MAONI: Simba, Yanga kazi ni moja tu, kuvuna ushindi nyumbani

Muktasari:

Timu hizo zitakuwa nyumbani katika kampeni yake ya pili ya kusaka nafasi ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

ILE safari ya matumaini ya Simba na Yanga kwenye mechi za kimataifa, inaendelea leo Jumanne na kesho Jumatano.

Timu hizo zitakuwa nyumbani katika kampeni yake ya pili ya kusaka nafasi ya kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa itakuwa wenyeji wa Township Rollers ya Botswana leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo kali na ya kusisimua inatarajiwa kutoa mwanga kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kama wanaweza kufuzu hatua ya makundi ya Ligi hiyo ya Mabingwa.

Yanga ilifuzu raundi ya kwanza baada ya kuiondosha St Louis ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 2-1 huku Rollers ikifuzu katika raundi hiyo baada ya kuifunga Al Merreikh ya Sudan mabao 5-2.

Kitendo cha Rollers kuwatoa Merreikh kinatosha kuonyesha ni timu ya aina gani kwani kuwatoa Waarabu hao wa Sudani si jambo jepesi.

Ni dhahiri kuwa Yanga inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Wabotswana hao ambao wanaongoza Ligi Kuu nchini mwao.

Hata hivyo, rekodi za mechi saba za mwisho za Yanga zinaonyesha kuwa inaweza kufanya vizuri hapa nyumbani na pia ugenini.

Yanga haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake saba za mwisho ikiwa imeshinda mara sita na kupata sare moja.

Rekodi hiyo inaonyesha pia Yanga ipo kwenye njia sahihi kuelekea kwenye mchezo huo.

Tunawahimiza wachezaji wa Yanga kujituma zaidi katika mchezo wa nyumbani ili kuweka hesabu zao vizuri na kujiweka katika nafasi ya kusonga mbele.

Mechi za nyumbani zina nafasi kubwa ya kuamua kama timu inasonga mbele ama la, japokuwa siku hizi soka limebadilika na timu inaweza kushinda popote.

Yanga haipaswi kurudia makosa ya kupata ushindi mwembamba katika mechi ya kwanza kama ilivyofanya kwa St. Louis kwa kushinda bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza, hivyo kuweka nafasi yao ya kusonga mbele shakani.

Mwaka jana pia Yanga ilipoteza nafasi ya kufika hatua ya makundi baada ya kupata sare na Zanaco katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kisha suluhu kule Zambia ambayo iliwaondoa mashindanoni.

Benchi la ufundi la Yanga linapaswa kuingia kwenye mchezo huo na mbinu sahihi wakifahamu kuwa wapinzani wao watacheza kwa kujilinda zaidi kwani wanafahamu kuwa mchezo wa marudiano watakuwa nyumbani na wanaweza kushinda.

Kwa upande wa Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, itakuwa wenyeji wa Al Masry ya Misri kesho Jumatano hapo hapo kwenye Uwanja wa Taifa.

Ni mchezo mgumu pia kwani timu nyingi kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini zimekuwa na ushindani mkubwa, hivyo huwezi kutarajia mchezo mwepesi kutoka kwao.

Masry mbali na kwamba wanashikilia nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Misri, ni timu yenye ushindani mkubwa.

Timu hiyo inaundwa na wachezaji mahiri kama Ahmed Gomaa, Islam Slieman, Aristide Bance na wengineo ambao wanatarajiwa kuipa changamoto kubwa Simba.

Hata hivyo Simba haipaswi kulaza damu kwani mechi ya nyumbani ni fursa kubwa kwao kupata ushindi mnono ambao unaweza kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Simba imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za ukanda huo, ambapo miaka ya karibuni iliwahi kuitoa ES Setif ya Algeria huku pia ikiwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za Zamalek na Ismailia za Misri pia.

Tunawahimiza pia wachezaji wa Simba kuingia kwenye mchezo huo kwa nguvu kubwa ili waweze kupata ushindi ambao utawaweka pazuri.

Benchi la ufundi la Simba pia linahitaji kuwa na mbinu sahihi kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.

Lakini kingine tunachowaambia Simba na Yanga, wachezaji wacheze kwa tahadhari kuepuka kadi zisizokuwa na mpango.

Kama mwamuzi kakera, ni suala la nahodha kwenda kusimama.

Mambo mengine ya nje ya uwanja ifahamike kuwa kuna kamishna wa mchezo, huyu hafanyi makosa, anachukua kila kitu, hivyo ni lazima kucheza kwa tahadhari kubwa.

Zaidi ya yote wachezaji kujituma, kupambana na hali zao kuhakikisha wanashinda michezo hiyo muhimu.