Ligi Kuu imeanza tena; ni mtihani wa kutetea kombe

MAMBO yameanza kunoga tena kwa mashabiki wa soka katika sehemu mbalimbali duniani kwani ile ligi maarufu zaidi duniani, Ligi Kuu England (EPL), imeanza kutimua vumbi katika msimu wake wa 2018/19.

Hapana ubishi nafasi ya ubingwa inatolewa zaidi kwa timu sita kubwa; Manchester City ambao ni mabingwa watetezi, Manchester United, Liverpool, Chelsea, Arsenal na Tottenham Hotspur.

Hata hivyo, yanaweza kutokea maajabu kama yale ya Leicester City iliyotwaa ubingwa misimu mitatu iliyopita. Ni ligi ngumu na miongoni mwa klabu hizo sita, mbili zinaingia zikiwa na makocha wapya – Arsenal ikiwa na Unai Emery aliyechukua nafasi ya Arsene Wenger aliyeamua kung’atuka wakati Chelsea inaye Maurizio Sarri badala ya Mtaliona mwenzake, Antonio Conte aliyefukuzwa kazi.

Tangu mwaka 2009 hakuna timu iliyofanikiwa kutetea ubingwa na katika miaka ya karibuni baada ya Leicester kutwaa ubingwa, msimu uliofuata ulikuwa wa tabu nusura ishuke daraja, wakati Chelsea msimu uliomalizika ilishindwa hata kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati ilikuwa bingwa mtetezi wa EPL.

Je, msimu huu mambo yatakuwa tofauti kwa vile Pep Guardiola anacho kikosi kizito, kipana na chenye wachezaji wa kiwango cha hali ya juu?

Ikumbukwe a huyu ni kocha aliyekuwa na mafanikio pia katika Ligi Kuu za Hispania – La Liga na Ujerumani-Bundesliga.

Ni tamaa ya Guardiola kutwaa tena ubingwa huo baada ya kuuchukua kwenye msimu wake wa pili. Ameweka rekodi ya aina yake kwani ametwaa ubingwa mara tatu mfululizo Barcelona (2008-11) na Bayern Munich (2013-16). Aliiongoza Manchester City kumaliza ligi kwa tofauti ya alama 19 kileleni.

Lakini, ni timu ipi itaipa shida msimu huu? Pengine Liverpool iliyotumia kiasi kikubwa cha fedha kuimarisha kikosi chake misimu miwili iliyopita, itaweza kukabiliana nayo, ambapo Kocha Jurgen Klopp ameonekana kuimarisha kabisa kila eneo, akiwa na wachezaji mahiri kabisa.

Mwishoni mwa msimu uliopita, hata hivyo, Liverpool iliizabua vibaya sana City, idadi ya mabao sita katika mechi mbili za UCL na Guardiola alibaki akishangaa, sijui iwapo safari hii itakuwaje walau kwenye Ligi Kuu. Ni baada ya hapo Liverpool kwenda kuipiga AS Roma kisha ikafungwa na Real Madrid kwenye fainali kule jijini Kiev. Guardiola hajamsahau Klopp.

Vipi Spurs ambayo imekuwa ikikosa makombe kila msimu katika miongo ya hivi karibuni licha ya kufanya vizuri na kutisha wengine wakiwa chini ya Kocha Mauricio Pochettino? Wengine wanasema labda Arsenal na Chelsea zilizobadili makocha zinaweza kufanya vyema na kuchukua ubingwa wakati wengine wanamuangalia Jose Mourinho ikiwa anaweza kupunguza pengo lile la msimu uliopita ili Man United nayo ilishike tena kombe hilo baada ya muda mrefu.

City ilikuwa na kiwango cha juu msimu uliopita lakini pia hata kwenye maandalizi ya Ligi Kuu hii, ambapo Guardiola hatataka kuona kiwango hicho kikishuka na huenda ikacheza kwa mfumo na kiwango kilekile cha msimu uliopita ambapo ilimaliza ligi ikiwa na alama 100 na mabao 106.

Ilishinda mechi 32 kati ya 38 za ligi, ikiwa ni pamoja na 18 mfululizo na kwa hakika haikuwa ikikamatika, japokuwa ilikuja kushindwa kushika rekodi ya Arsenal ya kutopoteza mchezo ya msimu wa 2003/4 enzi za ‘The Invicibles’.

Guardiola anaonekana kuwa mshindi kwa asili na hilo halina ubishi, kwa sababu unaweza kuliona wazi kwa kujiamini kwake, kuelekeza, kuzungumza na hata anavyokabiliana na wapinzani wake – hana wasiwasi wowote, lakini hata kama ameshafunga mabao 3-0 kwa mfano, anakuwa anataka zaidi kutoka kwa wachezaji wake.

Amewajenga hivyo wachezaji wake, nao wamekubali kabisa, asiyetaka anaondoka kama alivyoondoka kipa wao namba moja ambaye Guardiola alimkuta – Joe Hart.

Alimweleza hataki akidaka mpira abutue, bali aanze kucheza yeye na kuwapa mabeki wake jirani na muvu ijengwe katika utaratibu huo, hakuweza na mara akatolewa kwa mkopo kabla ya kiangazi hiki kuuzwa.

Huu ni msimu wa tatu wa City chini ya Guardiola na hapana wasiwasi

kama ni mashine, basi imeshawekewa mafuta ya kutosha kwa ajili ya kazi. Wachezaji wameshaielewa falsafa yake na kama ni kutenganisha pumba na mchele, kazi hiyo ni kama ameikamilisha kwa kuondoa wasiofaa na kuingiza wapya wazuri.

Kwa City akikosekana mtu mmoja huwezi kusema eti wanaumia, bali akiondoka mmoja anaingia mwingine kuziba pengo.

Nani alijua asipokuwapo Sergio Aguero bado wangekuwa wakali pale mbele? Guardiola alidiriki kumweka benchi na kumjaribu Gabriel Jesus na mambo yalikuwa makali kama kawaida, kisha akamrudisha Aguero, halafu akaamua wacheze wote pale mbele.

City inaweza kuwa kali kuliko hata msimu uliopita kwa sababu tatizo lake lilikuwa beki ya kushoto, lakini sasa Benjamin Mendy aliyekuwa ameumia amesharejea akiwa timamu na tayari katisha akipanda na kushuka. Tazama maeneo mengine kwenye kikosi, ni nyota tupu wamejaa.

Hata ingeanza vibaya mechi za awali, bado sioni sababu ya kutokuwa mabingwa wa England tena msimu huu, ikizingatiwa imejiimarisha zaidi kwa kumchukua Mahrez na inaonekana kuwa na kambi yenye raha na kuelewana sana.

Bila shaka itakuwa ligi tamu itakayofurahiwa na wengi hapa England, lakini pia huko nyumbani Afrika Mashariki na kwingineko.