MAONI: Kichuya afanye maamuzi ya kuinufaisha Taifa Stars

Muktasari:

Kichuya amekuwa mchezaji muhimu ndani ya Simba tangu alipojiunga nayo Juni mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar, kwa mkataba wa miaka miwili.

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya tayari ameweka msimamo wa kutosaini mkataba mpya na klabu hiyo mpaka ule wa sasa utakapofikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.

Kichuya amekuwa mchezaji muhimu ndani ya Simba tangu alipojiunga nayo Juni mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar, kwa mkataba wa miaka miwili.

Kutokana na kuwa na kiwango cha kuvutia, Simba imeonyesha nia ya kumsainisha mkataba mpya lakini msimamizi wake, Professa Kikumbo amemshauri asisaini kwanza kwani wana ofa kubwa kutoka maeneo mengine.

Kuna taarifa kuwa moja ya timu nchini Misri, imeonyesha nia ya kumsajili Kichuya lakini Simba haipo tayari kumuuza kwa sasa, jambo ambalo limemfanya nyota huyo kugomea mkataba mpya ili kuona kama ataweza kutimkia nchini humo mwishoni mwa msimu kama mchezaji huru.

Ni kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukiwashauri wachezaji nchini kutafuta fursa ya kwenda kucheza nje, ili kuongeza ushindani katika timu ya Taifa ambayo kwa sasa bado inajikongoja.

Kwa wakati huu ambapo tayari wachezaji wameanza kuhamasika kwenda nje, ni vyema Kichuya naye akafanya uamuzi utakaolinufaisha taifa kwa kwenda kucheza kwenye ligi hizo kubwa zaidi.

Mwaka huu tumeona wachezaji kama Saimon Msuva na Abdi Banda wakifanya uamuzi mgumu na kwenda kujiunga na timu za nje ambazo bila shaka zimeanza kuonyesha matunda kwani kila wanaporudi wanaonekana kubadilika zaidi.

Hili limeisaidia Taifa Stars sasa kuwa na wachezaji wengi wanaocheza katika ligi nyingine, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo timu hiyo iliundwa na nyota karibu wote kutoka Ligi Ku Bara.

Banda kwa sasa anacheza Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL). Hakuna shaka kwamba PSL ni moja ya ligi bora Afrika kwa sasa.

Ukitazama bingwa wa Afrika kwa ngazi ya klabu mwaka jana alikuwa Mamelodi Sundowns ya nchini humo huku kwa mwaka huu timu ya Supersport FC ikitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mafanikio ya timu hizo yanathibitisha kuwa PSL ni moja ya ligi kubwa barani humu.

Msuva ametimkia nchini Morocco, akiichezea klabu ya Difaa El Jadidi. Morocco kwa sasa ni kilelezo pia cha soka la Afrika, na hata mabingwa wapya wa bara wametokea nchini humo ambao ni Wydad Casablanca. Ni wazi kwamba Msuva anacheza katika moja ya ligi kubwa Afrika, hivyo kuongeza vitu vingi kiufundi ambazo zinalisaidia taifa.

Kwa wakati huu ambapo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wapo Ulaya na wachezaji wengine wengi, uamuzi wa busara unahitajika kwa Kichuya ambaye ni mmoja wa mastaa wa Simba.

Kama winga huyo atatumia kiwango chake cha sasa kwenda kucheza katika ligi hizo za nje, ni wazi kwamba Taifa litanufaika zaidi.

Ligi ya Misri inaendelea kuwa bora Afrika, huku timu kama Al Ahly, Zamalek, Ismailia na nyinginezo zikiwa na historia kubwa barani humu.

Kama Kichuya atasaini katika timu hiyo ya Misri, timu ya Taifa itaongeza idadi ya nyota ambao watakuwa wameiva vilivyo kiufundi, jambo ambalo Watanzania wengi wanatamani litokee.

Majirani zetu Kenya tayari wamepiga hatua katika kuhamasisha wachezaji wao waende kucheza nje, ambapo kwa sasa ni golikipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch pekee mwenye nafasi kikosi cha kwanza kutoka kwa wachezaji wa ligi ya ndani.

Nyota 10 wa kikosi cha kwanza cha Kenya wanatoka katika ligi kubwa za nje, jambo ambalo linawaimarisha kila siku.

Kwa Uganda pia wachezaji wao mastaa wanajitahidi kutoka kila siku, ili kutoa wigo mpana kwa timu ya Taifa. Hakuna ubishi kwamba kiwango cha Kichuya sasa kinatosha kumbeba kwenda kucheza nje, hivyo asilaze damu. Tangu amejiunga na Simba mwaka jana amekuwa ndiye mchezaji muhimu zaidi, akifunga mabao 17 Ligi Kuu na kuwa mchezaji aliyeifungia timu hiyo zaidi katika kipindi cha miezi 14 iliyopita. Amekuwa pia chachu ya mabao mengine mengi huku pia akifanya vizuri na timu ya Taifa. Tunapenda kumshauri Kichuya pamoja na Professa Kikumbo anayemsimamia kuwa wafanye uamuzi kwa ajili ya kulisaidia taifa.