Kwa Simba hii, hawa waondoke tu

Muktasari:

  • Wakati klabu hiyo ikiendelea kusajili kwa haraka haraka, kunaonekana kabisa kwamba baada ya kuingia wachezaji wapya, wapo nyota kadhaa watalazimika kuondoka kutokana kinachoonekana watakuwa na nafasi ndogo ya kucheza.

SIMBA wanaogelea pesa. Ndio, wapo katika bahari tamu, wanakata mawimbi ya raha na ndicho kinachowafanya wazidi kufanya usajili kila siku kwa nia ya kukitanua kikosi chao kiweze kutamba katika michuano ya msimu ujao; Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati klabu hiyo ikiendelea kusajili kwa haraka haraka, kunaonekana kabisa kwamba baada ya kuingia wachezaji wapya, wapo nyota kadhaa watalazimika kuondoka kutokana kinachoonekana watakuwa na nafasi ndogo ya kucheza.

Mwanaspoti limeiangalia Simba kwa namna inavyosajili kuona kwamba kuna wachezaji hawana namna, itawalazimu kuondoka tu na kwenda kutafuta sehemu watakayokuwa wanapata nafasi ya kucheza. Cheki namna ishu yenyewe ilivyokaa.

EMMANUEL MSEJA, SAID MOHAMMED ‘NDUDA’

Makipa hawa wapo katika mstari mwekundu kwa sababu katika msimu uliopita wote hawakupata nafasi ya kuanza mbele ya Aishi Manula, na sasa uongozi wa Simba umeamua kumsajili Deogratius Munishi ‘Dida’.

Ujio wa Dida kikosini humo unawamulikia taa nyekundu Mseja na Nduda kwa sababu kwa namna yoyote ile, Dida hatokubali kuanzia nje kirahisi.

Ushindani utakuwa baina ya Dida na Manula. Hapo unadhani Mseja na Nduda watakuwa na chao? Hawana namna.

JAMAL MWAMBELEKO

Wakati anasajiliwa Simba akitokea Mbao FC, alikuwa hakosi namba katika timu hiyo ya Mwanza, lakini kibao kiligeuka alipohamia kwa Wana Msimbazi na sasa amekalia kuti kavu.

Ujio wa Asante Kwasi hapo Simba ndio uliommaliza zaidi kwa sababu alikuwa kama mbadala wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini baadaye alikuwa namba tatu baada ya Tshabalala kucheza na Kwasi.

Amekuwa akitajwa mara kwa mara kuondoka katika timu hiyo na sasa Singida United inatajwa kuwa ipo katika hatua za mwishoni kumchukua kwa mkopo.

Kwa matajiri hao wa Alizeti ndio kunaweza kuwa sehemu sahihi kwake kwa sababu anahitaji kucheza zaidi na msimu ujao ndio utakuwa wa mwisho katika mkataba wake na Simba.

ALLY SHOMARI

Kila akipewa nafasi huwa anatetemeka. Kwa namna hii hawezi kuwa mbadala wa Shomari Kapombe pale Simba. Mashabiki walitegemea kumuona Ally Shomari akifanya vizuri katika mechi za Kombe la Kagame, lakini hali ikawa tofauti.

Alijikuta akipoteza nafasi mbele ya Nicholas Gyan ambaye alikuwa akicheza mshambuliaji na kurejeshwa beki, hali hiyo inaonyesha dhahiri kwamba mlango wa kutokea kwake umejifungua wenyewe na hana budi kutoka.

Simba inahitaji kufanya usajili katika nafasi ya beki wa kulia kwa sababu Kapombe mara kwa mara amekuwa akitumika kiungo mshambuliaji badala ya beki, hii ni kwa mujibu wa mfumo 3-5-2 uliotumiwa na timu hiyo msimu uliopita.

YUSUPH MLIPILI

Katika nafasi ya beki wa kati patakuwa bato la aina yake. Msimu uliopita, Mlipili, alionyesha kiwango kikubwa alipocheza katikati na Erasto Nyoni licha ya kwamba wote walikuwa wageni.

Paul Bukaba hakupata nafasi ya kutosha msimu uliopita, lakini kocha Masoud Djuma, amempa nafasi katika Kombe la Kagame, akaonyesha ukomavu wa hali ya juu katika nafasi hiyo, jambo linaloanza kumpa Mlipili shaka.