Miguu yao inanukia noti kama wakisukwa vyema

KLABU zinazoaminika kuwa na fedha katika Ligi Kuu Bara kwa maana ya Simba, Yanga na Azam FC, zimefanikiwa kuwa na chipukizi wenye madini ya soka miguuni ambao wakisimamiwa, wanaweza kuzitajirisha timu hizo mbele ya safari.

Wachezaji hao wanaweza hata kuwapiku baadhi ya mastaa waliopitia klabu hizo na sasa wakitamba duniani kwa kuvuka mipaka ya nchi; wachezaji kama Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk au Simon Msuva anayekipiga Difaa El Jadida ya Morocco.

Katika makala haya Mwanaspoti linakutelea orodha ya chipukizi waliopo Simba, Yanga na Azam ambao wanaweza kuwapiku akina Samatta na Msuva kama wakikaza vyema.

AZAM FC

Kwa matajiri hawa wa Chamazi, Shaban Idd ‘Chilunda’ hivi karibuni alihamia Hispania. Ni baada ya kufanya makubwa katika Ligi Kuu Bara iliyopita na Kombe la Kagame ambapo timu yake ilitwaa ubingwa.

Kama ambavyo Samatta aliyeibukia African Lyon na kuitumia Simba kuwa mlango wa kutokea au Msuva aliyetokea Yanga, Chilunda naye amepenya, anafuata nyayo zao kwa kipaji alicho nacho.

Yahya Yayd

Ana kipaji cha aina yake akiongezewa na maarifa ya Kocha Hans Pluijm bila shaka Azam itamuuza kama ilivyofanya kwa Chilunda.

Ditram Nchimbi

Ni kati ya wachezaji wapya walioongezwa Azam sasa. Kujituma ndio siri klabu mbalimbali kumtolea macho licha ya timu aliyokuwa nayo msimu uliopita (Njombe Mji) kushuka daraja.

Ally Bizimungu, kocha wa Mwadui alikibaini kipaji chake na akakitaka lakini amemkosa. Akiendelezwa na mwenyewe akjituma, klabu yake na hata yeye mwenyewe atazikoga fedha.

SIMBA

Ndani ya kikosi hicho kuna chipukizi ambao wakiwa makini kwa kuzingatia maelekezo ya Kocha Mbelgiji Patrick Aussems, basi wanaweza wakawa habari nyingine na kuiletea Simba pesa na wao kulamba madili ya maana.

Rashid Juma

Ni winga matata kikosini humo, alipandishwa timu ya wakubwa na kocha aliyeondoka, Pierre Lechantre. Katika Kagame alikuwa anatoa mapande ya nguvu kwa Meddie Kagere. Anajituma, lakini kwa umri wake anatakiwa kupewa mwongozo sahihi, anaweza kuja kuipatia Simba fedha nyingi.

Ally Salim

Kuthibitisha uwezo wake amewapiku wakongwe Emmanuel Mseja na Said Mohamed ‘Nduda’. Anapokuwa langoni, kipa huyo huwa na hesabu kali za kudaka faulo, penalti na hata krosi, iwe kali vipi ataifuata tu.

Ni hazina nyingine Simba, kazi sasa ni kwa benchi la ufundi na viongozi kumjenga kiufundi na kisaikolojia ili muda si mrefu watavuna fedha kutoka kwake kama ilivyotokea kwa Samatta.

Abdul Khamis

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, anamwelewa vyema chipukizi huyu kwa namna anavyolijua goli. Ni jukumu la Djuma na bosi wake Aussems kuhakikisha wanakifikisha mbali kipaji chake kiufundi, pia nao uongozi umsaidie kupalilia ndoto zake.

YANGA SASA

Kwa sasa pale Jangwani kuna ukata, fedha imeota mbawa, ni hali ngumu. Lakini hiyo haijazuia vijana wenye miguu sahihi ya soka kutua hapo.

Feisal Salum ‘Fei Toto’

Uwezo wake unafahamika wazi. Ndio maana hata Singida United nayo ilimng’ang’ania kabla ya Yanga kumtuliza. Kazi imebakia kwa Kocha Mwinyi Zahera kumuongezea maujuzi.

Ni kiungo mtaalamu ambaye kama Yanga itamtumia vizuri, anaweza kuipa mafanikio uwanjani na hata kwenye akaunti yao atakapouzwa kwa bei nzuri kama akiongezewa makali

Ramadhan Kabwili

Alianza kung’ara akiwa timu ya taifa ya vijana U-17 ‘Serengeti Boys’ na Yanga haikutaka kumchelewesha ikamsajili. Kinachoonekana kwake anahitaji kuongezewa uzoefu, hiyo ni kazi ya kocha. Ni kipa chipukizi anayeweza kufika mbali hasa kama klabu itamsaidia kupita njia sahihi za kufikia ndoto zake za kucheza nje ya nchi.

Yusuph Mhilu

Hajaangaziwa sana na vyombo vya habari, lakini ni kati ya chipukizi wenye uwezo mkubwa ndani ya Yanga.

Kama Kocha Zahera analo jicho zuri, atakuwa ameshabaini utajiri uliojificha kwa mchezaji huyu. Anaweza kuinua uchumi wa klabu sambamba na wake akinolewa vyema na kuzingatia.