Miaka 45 ya harakati za Hip hop

ILIKUWA Agosti 11, 1973, kwenye ukumbi mmoja uliokuwa kwenye jengo fulani katika mtaa wa 1520 Sedgwick Bronx, New York, Marekani pale kijana wa miaka 18 mwenye asili ya Jamaica, Clive Campbell maarufu kama DJ Kool Herc, alipokuwa akiwarusha watu kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa aliyomwandalia dada yake.

Wakati akifanya makamuzi, DJ Look Herc aliamua kubuni kitu cha tofauti na vilivyozoeleka. Badala ya kupiga wimbo kamili, yeye alipiga ala (instrumental) pekee huku rafiki yake, Coke La Rock, akishika kinasa sauti na kuchombeza kwa maneno ya hapa na pale...! Hivyo ndivyo Hip Hop kama muziki, ilivyozaliwa.

HIP HOP KAMA MUZIKI

Mwanzoni, jina la muziki huu mpya, yaani HIP HOP, halikuwa maarufu sana hadi mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa 1980 pale vilipoibuka ‘vichwa’ kama Rakim, KRS-One, Slick Rick, Kool G Rap, Roxanne Shante, Big Daddy Kane, LL Cool J, Ultra Magnetic MCs, Schooly D na wengine wengi waliokuja na ubunifu wa kucheza na maneno.

HIP HOP KAMA UTAMADUNI

Watu hawa wakahusisha muziki huu na maisha yao ya kawaida na kufanya kuwa zaidi ya muziki...ukawa utamaduni. Kwa mujibu wa vuguvugu la harakati za Hip-Hop la Zulu Nation lililonzishwa na Afrika Bambataa, Hip Hop imegawanyika katika nyanja kuu nne; U-DJ (Deejaying)- ndicho alichokifanya Kool Herc. U-MC (Emceeing)- ndicho alichokifanya Coke La Rock. Mabreka (Breaking) na uchoraji wa ukutani.

Pia kwa mujibu wa vuguvugu jingine la Hip Hop la The Temple of Hip Hop lililoanzishwa na gwiji wa rap, KRS-One, Hip Hop inajumuisha nyanja zingine kama kuigiza midundo ya muziki kwa mdomo (beat-boxing), mitindo ya kitaani (street fashion), lugha za kitaani (street language), elimu au maarifa ya kitaani (street knowledge) na ujasiriamali wa kitaani (street entrepreneurialism).

HIP HOP KAMA HARAKATI

Wakati Hip Hop inazaliwa, 1973, Jiji la New York, hasa kitongoji cha The Bronx, lilikumbwa na bomoa bomoa kubwa kupisha ujenzi wa Barabara Kuu ya Cross Bronx Expressway mwaka 1972.

Nyumba nyingi za watu masikini zilivunjwa na kusababisha machungu. Vijana waliokulia kwenye familia zilizoishi kwenye maeneo yale, wakajikuta kwenye wakati mgumu hivyo wakatafuta kitu watakachokitumia kama utambulisho wao na kupaza sauti ili taifa lisikie maumivu yao. Kwa hiyo, ujio wa muziki huu ukawa majibu ya maswali yao na ndipo wakaukumbatia.

MJADALA WA BONGO FLAVA

Hip Hop ilianza kuingia nchini Tanzania miaka ya mwishoni ya 1980. Waimbaji wa mwanzo kabisa hawakuwa wakitunga nyimbo zao wala kutengeneza midundo yao, badala yake, walitunga mashairi kwa kufuata mtiririko wa nyimbo za Kimarekani na midundo ile ile lakini waliimba kwa Kiswahili.

Kwa kuwa nyimbo zenyewe na midundo ilikuwa ya Kimarekani lakini iliongezewa ladha ya kibongo ya Kiswahili...ndipo ilipoitwa Bongo Flava. Ladha ya kibongo yaani Bongo Flava, haikuishia kwenye lugha pekee bali hadi ujumbe ulioimbwa. Nyimbo hizo hazikuwa tafsiri ya zile za Marekani bali zilitungwa kuyalenga maisha halisi ya kibongo. Heshima kubwa iende kwa Saleh Jabir ambaye anatajwa kama baba wa Bongo Flava. Yeye ndiye aliyepita kwenye mistari ya nyimbo zilizotamba sana wakati ule, kama Ice Ice Baby wa Vanilla Ice wa mwaka 1990. Nitautumia kama mfano ubeti wa kwanza wa wimbo wa OPP wa Naughty By Nature ambao Saleh J alipita nao kibongo flava.

Naughty By Nature

OPP, how can I explain it. I’ LL take you frame by frame. To have why’all jumpin’ shall we singin’ it. O is for Other, P is for People scratchin’ temple. The last P...well.. that’s not that simple. It’s sorta like another way to call a cat a kitten.

Saleh J

OPP, how can I explain it. Kila mmoja kwa pembeni. Kwa kungoja kurest ‘tasema nini. O for All PP for Pure Penzi. Mtoto muweke ndani hakikisha anakuenzi. Vibishoo vya mtaani vyote avione sio kitu. Asijali Honda wala Mercedes Benz.

Utaona alichokiimba Saleh Jabir hakikuwa na uhusiano wowote na walichokiimba Naughty By Nature wenyewe.

Saleh Jabir ameunga unga OPP anavyojua yeye akatokea kwenye mapenzi na vita dhidi ya mabishoo. Hivyo ndivyo mambo yalivyoanza.

Miaka mingi ikapita na Bongo Flava ikakuwa kiasi cha vichwa vipya kuja na kuanza kutunga mashairi yao kwa kutumia midundo yao.

Makundi kama Kwanza Unit na Diplomatz na watu kama Father Nelly na baadaye 2Proud walibadilisha upepo wa Bongo Flava. Kadri siku zilivyozidi kusonga na muziki huu ukavutia watu wengi zaidi ambao nao walikuja na ubinifu wao.

Watu kama kina Ebony Molim wakaja na aina mpya ya Bongo Flava, badala ya kurap, wakawa wanaimba...mambo yakazidi kunoga.

Ujio wa aina hii ya Bongo Flava ukaanza kuwatofautisha wale wa kurap na hawa wa kuimba kiasi cha maingizo mapya ya kurap kuanza kulikataa jina la Bongo Flava na kujiita Hip Hop huku jina hilo la kizalendo likisukumiwa kwa waimbaji ambao huitwa wabana pua.

Wakati umefika sasa wa kizazi kipya cha Hip Hop Tanzania kufahamu asili ya BONGO FLAVA ni Hip Hop ya kimarekani iliyowekewa vionjo yaani ladha ya Kibongo na wala siyo vinginevyo.