NINACHOKIAMINI: Matola huyu, tutakuja kumkubali siku si nyingi

Muktasari:

Tatizo kubwa ambalo limezikumba nchi nyingi hasa zinazoendelea, hususan zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ni matumizi ya hovyo ya mitandao ya kijamii.

KILA nchi ina changamoto zake, hata mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa kiuchumi, hayawezi kukwepa baadhi ya changamoto.

Tatizo kubwa ambalo limezikumba nchi nyingi hasa zinazoendelea, hususan zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ni matumizi ya hovyo ya mitandao ya kijamii.

Nikiri kuwa mitandao ya kijamii imesaidia sana kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja, vikundi, jamii na hata nchi kwa jumla.

Lakini mitandao ya kijamii pia imesababisha migogoro mingi kati ya mtu na mtu, jamii na jamii hata taifa kwa taifa.

Matumizi ya mitandao ya kijamii yakitumiwa vibaya huwa inaharibu na ndio maana tunapaswa kuwa makini tunapotumia.

Nilikuwa namuangalia Kocha wa Lipuli, Selemani Matola alivyokuwa na hasira wakati timu yake ilipokuwa inacheza na Simba.

Hazikuwa hasira za mechi, zilikuwa hasira za mitandao ya kijamii. Alikuwa anatuhumiwa kuwa ‘ameuza mechi’. Alikuwa katika wakati mgumu.

Sikuona hilo tu, niliiona falsafa ya Simba ilivyokuwa inafanya kazi katika klabu ya Lipuli.

Katika makocha wa Tanzania kwa sasa, Matola anaweza kuwa kocha mwenye ujuzi zaidi kuliko wengine wote wazawa.

Maana yangu ni kuwa Matola, amekuwa kocha msaidizi wa Simba akiwa na makocha wenye majina makubwa kuanzia Mzambia, Patrick Phiri hadi Mfaransa, Patrick Liewig.

Pia, Matola amekuwa nahodha wa Simba chini ya makocha wenye majina makubwa kama Mkenya, James Siang’a, Syllersaid Mziray na Talib Hilal. Kwa jumla kama ni shule, Matola amepata mafunzo kutoka kwa makocha mbalimbali wenye majina makubwa na kwa idadi ya chini wanaweza kufika hata 10.

Kwa mtu ambaye anajielewa kama Matola, hawezi kukosa kitu fulani na hakika tumeliona hilo katika timu ya Lipuli dhidi ya Simba.

Ukiangalia aina ya wachezaji wa Lipuli na jinsi wanavyocheza katika mechi mbalimbali, unaiona falsafa ya Kisimba-Simba.

Ukweli huo hauwezi kufichika na nzuri zaidi hata kocha mwingine wa timu hiyo ya Lipuli, Amri Said naye ameichezea Simba kwa miaka kadhaa ingawa hakupata nafasi kubwa kama Matola katika benchi la ufundi la Msimbazi.

Nikiangalia Lipuli inavyocheza pamoja na hali duni, ninaona jinsi Matola anavyoweza kuwa kocha mwenye mafanikio siku za mbele.

Kama atakuwa anakumbuka mbinu za makocha aliokuwa nao Simba, halafu na yeye mwenyewe akajiongeza katika mafunzo ya ukocha yanayotolewa na Shirikisho la Soka la Africa (Caf), sioni sababu kwanini miaka mitano ijayo asiwe miongoni mwa makocha wenye mafanikio makubwa nchini.

Jambo jingine ambalo limenifurahisha kwake ni kuonyesha uweledi katika kazi yake na kuondoa hisia za baadhi ya mashabiki kuwa angeuza mechi kwa timu yake ya zamani.

Katika soka la fitina, ungetegemea Simba ipate mechi rahisi dhidi ya Lipuli, kwa sababu ya makocha wake kuwa ni wachezaji wa zamani wa Simba lakini pia ni kama wanafamilia ya Msimbazi.

Lakini, Matola na mwenzake Amri Said waliweka pembeni ushabiki na wakaonyesha uweledi wao na hakika tulifurahia soka.

Matola hana sababu ya kuwa na hasira ya mitandao ya kijamii, badala yake mitandao hiyo inatakiwa kumpa motisha zaidi ili awe kocha bora nchi hii, na hilo linaliona.

Ndani ya miaka mitano Matola hatakuwa kama sasa, atakuwa miongoni mwa makocha bora nchi hii.

Nikimkumbuka Matola aliyekuwa nahodha wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika 2003, baadaye akawa kocha msaidizi, sasa akiwa Lipuli, naona miaka mitano akiwa kocha ambaye kila timu itataka kuwa naye.