MAONI YA MHARIRI: Makocha wasaidie kuwabeba nyota wa Serengeti Boys

Muktasari:

Wachezaji wa timu hiyo walikwenda kujiunga na timu za Ligi Kuu pamoja na madaraja ya chini

TUNAAMINI kila mmoja anakikumbuka vyema kikosi cha Serengeti Boys kilichokwenda nchini Gabon, mapema mwaka huu katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.

Kikosi hicho kilifuzu kwa mara ya kwanza kushiriki fainali hizo kubwa zaidi kwa vijana Afrika, na kwa bahati mbaya kiliishia katika hatua ya makundi.

Kwa miaka mingi, Tanzania ilikuwa ikisaka tiketi ya kufuzu kushiriki katika mashindano hayo na kuangukia pua, kabla ya mwaka huu kutolewa kimasomaso na vijana hao.

Nyota hao, punde baada ya timu hiyo kuvunjwa kutokana na wengi wao kuanza kuvuka umri, ipo haja ya kuwaendeleza kwa kuwatafutia nafasi ya kucheza mechi nyingi za mashindano. Hivi sasa unaweza usifahamu nyota wale wote walipo. Inawezekana ni asilimia ndogo tu wanaendelea na soka.

Wachezaji wa timu hiyo walikwenda kujiunga na timu za Ligi Kuu pamoja na madaraja ya chini, lakini ni wachache wamefanikiwa kuwa na nafasi za kucheza kila wakati.

Mchezaji anayeonekana kupiga hatua kutoka kikosi hicho cha Serengeti Boys ni Shaaban Zubeiry Ada anayeichezea Lipuli ya Iringa.

Ada amekuwa sehemu kubwa ya kikosi cha Lipuli, akicheza katika mechi nyingi.

Amekuwa akipangwa pia katika mechi ndogo na kubwa.

Msimu huu amekuwa na kiwango bora alipocheza dhidi ya Yanga na kisha Azam na kwa kiasi kikubwa aliwazima viungo wa timu pinzani uwanjani.

Bahati mbaya kwa Ada ni kwamba, anacheza katika nafasi ya kiungo ambayo kwa hapa nchini imejaa nyota wengi wanaofanya vizuri, jambo ambalo linamnyima fursa ya kuanza kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Ni vigumu kumuacha Himid Mao, Jonas Mkude, Mudathir Hahya na wengineo na kumuita Ada.

Hata hivyo, tunapenda kuwapongeza makocha Selemani Matola pamoja na Amri Said kwa kutoa fursa kwa kijana huyu, ambaye bila shaka siku zijazo atakuwa mchezaji muhimu wa Taifa Stars.

Mchezaji mwingine, ambaye anapata wasaa wa kucheza kwenye timu za Ligi Kuu ni Abdul Suleiman aliyeko Ndanda ya Mtwara.

Kama una kumbukumbu nzuri, Abdul ni yule mchezaji wa Serengeti aliyepimwa kama anatumia dawa za kuongeza nguvu nchini Gabon.

Nyota huyo anayecheza nafasi za ushambuliaji amekuwa na kiwango kizuri pia licha ya kwamba, ana kazi ya kuendelea kufanya ili apate nafasi zaidi katika timu yake hiyo ya Mtwara.

Nyota mwingine anayepambana ni Dickson Job aliyeko Mtibwa Sugar. Job alipata nafasi katika baadhi ya michezo ya mwanzo wa msimu na kufanya vizuri, licha ya siku za karibuni amekuwa hapangwi.

Kwenye kikosi cha Mtibwa yupo pia Nickson Kibabage, ambaye bado hajaanza kupata nafasi ya kucheza kutokana na kiwango bora cha Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ katika upande wa kushoto.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, Kelvin Nashon ndiye amezidi kuimarika zaidi na msimu ujao huenda akarejea Ligi Kuu na timu yake ya JKT Ruvu.

Nashon alianza kutumiwa na kocha Bakari Shime katika kikosi cha Ruvu tangu msimu uliopita ikiwa Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja baadaye.

Bahati nzuri kwa Nashon ni kwamba, Shime ndiye aliyekuwa kocha wa Serengeti Boys hivyo anamfahamu vizuri na ndiyo sababu anampa nafasi ya kutosha katika timu yake.

Wachezaji wengine kama Assad Juma, Ali Msengi, Ally Ng’anzi na Yohana Mkomola bado hawajaweza kupata uzoefu wa Ligi Kuu licha ya kuwa wana vipaji vikubwa.

Tunazidi kuwaomba makocha wa timu mbalimbali kuendelea kuwatumia wachezaji hao kwani, kwa kufanya hivyo tutawasaidia kukua kisoka na kuimarika.

Pamoja na kwamba wachezaji hawa wamepelekwa kwenye timu ya vijana chini ya miaka 20 na 23, bado wanahitaji mechi za ligi ili kuweza kufikia ubora wa juu zaidi.

Ifahamike kwamba mchezaji kuwa na kipaji ni kitu kimoja, lakini kuendeleza kipaji hicho ni kitu cha pili.

Kama wachezaji hawa hawatapata nafasi katika timu za Ligi Kuu na ligi nyingine za chini, uwezo wao unaweza kuishia hapo hapo walipo sasa.