Labda City, Liverpool...Arsenal, Man U mmh!

BAADA ya mabadiliko makubwa kutokea kwenye benchi la ufundi pale Arsenal kwa kuondoka Kocha Arsene Wenger na kuingia Unai Emery, kulikuwa na matarajio makubwa ya mafanikio msimu huu.

Ndio, Ligi Kuu England (EPL) msimu mpya ndio kwanza umeanza, ni mapema mno kwa sasa kutabiri lolote, lakini kwa namna iliyouanza mchezo wa kwanza kwa Arsenal kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 tena nyumbani Emirates, bila shaka matokeo yanayoweza kuleta mchecheto mwingi.

Arsenal ilifungua pazia na mabingwa watetezi Manchester City, vijana wa Kocha Pep Guardiola walionyesha ubabe wao kwa Arsenal mbele ya mashabiki wa Washika Bunduki hao.

Mashabiki wa Arsenal waliamini kuwa kiu yao ya kupata furaha sasa itatimia kwa haraka sana. Lakini mambo si hivyo.

Ilikuwa huzuni kubwa kwa Kocha Emery hasa ukizingatia upya wake ulioleta matumaini kwa mashabiki wa Arsenal. Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza ya kimashindano klabuni hapo.

Emery alipata nafasi ya kuwaanzisha wachezaji wote ambao walisajiliwa msimu huu wakiwemo Matteo Guendouzi, Sokratis Papastathopoulos na Stephan Lichsteiner, lakini maji yalizidi unga na wakalala.

Matokeo hayo yanaonyesha bado Arsenali ina shida kubwa. Ikumbukwe ndani ya misimu miwili iliyopita, ilishindwa kumaliza ndani ya Nne Bora ‘Top Four’ ya ligi hiyo jambo lililowafanya wasipate nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa muda wote huo, Kocha Wenger alikuwa lawamani akitajwa kushindwa kuiunganisha timu, sasa swali linabaki vinywani mwa mashabiki na wapenzi wa soka. Je, Arsenal hii ya kocha mpya ina kikosi cha kutinga Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa maana ya kuwamo Top Four?

Binafsi sioni kama ina uwezekano huo. Kwa sababu naona kabisa zipo timu nne zenye nafasi hiyo, Arsenal si miongoni mwa hizo.

Timu ninazoziona katika uwezekano huo ni Chelsea, Manchester City, Manchester United na Liverpool.

Kwa jinsi ilivyo, kama kuna timu inataka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England basi ni lazima ihakikishe inapata angalau alama moja kutoka katika mechi za timu hizo hapo Juu.

Lakini tayari Arsenali imeshapoteza alama tatu mbele ya mmoja wao tu, Man City. Mbaya zaidi Arsemal imefungwa katika uwanja wake wa nyumbani. Inakuwa vigumu zaidi kuweza kuiweka kama mojawapo kati ya klabu zinazopigiwa upatu wa kushinda taji hilo.

Mashabiki walipiga kelele sana kushinikiza Kocha Wenger aondoke na kweli baada ya miaka 22 pale Emirates, ameamua kurusha taulo uwanjani na kusalim amri, mzee wa watu akasepa zake.

Kocha mpya ameingia, lakini maisha pale Emirates ni yaleyale. Bado magumu kwa kweli. Hivi tujiulize, kwa dalili hizi ni kweli Kocha Unai Emery ataweza kustahimili haya maisha?

Mechi ya pili ya Arsenali ni dhidi ya wababe wengine wa Ligi Kuu England, Chelsea na hii itapigwa Stamford Bridge. Naona maisha ya Arsenal yakiwa magumu sana.

Acha tungojee hiyo mechi tutazame itamalizikaje maana wakati mwingine ni bora kuupa wakati nafasi yake ili utoe majibu yasiyo na shaka.

Lakini ikumbukwe tu kuwa Chelsea imeianza ligi hii kwa kishindo baada ya kuitandika Huddersfield mabao 3-0. Kichapo hicho najua kimewatia kiwewe Arsenal.

Wakati huo huo Manchester United nayo ilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Leicester City. Ni timu nyingine ambayo haijasimama vilivyo licha ya ushindi huo.

Kulingana na mchezo ulivyokuwa, naweza kusema kikosi cha Kocha Jose Mourinho bado kina kazi nzito ya kudhirisha ubora wake. Licha ya kushinda lakini kilionyesha mchezo wa kinyonge sana.

Ligi imeanza kwa kishindo kwelikweli. Liverpool imetuma onyo kwa washindani wengine baada ya kupata ushindi wake wa mabao 4-0 dhidi ya West Ham United.

Ushindi huo ni dhihirisho kamili kuwa Liverpool ipo tayari kupigania taji hilo baada ya kulikosa kwa muda mrefu sana. Mambo sasa ndio yameanza. Vita vipo uwanjani, sasa ni mwendo wa mbio, nani atashinda?

Naiona Manchester City ikiendelea kutesa tena msimu huu. Yaani kama Manchester United inautaka ubingwa, ni lazima iimarishe kikosi chake na hakuna budi kwa sasa hadi kusubiri dirisha la Januari.

Bila kificho United haijafanya usajili mkubwa, iliwakosa wachezaji kadhaa ambao Kocha Mourinho aliwataka, jambo hili limemkera Mreno huyo na sasa itabidi apige shughuli kwelikweli kwa wachezaji alio nao.

Kwa kweli kazi ipo pale Old Trafford. Tukutane viwanjani.