Man United itafanya vizuri chini ya kocha mwingine

JOSE Mourinho ni kocha ambaye amezijenga timu nyingi. Ni kocha mwenye uzoefu wa miaka mingi na pia ni kocha ambaye ametokea kupata mafanikio katika kila klabu aliyoifundisha. Hii ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga msingi imara.

Haina ubishi wala shaka yoyote kwamba timu za Mourinho zimekuwa na uwezo mkubwa wa kukaba. Huwa zinakuwa na ngome za uhakika.

Mourinho alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2010 akiwa na Inter Milan kwa kutumia mchezo wa kujihami ‘kupaki basi’ huku timu yake ikifunga mabao ya mashambulizi ya kushitukiza.

Mashabiki wa Inter Milan wanajua timu yao haikucheza mpira wa kuvutia chini ya Kocha huyo Mreno, lakini wataendelea kumkumbuka kwa mazuri kutokana na mafanikio ambayo timu hiyo iliyapata chini yake.

Msimu uliopita, Manchester United, iliishia nafasi ya pili katika Ligi Kuu England. Hata hivyo, mashabiki wengi wa timu hiyo walimlaumu na kumkosoa Mourinho kadiri msimu ulivyoendelea, hiyo ilitokana na namna Man United ilivyocheza soka lisilo la kuvutia.

Wiki iliyopita msimu mpya wa Ligi Kuu England ulianza tena. Jinsi mambo yalivyokuwa, ni sawa tu kusema Man United ilianza pale ilipoishia msimu uliopita.

Sawa ilishinda mechi ya ufunguzi dhidi ya Leicester City mabao 2-1, lakini ni ukweli kuwa timu hiyo haikucheza mpira wa kuvutia. Mourinho alionyesha tena anaridhika na mchezo ule.

Kocha huyu ameshawahi kusema kushinda mataji ni muhimu zaidi kuliko kucheza mpira wa kuvutia. Shida ni kwamba kama unashindwa kushinda mataji huku pia unacheza mpira ambao hauvutii, hautaweza kueleweka kwa mashabiki.

Uvumilivu wa mashabiki wa United ulijaribiwa mara nyingi msimu uliopita na bila mafanikio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo kwa msimu huu siamini kama Mourinho atapata nafasi kuumaliza mkataba wake.

Mashabiki wa United wanajua wana kikosi ambacho katika karatasi kina uwezo wa kushinda Ligi Kuu England. Ni kwa sababu inao watu kama Paul Pogba, Nemanja Matic, David de Gea, Alesis Sanchez, Lumelu Lukaku na Eric Bailly. Wote hao ni kati ya wachezaji bora zaidi duniani katika nafasi zao. Hapo bado sijawataja Marcus Rashford na Antony Martial, wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani.

Hata hivyo, katika mfumo na harakati za Mourinho, wachezaji kama Lukaku, Pogba na Rashford hawajapata nafasi kuendelea kimpira.

Kwa takribani mwezi mmoja sasa, Mourinho ameukosoa uongozi wa Manchester United na amedai hajapata nafasi kusajili wachezaji ambao anawahitaji.

Lakini kwa mtazamo wangu shida ya Manchester United si kwamba haina kikosi kizuri, bali haina kocha mwenye uwezo wa kukitumia vizuri. Mourinho ana nafasi msimu huu kubadili aina yake ya soka na kucheza mpira wa kushambulia zaidi. Lakini kama anaendelea kucheza mpira wa kujihami bila kupata mafanikio makubwa, basi hatastahili kuwa kocha wa Manchester United.