MTU WA PWANI: Naona kabisa Wapare walivyoliteka soka letu

Friday December 1 2017Abel Charles_charlesabel24@gmail.com

Abel Charles_charlesabel24@gmail.com 

By CHARLES ABEL

KUNA hisia ambayo imekuwa kwa muda mrefu nchini kwamba Wapare wanapatikana Kaskazini mwa Tanzania na ndilo kabila linaloongoza kwa ubahili kuliko mengine yote zaidi ya 300 ambayo nchi hii imebahatika kuwa nayo. Ndiyo!

Hadi sasa hakuna utafiti na ushahidi usioacha shaka juu ya hilo lakini ni dhana ambayo imekuwa ikiendelezwa vizazi na vizazi jambo linalofanya iwe ngumu kuifuta vichwani mwa watu.

Na ndio maana sio jambo la ajabu kuona mtu anaitwa Mpare hata kama sio wa kabila hilo kwa sababu tu anaonekana amekuwa bahili na hela yake haitumiki kirahisi rahisi.

Watu wenye tabia za Kipare wamejazana katika kila eneo hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu inapitia katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Wapo makanisani, misikitini, kwenye taasisi za kielimu, katika vyama vya kisiasa, ndani ya asasi za kiserikali, mitaani na hatimaye hivi sasa wameanza kuja kwa kasi kwenye soka.

Mjadala unaoendelea hivi sasa juu ya thamani ya kikosi cha Simba ni mfano tosha unaoweza kudhihirisha kwamba roho ya Kipare imeshaota mizizi kwa mashabiki na wadau wa soka nchini tofauti na kwingineko.

Simba inatajwa kutumia kiasi cha fedha zaidi ya Shilingi 1.3 bilioni katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu, fedha ambazo walisajili kundi kubwa la mastaa kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.

Sio jambo la kushangaza kwa timu kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye dirisha la usajili kwani maisha siku hizi yamebadilika na mchezo wa mpira wa miguu umekuwa ukiendeshwa kwa gharama kubwa.

Kwa muda mrefu Simba wamekuwa wakisota kwenye Ligi Kuu Tanzania Baraka kwa sababu walikuwa na kikosi cha wachezaji wenye kiwango cha kawaida ambao hawakuwa na ubavu wa kushindana na nyota wa Yanga na Azam katika mbio za ubingwa.

Simba haikuwa inapenda kusajili wachezaji wa namna hiyo bali misuli yao ya kiuchumi ilikuwa dhaifu kiasi cha kutokuwa na uwezo wa kushinda vita ya kusajili mchezaji mbele ya Azam na Yanga.

Bahati mbaya kwa Simba ni nguvu yao ya kiuchumi kuja katika kipindi ambacho roho na tabia za Kipare zimeshika hatamu kwenye soka hivyo chochote ambacho kinawatokea uwanjani, watu wanakitazama kwa mtazamo wa fedha badala ya hali hali ya mchezo wa soka.

Wapare wa soka letu, hawataki kuona Simba ikifungwa, kutoka sare wala kuzidiwa kiwango cha umiliki mpira pindi wanapocheza mechi yoyote ile na badala yake wanataka kuona ikipata matokeo mazuri uwanjani pindi inapocheza mechi yoyote ile.

Kuna mambo kadhaa ambayo wadau na mashabiki wa soka nchini hawayazingatii ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Kwanza fedha haichezi mpira bali ina nafasi kubwa ya kufanya mpira uchezwe na ndio maana hadi sasa, licha ya klabu za Uingereza kutumia fedha kubwa katika kujiendesha bado zinafukuza kivuli cha klabu za Hispania na Ujerumani ambako hakuna uwekezaji mkubwa wa fedha kwenye mpira wa miguu kulinganisha na Uingereza.

Timu inaweza kutumia kitita kikubwa cha usajili lakini bado ikahitaji kupata muda wa kuwaunganisha pamoja wachezaji waliosajiliwa ili waweze kuendana na mbinu na falsafa ya kitimu na kuachana na zile za kule kwenye timu walikotoka.

Ni kweli kwamba Simba wamefanya usajili wa gharama kubwa msimu huu lakini wachezaji waliosajiliwa, wametoka katika klabu zenye falsafa na mbinu tofauti hivyo ni lazima wapate nafasi ya kutosha ili waweze kuzoeana moja kwa moja.

Mfano wa hili tunaweza kuuona nchini Hispania ambako licha ya Real Madrid kuwa timu inayoongoza kwa kumwaga kitita kikubwa katika kipindi cha usajili, walikaa misimu minne bila kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo huku wakiwa na kikosi kilichoundwa na wachezaji nyota akiwemo mchezaji bora wa dunia mara tano, Cristiano Ronaldo.

Lakini kingine, siku zote usajili ni kama kamali ambayo kuna wakati unaweza kufanikiwa lakini pia inatokea mtu ukashindwa kufanikiwa. Sidhani kama Simba walitegemea baadhi ya mastaa waliowasajili watakuja kushindwa kuonyesha ubora wao kama inavyotokea kwa sasa na bila shaka walijiaminisha kwamba watawapa kilicho bora.

Katika hali ya kawaida hakuna klabu hapa nchini ambayo ingeweza kukataa kuwa na mchezaji Haruna Niyonzima ambaye alionyesha kiwango kizuri katika kikosi cha Yanga msimu uliopita kilichomfanya apate tuzo ya kuwa mchezaji bora wa kigeni msimu uliopita. Nani aliyetegemea Fernando Torres angekabiliana na ubutu wa kufunga katika kikosi cha Chelsea ambayo ilimsajili akiwa moto wa kuotea mbali katika upachikaji mabao ndani ya timu ya Liverpool? Kumbe tunajifunza kuwa changamoto wanayokabiliana nayo Simba kwa sasa ni jambo la kawaida kwenye soka na zipo timu ambazo zinatumia kitita kikubwa cha fedha zaidi ya Simba.