MAONI YA MHARIRI: Umefika wakati wasemaji wa klabu kujiongeza

Friday August 4 2017

 

By MWANASPOTI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) lilipitisha Azimio maarufu lililofahamika kama Azimio la Bagamoyo mwaka 2007, ambalo lilibadilisha mfumo wa utendaji wa viongozi wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azimio hilo ndilo lililowaibua maofisa habari, ambao kwa miaka ya nyuma nafasi hizo zilishikiliwa na Makatibu Wenezi, waliokuwa mafundi wa kupiga propaganda kwa manufaa ya klabu zao.

Makatibu wenezi hao walikuwa wakipatikana kupitia chaguzi za klabu husika na hata vyama vya soka, waliokuwa wakitumikia nafasi hizo kwa kujitolea zaidi na hawakuthaminika sana kama ilivyo kwa maofisa habari wa sasa.

Azimio la Bagamoyo lilitaka maofisa habari waajiriwe wakiwa na sifa za kitaaluma tofauti na ilivyokuwa kwa makatibu wenezi, ambao wengi wao walikuwa ni watu wa kawaida ilimradi ni wanachama wa klabu walioshinda kupitia chaguzi za klabu.

Kwa mnasaba huo ni kwamba maafisa habari wa klabu ni watu muhimu wakiwa ni waajiriwa wanaolipwa mishahara kama miongoni mwa watendaji wa klabu, hivyo kila wanalofanya huwa linaakisi hadhi na heshima ya klabu wanazotumikia.

Hata kama aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage aliwahi kudai   wasemaji wa klabu ni kama makarani tu, lakini ukweli watu hao wanaajiriwa wakiwa na taaluma zao katika sekta ya habari na mawasiliano ya umma na hivyo wanajua kipi cha kufanya kulinda hadhi za klabu zao.

Kwa bahati mbaya katika miaka ya karibuni, imeshuhudiwa wasemaji wa klabu ama maofisa habari wakigeuka kuwa kama mashabiki tu wa mitaani kwa kauli zao na hata tambo wanazozitoa kupitia vyombo vya habari hasa redio na televisheni.

Baadhi yao wanashindwa kulinda hadhi za klabu zao na hata heshima ya taaluma zao kwa kuzungumza ilimradi wamejisikia kuzungumza, wakati mwingine mambo yaliyo nje ya mchezo wa soka.

Mwanaspoti halina tatizo na wasemaji hao, pengine ndivyo majukumu yao ya kazi walivyopangiwa kufanya kazi za propaganda kuliko utaalamu, lakini kwa yakini mambo hayo yanawavunjia heshima na kuchafua hadhi ya klabu wanazotumikia.

Inawezekana wakati mwingine unazi wa klabu zao unawasukumua kuwa kama mashabiki, lakini wajibu wao kukumbuka kuwa wao ni waajiriwa na maofisa wenye kuaminiwa na klabu, hivyo hata wanachokizungumza kinafuatiliwa kwa karibu.

Wapo maofisa wachache wenye kujitambua na wanaojua kuzitumia vyema nafasi zao kwa manufaa ya klabu, hawa wanapaswa kuigwa na wenyewe kuendelea kushikilia pale pale waliposhikilia kwa sababu ndivyo wanavyotakiwa wawe.

Kwa wale ambao wanajisahau na kufanya mambo yao kama wahuni wa mitaani wabadilike kwa sababu wanazitia aibu klabu zao na kujiharibia hata wao wenyewe kuweza kupata ajira sehemu nyingine inapotokea wanaondoka katika klabu zao.

Kuwa ofisa habari sio kigezo cha mtu kuwa kama Ma-MC (Msema Chochote) hata kama wanachokisema kinawavutia mashabiki wa klabu yake, ukweli kuna wanaowafuatilia na kuwapima uwezo wao wa kusimamia eneo hilo la habari.

Maofisa habari wanaweza kuwa daraja la kuitengenezea klabu mafanikio sio ya uwanjani tu, bali hata katika suala zima la kiuchumi kwa kutumia nafasi yake kuitangaza klabu na kuvutia wawekezaji wanaoweza kujitosa kumwaga fedha.

Hivyo kwa namna soka la sasa lilivyo na linavyohitaji fedha kuliko kitu kikingine chochote ili klabu zikiendeshe, ndio maana tunawakumbusha maofisa habari ama wasemaji kujiongeza kwa kuachana na utendaji kazi kama watu wa mitaani.

Siyo kila wanachoulizwa wanaweza kukitolea ufafanuzi, ama sio kila jambo wanaopaswa kulisemea hewani, kuna mengine wanaweza kukwepa kitaalamu kama ambavyo baadhi ya maofisa habari hao wa klabu wamekuwa wakifanya.

Suala la kitaaluma kuhusu timu ni lazima waachie makocha walizungumzie, suala la afya za wachezaji wayaseme kulingana na madaktari wao walivyowapa taarifa na suala nyeti lililo nje ya uwezo wao, wawaachie mabosi wao wayaseme.

Kuendelea kuzungumza kila jambo kishabiki sio tu inawashushia hadhi zao, pia zinatoa picha mbaya kwa wasemaji hao, hata kama sio wote wenye kuyumba katika utekelezaji wa kazi zao kama maofisa habari, ndiyo maana tunawazindua tu.

Mambo ya ushabiki na uhuni mwingine waachiwe mashabiki, lakini kwa maofisa habari ni lazima walinde hadhi na heshima ya taaluma hiyo kwa namna yoyote kuanzia kuzungumza na hata mengine wayafanyayo nje na ndani ya klabu zao.