MAONI: Klabu ziache visingizio zicheze soka ligi bado

Tuesday September 12 2017

LIGI Kuu Bara msimu wa 2017-2018 ndio kwanza imemaliza mechi za raundi ya pili, ikishuhudiwa klabu ya Mtibwa Sugar wakiipokea Simba uongozi wa ligi hiyo.

Simba ilikuwa ikiongoza msimamo kabla ya mechi za juzi kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga kabla ya Mtibwa kukwea kileleni kutokana na kuwa timu

pekee iliyoweza kushinda mechi zake zote mbili na kufikisha pointi sita.

Alama mbili zaidi na ilizonazo Simba na klabu nyingine nne zilizokusanya kila mja pointi nne na kutofautiana mabao ya kufunga na kufungwa tu, huku Stand United ikiwapokea Ruvu Shooting mzigo wa kuburuza mkia katika msimamo huo.

Hata hivyo wakati ligi hiyo ikianza kuchanganya kwa wikiendi hii kushuhudiwa mechi za raundi ya tatu, tayari baadhi ya viongozi na makocha wa klabu shiriki wameanza kusikika kuwatupia lawama waamuzi wa mechi zao.

Wenyewe wanaamini wamekuwa wakipata matokeo mabaya katika mechi zao kwa sababu ya maamuzi mabaya ya waamuzi.

Mwanaspoti linaamini ni mapema mno kwa klabu kuanza kuwatupia lawama waamuzi kwa sababu mpaka sasa katika mechi 16 zilizochezwa hakuna tatizo

lolote lililoonyeshwa na waamuzi kiasi cha kuanza kunyooshewa vidole.

Tungependa kuwaona makocha, viongozi na hata wachezaji kutafakari na kufanya tathmini katika mechi walizocheza kuona wapi walikosea badala ya kutafuta mchawi.

Ni lazima klabu ziige mfano wa Ruvu Shooting ambayo baada ya kufumuliwa mabao 7-0 na Simba katika mechi ya ufunguzi, walijitathmini na kuangalia wapi walipojikwaa na kujipanda kabla ya kwenda kupata pointi moja mjini Bukoba.

Hata ukimsikiliza Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ mara baada ya mchezo wao na Simba akikiri kuwa walifungwa kwa sababu kikosi chao

kilikuwa dhaifu kwa kukosekana kwa nyota wake wa kikosi cha kwanza wapatao sita na kwamba Simba ni timu kubwa na yenye wachezaji wazoefu.

Na juzi walienda Kagera na kuwashtukliza wenyeji wao Kagera Sugar kwa kutangulia kupata bao lililodumu kwa muda mrefu kabla ya kusawazishwa dakika

za jioni na timu hiyo kugawana pointi moja moja.

Hivi ndivyo klabu nyingine zinapaswa kuwa, zicheze soka na kujitathmini kwa kila mchezo wanaocheza ili kujua mapungufu yao na kuyarekebisha badala ya kila mara kusaka kichaka cha kujificha udhaifu wao.

Hatukatai waamuzi ni binadamu na wakati mwingine hukosea katika maamuzi yao kama binadamu, lakini klabu hususani watu wa benchi la ufundi kujitathmini juu ya vikosi vyao na namna vijana wao wanavyowajibika uwanjani.

Kwa mfano ingeshangaza sana kuwasikia makocha wa Simba wakiwalalamikia waamuzi wa mechi yao na Azam, wakati wachezaji wao walitengeneza zaidi ya

nafasi 10, lakini hakuna hata moja waliyoitumia kujipatia mabao.

Hata hivyo Kocha Msaidizi wa klabu hiyo, Jackson Mayanya alisikika akikiri udhaifu wa vijana wake katika umakini wa kutumia nafasi na kuwasifia pia

wapinzani wao Azam kuwa walikuwa imara eneo la ulinzi na kuwanyima mabao.

Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa watu wa ufundi, kuzungumzia udhaifu na uimara wa timu zao na wapinzani wao, badala kuishia kuwalalamikia waamuzi wakati mwingine bila sababu kutokana na ukweli soka ni mchezo wa hadharani.

Kama waamuzi wanavurunda ni rahisi kuonekana kwa vile watu wapo uwanjani na wengine wanaziangalia mechi za Ligi Kuu kupitia kwenye runinga kadhalika kama timu zimechemsha ni rahisi kubainika na hakuna mahali pa kujificha.

Tunaamini kama viongozi wa klabu wakiwamo Makocha watajikita katika eneo hilo itasaidia kuimarisha vikosi vyao na kuwafanya wachezaji kuwajibika ipasavyo uwanjani na kuondokana na mawazo kuwa timu zao zinaonewa na waamuzi.

Wachezaji wanaposikia malalamiko ya kila mara ya makocha na viongozi wao na hata wanachama na mashabiki, inawaathiri kisaikolojia na kuamini wanashindwa kupata matokeo mazuri kwa vile tu wanaonewa na waamuzi.

Hivyo hata inapotokea ndani ya uwanja waamuzi wakatoa maamuzi sahihi watayapinga na kuyalalamikia tu kwa kuamini kuwa, waamuzi wanawaonea na

mwishowe kuvuruga mchezo mzima na hata kuziathiri zaidi timu zao.

Kadhalika ligi bado mbichi, klabu zinapaswa kujipanga ili kuhakikisha zinapata matokeo mazuri kwa sababu mtu hujifunza kwa makosa, mbele kuna mechi zaidi ya 25, hivyo bado kuna fursa ya timu zilizoanza vibaya kurekebisha makosa.

Iwapo kila klabu itakuwa ikijitathmini na kujipanga upya, huku wachezaji wakaonyeshana ujuzi kusaka matokeo mazuri zaidi ni wazi Ligi itakuwa tamu na yenye ushindani zaidi, pia itawarahisisha kazi waamuzi uwanjani.