INAWEZEKANA: Mike Ashley anahitaji kusepa Newcastle United

Muktasari:

Ingawa Newcastle United haijashinda mataji mengi ukilinganisha na klabu kama Liverpool na Man United, timu hiyo bado ni kati ya klabu kubwa zaidi England na yenye historia kubwa barani Ulaya.

MSOMAJI, Mike Ashley ni Mwingereza anayemiliki klabu ya Newcastle United England.

Ingawa Newcastle United haijashinda mataji mengi ukilinganisha na klabu kama Liverpool na Man United, timu hiyo bado ni kati ya klabu kubwa zaidi England na yenye historia kubwa barani Ulaya.

Mashabiki wengi wa soka wakisikia Newcastle wanamfikiria Alan Shearer, ambaye ni Mwingereza mwenye rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu ya England. Mchezaji huyu alifunga idadi kubwa ya mabao hayo akiwa katika jezi ya Newcastle. Wengi pia wanaitambua klabu ya Newcastle kwa kuwa ina mashabiki wenye jina la utani la ‘Jordis’ ambao wanachangamka sana katika mechi zao za nyumbani.

Lakini katika misimu ya karibuni, sauti kutoka jukwaa la St. James Park, uwanja wa nyumbani wa Newcastle, zimepungua.

Chini ya uongozi wa Mike Ashley imekuwa wazi, Newcastle haijatapata mafanikio makubwa. Shida imekuwa ni kwa sababu Ashley ni mfanyabiashara na ameimudu Newcastle kama biashara. Lengo kubwa la Ashley si kwa klabu hiyo kupata mafanikio makubwa, lengo lake kwa Newcastle na yeye kupata fedha nyingi tu.

Kutokana na falsafa hiyo Mike Ashley hajataka Newcastle iwasajili wachezaji kwa fedha nyingi. Pia, amekataa kutumia fedha zake kusajili wachezaji. Na badala ya kujaribu kuhakikisha kwamba, wachezaji bora katika kikosi cha Newcastle wanabaki katika klabu hiyo, Ashley amekubali kuuza wachezaji nyota kila baada ya msimu.

Katika miaka ya hivi karibuni Newcastle imeuza wachezaji wake nyota kama Yohan Cabaye, Demba Ba, na Mathieu Debuchy. Kwa kweli Newcastle ilipata fedha nyingi kutokana na kuuza wachezaji wake hao. Lakini chini ya Ashley, Newcastle imesajili wachezaji kwa bei nafuu ambao wameshindwa kuziba pengo la wachezaji hao.

Misimu miwili iliyopita Newcastle ilishuka daraja kutokana na kutokuwa na kikosi chenye uwezo wa kupambana katika Ligi Kuu.

Msimu huu Newcastle imerejea katika Ligi Kuu lakini katika dirisha kubwa la uhamisho Mike Ashley alimkataza Kocha wa Newcastle, Rafael Benitez kusajili wachezaji ambao aliwahitaji.

Matokeo yake ni kwamba Newcastle sasa imeshika nafasi ya 15 na ipo katika hatari ya kushika mkia. Idadi kubwa ya mashabiki wa Newcastle kwa sasa inataka klabu yao ipate mmiliki mpya. Na wengi wanataka klabu ipate mmiliki kabla dirisha dogo la uhamisho kufungwa ili klabu yao ichukue uamuzi wa kusajili wachezaji wapya.

Mike Ashley ametangaza nia ya kuiuza Newcastle United. Na kuna tetesi wadau kutoka sehemu mbalimbali wapo tayari kuinunua klabu hiyo.

Bado haijajulikana kama Ashley atafanikiwa kuiuza Newcastle kabla dirisha dogo la uhamisho kufungwa.

Na inasemekana Ashley anashindwa kuiuza Newcastle kwa kuwa anataka kuiuza klabu hiyo kwa fedha nyingi sana.