MEZA YA UFUNDI: Kombe la Dunia limebadili umuhimu wa mifumo

Muktasari:

  • Ndani ya miaka minne ni lazima kuwe na mabadiliko ya makuzi yake kuanzia tabia hadi ubunifu.

MWEZI huu ndio muda mwafaka wa kujua dunia imevuna nini baada ya miaka minne. Hii ni sawa na mwanafunzi anayesoma shule ya sekondari kwa miaka minne kisha anafanya mitihani ya kumaliza shule.

Ndani ya miaka minne ni lazima kuwe na mabadiliko ya makuzi yake kuanzia tabia hadi ubunifu.

Namna ya kulikaribia jambo jema ndio maana halisi ya fainali hizi za Kombe la Dunia ambapo nchi hutumia muda mrefu kuziandaa timu zao kuanzia kujenga vijana watakaotumika, kwa kuwapa michezo mingi ya kujipima Nguvu na kutengeneza taratibu za uchezaji wa timu yako.

Hapa ndipo tunapoona timu za nchi mbali mbali kupitia benchi lake la ufundi huwa na muda mrefu wa kuandaa mbinu ndani ya mifumo na hasa pale timu zinapokuwa zimefuzu kushiriki fainali hizi.

Muda mwingi baada ya ratiba kutokewa makocha huandaa mipango kazi kwanza wa kukabiliana na timu walizopangwa nazo kwenye kundi moja.

Kinachoendelea sasa kule Urusi ni jinsi mifumo ya timu mbalimbali inavyotumika na kurahisisha ushindi kwa baadhi ya timu.

Wote tunajua jinsi mpangilio wa wachezaji ndani ya uwanja unavyoweza kuonyeshwa wazi na mfumo husika. Na hii hujidhihirisha mwanzoni mwa mchezo kutegemeana na aina ya wachezaji timu iliyonayo. Kumekuwa na mabadiliko mara nyingi ndani ya uwanja kutegemeana pia na aina ya timu unayokutana nayo.

Aina ya wachezaji timu pinzani inaovyowatumia na zaidi kama ndani ya timu hiyo pinzani kuna wachezaji wenye uwezo wa kuamua matokeo!

Lakini hivi sasa mpira umebadilika sana na hii inadhihirika kuwa sayansi ya soka inafanya kazi yake. Soka la mifumo limebadilika na sasa kinachofuatwa na kutekelezwa ni majukumu ndani ya mifumo, mbinu ndani ya uwanja kutegemeana na mpinzani wako ndio kila kitu.

Timu zimekuwa makini sana kupanga mipango yao kutokana na timu wanazokutana nazo.

Huwezi kuuona mchezo wa wazi sana kwa timu zote, pale timu moja inapocheza mchezo wa wazi timu ya pili itacheza kwa mbinu zaidi. Huwezi kukuta timu zote mbili zikicheza soka la wazi na linalofanana ndio maana tunaona uhaba mkubwa wa mabao na hata inapotokea timu kupata bao, mara moja hubadilika na kucheza soka la mbinu zaidi ili kujilinda.

Michezo iliyozihusisha timu za Argentina dhidi ya Iceland ai Hipsnia dhidi ya Ureno ni mfano mzuri. Ni uthibitisho wa kile tunachokiona. Wakati Hispania ilifunguka na kucheza soka la wazi, Ureno ilicheza soka la mbinu zaidi huku ikijilinda kwenye eneo lao na kisha kufanya mashambulizi machache yenye tija. Mbinu sahihi dhidi ya mpinzani zimebadili kwa kiasi ile dhana ya mifumo kuchezwa bila mabadiliko.

Mchezo wa pili uliowahusu Argentina dhidi ya Iceland pamoja na Iceland kucheza kwa kuzuia zaidi lakini bado uwezo wao wa kukamilisha majukumu yao ndani ya uwanja kwa asilimia kubwa ulifanikiwa. Iceland ilizuia kwa uwingi huku ikiziba mianya ya kupitwa na wachezaji wa Argentina wenye uwezo wa kuamua matokeo wakiongozwa na Lionel Messi

Wenzetu pamoja na uwezo mkubwa wa wachezaji wao, bado utekelezaji wa majukumu yao ndani ya uwanja ni mkubwa na unaonekana kufanikiwa zaidi.

Kwa maana kwamba wachezaji wao wameiva kiasi cha kuwa uelewa mkubwa kwa kuwa kile kinachoonekana kuwa kimeongelewa ndani ya viwanja vya mazoezi vinaonekana kufanya kwa usahihi na wachezaji hao. Imekuwa hivyo si kwa timu zinazoonekana kuwa ndogo kwenye fainali hizo, bali hata zile kubwa nazo zimeingia kwenye kucheza kwa mbinu zaidi pale zinapokutana na timu zinazomiliki mchezo.

Tuliona Brazil ilipocheza dhidi ya Uswisi ambapo ilicheza kimbinu zaidi na kutoka kwenye soka la wazi ikiogopa kufungwa kirahisi. Tumeiona Ufaransa ikijilinda sana mbele ya nchi ndogo kama Peru baada ya kuongoza kwa bao moja. Si hao tu hata Hispania inayocheza soka la wazi ilibidi kubadili mbinu kujilinda kiasi dhidi ya Iran kisha inakaa na mipira na kushambulia kwa kasi.

Ni majukumu na mbinu kwa sasa ndizo zinazoonekana zaidi kuunadhifisha mfumo na hasa dhidi ya timu unayokwenda kucheza nayo!

Kwa sasa hakuna mifumo ndani ya timu inaonekana kubadilika kila kukicha na kutegemeana na timu unazokutana nazo. Huu si wakati wa kutangaza kuwa kocha huyu anahusudu mfumo mmoja siku zote.

Badala yake timu zimekuwa zikibadilika kila mara. Hii inahitaji sana akili nyingi za wachezaji wenyewe ili kufikia malengo makubwa.

Kwa kifupi hili ni funzo kwetu kwa nchi na wachezaji kwa jumla kuweza kuwa na mipango na kujua kile tunachokitengeneza mazoezini na kukifanyia kazi kwenye mechi.