Mliopanda Ligi Kuu pokeeni simu yangu

Muktasari:

Zilizopanda zinastahili pongezi kwa kuwa zimefanikiwa kutimiza malengo ambayo zilijiwekea kabla ya ligi hiyo kuanza.

NI uungwana kupongeza anayefanya vizuri. Nami sina budi kutoa pongezi zangu za dhati kwa timu zote zilizofanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza kwa maana ya kupanda daraja hadi kutinga Ligi Kuu Bara.

Zilizopanda zinastahili pongezi kwa kuwa zimefanikiwa kutimiza malengo ambayo zilijiwekea kabla ya ligi hiyo kuanza.

Pia ni uungwana kuwapa salamu za pongezi walioshindwa na hata walioshuka daraja.

Bila ya wao kushiriki na kushindwa, hakuna mshindi ambaye angepatikana.

Hata hivyo, pongezi hizi kwa timu zilizopanda daraja zinapaswa kutafsiriwa kama simu ya kuwaamsha. Kwa lugha ya Kiingereza hii ni ‘wake up call’ kwao.

Hapa ninamaanisha kwa Coastal Union ya Tanga, KMC ya Kinondoni Dar es Salaam, Biashara FC ya Mara, Alliance FC ya Mwanza, JKT Tanzania na African Lyon za Dar es Salaam.

Ni simu ya kuwaamsha kwa sababu timu hizi zinatakiwa kujipanga hasa ili kuwa na ushiriki mzuri Ligi Kuu msimu ujao. Muda uliosalia kabla ya msimu huo kuanza hauzidi miezi sita kuanzia sasa.

Msimu tulionao unatarajia kumalizika Mei kabla ya dunia nzima ya soka kuelekeza macho na masikio Urusi katika fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Juni. Ni mwezi huo utapita kwa kasi ya ajabu.

Baada ya hapo kutakuwa na mwezi mmoja tu iwapo ligi itaanza Julai au miezi miwili iwapo ligi itaanza Septemba.

Hivyo timu hizi zinatakiwa kuanza maandalizi sasa na si wakati mwingine kwa kuwa muda wa maandalizi ndio huu.

Maandalizi ya zama hizi ni makubwa zaidi kuliko ya miaka ya nyuma.

Kwa nyakati hizi za sasa, pamoja na mambo mengine timu zinazoshiriki Ligi Kuu zinatakiwa kukidhi matakwa ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ili ziweze kupata leseni ya kushiriki mashindano yaliyo chini ya shirikisho hilo.

Mtakumbuka, utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za CAF wa klabu ulianza tangu mwaka 2010.

Japo hapa Tanzania hatujafanikiwa kuutekeleza, lakini mahitaji yake ni pamoja na klabu kuwa na wataalamu katika nafasi muhimu za uongozi ili ziweze kuendeshwa kwa kuzingatia weledi.

Hii ni kwa kuwa soka sasa linaendeshwa kibiashara.

Pia kuna suala la miundombinu. Kwa sasa ni lazima klabu ya ligi kuu iwe na uwanja angalau wa kufanyia mazoezi.

Klabu zisizo na uwanja zinatakiwa kuwasilisha katika shirikisho mikataba baina yao na wamiliki wa uwanja watakaoutumia kwa mechi za nyumbani.

Ukiangalia mahitaji hayo tu utaona muda uliopo ni ni mfupi kwa timu hizo ukiachilia mbali JKT Tanzania ambayo mwaka jana ilizindua uwanja wake uliopo Mbweni, jijini Dar es Salaam, ambao pia ulitumika kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza.

Lakini pia changamoto ya gharama za uendeshaji wa timu zenyewe ikizingatiwa kwa sasa kazi ya kucheza soka kwa mchezaji ni ajira.

Hivyo kunapaswa kuwepo mna uhakika wa namna maisha ya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi watakavyoishi.

Hapa namaanisha uhakika wa mishahara.

Ni hapo ndipo linapokuja suala la kutafuta washirika au wabia wa kushirikiana nao, kwa lugha rahisi-wadhamini kama tunavyoona kwa baadhi ya timu zenye mikataba ya namna hiyo; Simba, Yanga, Azam, Mbao na Singida United ambazo zina udhamini wa kampuni mbalimbali.

Kufanikisha mambo yote haya kunahitaji muda wa kujipanga, kwanza kiuongozi kabla ya kushirikisha washirika wengine.

Hivyo ni wakati wa timu hizi sita zilizopanda kuanza kujipanga kwenye maeneo hayo ili isije ikawa zimepanda ili zishuke ghafla kwa kukosa mikakati endelevu kama hii niliyoitaja.

Nikimalizia, ninataka kuwakumbusha zaidi kuwa waanze kusaka wadhamini, wafadhili kwa ajili ya kupunguza makali.

Ninafahamu timu zilishangilia kupanda Ligi Kuu, zilipiganma kupanda Ligi Kuu, sasa wamepata kilichokuwa kinatakiwa, kinachofuata ni kupambana kupata wahisani. Huku gharama ni kubwa kuliko hata hizo za Ligi Daraja la Kwanza zilizomalizika hivi karibuni,

Kwa leo naomba kuishia hapa, nasubiri mrejesho kutoka kwenu.