MAONI YA MHARIRI: Mkutano wa CCM, TFF ulete tija kwa soka la Tanzania

Uwanja wa CCM- Kirumba

Muktasari:

  • Kwa kifupi, bila viwanja hivyo vya CCM, soka la Tanzania ni vigumu kuchezwa kwa ufanisi

UONGOZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wamiliki wa viwanja vinavyotumiwa kwa mechi mbalimbali za Ligi nchini, Chama cha Mapinduzi (CCM) wanatarajia kukutana wiki ijayo kujadiliana mambo mbalimbali.

Mkutano huo umepangwa kufanyika Oktoba 20, ikielezwa umeombwa na CCM wakitaka kukutana na TFF kwa nia ya kujadiliana namna kuboresha viwanja hivyo na miundo mbinu yake.

Hakuna ubishi kuwa, asilimia kubwa ya viwanja vya soka nchini vinamilikiwa na chama hicho tawala na TFF pamoja na klabu za soka zikiwamo wakongwe Simba na Yanga zimekuwa zikivitegemea kwa kiasi kikubwa viwanja hivyo.

Miongoni mwa viwanja vinavyotumiwa kwa ligi mbalimbali na vinamilikiwa na CCM ni; CCM Kirumba-Mwanza, Kambarage-Shinyanga, Majimaji-Songea, Sheikh Amri Abeid-Arusha, Ali Hassan Mwinyi-Tabora, Sokoine-Mbeya, Namfua-Singida, Jamhuri-Dodoma, Mkwakwani-Tanga na Jamhuri- Morogoro.

Kwa kifupi, bila viwanja hivyo vya CCM, soka la Tanzania ni vigumu kuchezwa kwa ufanisi na ndiyo maana leo inashuhudiwa timu za Mkoa wa Arusha zikihaha kusaka viwanja vya kuchezea mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL) kutokana na Sheikh Amri Abeid kufungwa kwa ajili ya ukarabati.

Hata kama viwanja vingi kati ya hivyo vinavyotumiwa kwa ligi na vilivyopo chini ya CCM ni vibovu na chakavu kiasi cha kuondoa msisimko wa soka letu, bado vimekuwa msaada mkubwa kwa TFF na klabu husika.

Ndiyo maana kama wadau wa soka tumefurahia kusikia CCM imeomba kukutana na TFF ili kujadiliana kwa kina namna ya kuviboresha viwanja hivyo sambamba na miundo mbinu yake.

Hii ni fursa nzuri ya TFF kukifikisha kilio cha muda mrefu cha mashabiki wa soka juu ya kutaka kuona viwanja vya soka vinaboreshwa na kuwa rafiki kwao kuhudhuria kwa wingi kushuhudia mechi mbalimbali za ligi.

Kwa mfano Sheikh Amri Abeid umefungwa kwa muda ili ukarabatiwe  kutokana na kuharibika eneo la kuchezea na viwanja vya michezo mingine, miundo mbinu ya vyoo na hata majukwaa kuwa hatarishi kwa mashabiki wanaokwenda uwanjani.

Hivyo mkutano huo wa Oktoba 20 unapaswa kusaidia kuleta tija na suluhisho la matatizo ya viwanja vinavyolalamikiwa kwa pande hizo mbili kujadiliana kwa kina na kutafuta namna ya kuvifanya viwanja vya soka kuwa sehemu ya rasilimali ya kuzalisha mapato, pia rafiki kwa watumiaji wake na timu shiriki.

Mwanaspoti limefurahishwa na maamuzi ya CCM kuutafuta uongozi wa TFF na kutaka kukaa nao chini kuweza kujadiliana kwa kina jinsi ya kuviboresha viwanja hivyo na hii itasaidia wamiliki kujua kipi kinachotakiwa na mashabiki wa soka. Inawezekana kelele za viwanja ni vichakavu na visivyofaa kutumiwa na wachezaji wa soka, CCM haijui na wala haijawahi kuambiwa kwa ufasaha na labda hawajui athari zinazotokana na viwanja kuwa na mwingiliano na matumizi mengine ya viwanja vyao na kuathiri ratiba za michezo mbalimbali ya ligi.

Tunaamini hata CCM wana dukuduku lao dhidi ya TFF katika matumizi ya viwanja na namna ya kuangalia jinsi wanavyoweza kunufaika navyo katika suala zima la mapato. Kwani hivi karibuni uongozi wa CCM Arusha ulikaririwa wakati ukifafanua kwa nini wameufunga uwanja wao, ukidai kuwa mgao mdogo wanaopata kupitia mechi za soka ni sababu ya kuutoa  uwanja wao kwa matumizi mengine.

Aidha ulidai kuwa, TFF na wasimamizi wa soka wamekuwa wakikurupuka kutaka kupewa uwanja ghafla ilihali walikuwa na uwezo wa kuwahisha kuuomba mapema na kuwapa nafasi wamiliki hao kupanga matumizi yake kwa faida.

Inawezekana kupata mgao mdogo wa mapato unachangiwa na mahudhurio duni ya mashabiki wa soka, pengine kwa hali mbaya ya viwanja, kukosekana kwa matangazo na mambo mengine, hivyo mkutano huo ni kuambiana kweli.

Kuambiana huko na kutafuta njia ya kuleta neema itakayosaidia kila upande kunufaika na matumizi ya viwanja hivyo ni vikao na mikutano kama hiyo ndiyo maana tunasisitiza mkutano huo wa Oktoba 20 ulete tija na maendeleo ya kweli.