabla ya msimu kumalizika. Lakini, kuna kundi jingine la mashabiki wa Arsenal na timu nyingine wanaoamini Emery atamaliza ligi na ndiyo maana kuna kura 310 zimepigwa kuonyesha kocha huyo Mhispaniola atabaki Emirates hadi mwishoni mwa msimu.

1.Jose Mourinho - kura 130

Mreno, Jose Mourinho ana kazi ya kufanya kuwaumbua mashabiki ambao wanaamini hawezi kumaliza msimu huu akiwa bado kocha wa Manchester United.

Kuna kura 130 zilizopigwa zinazodai Mourinho atafutwa kazi mapema tu kwenye kikosi cha Man United msimu huu. Hizo ndizo kura nyingi zaidi zilizopigwa kwenye orodha ya makocha wanaoweza kufutwa kazi mapema kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Kuna kura 44 tu ndizo zinazoamini Mreno huyo aliyejipachika jina la Special One atamaliza msimu huu wa 2018/19 akiwa bado kocha wa Man United kutokana na mambo kadhaa yanayoikabili timu yake.