Kuna Cannavaro wawili, Nadir Haroub mmoja tu

KUNA Cannavaro wawili. Mmoja ana jina kubwa zaidi. Fabio Cannavaro. Mwingine ni huyu hapa aliyeagwa juzi Jumapili na Yanga Morogoro. Kama utatumia majina mawili ya mwanzo, basi kuna Nadir Haroub mmoja tu. hakuna mwingine.

Inanijia kumbukumbu ya miaka 13 nyuma. Taifa Stars iliposafiri kwenda Maputo Msumbiji mwaka 2006. Katika safu ya ulinzi siku ya pambano walicheza Victor Costa na Salum Sued ‘Kussi’.

Ilikuwa mechi ngumu kwa Stars huku taifa likiota kwenda Ghana katika Afcon 2008.

Stars ilishambuliwa mwanzo mwisho na kina Tico Tico. Mwishowe tuliambulia suluhu ya bahati. Ni Mungu tu ndio alitubeba mechi imalizike kwa suluhu. Baadaye tukarudi hotelini ambako kulikuwa na shangwe kubwa.

Nilienda chumbani kwa Cannavaro aliyekuwa analala na staa mwenzake wa Zanzibar, Abdi Kassim ‘Babi’. Nilitaka kufahamu nafasi yake katika timu. Aliniambia “Sikia bro, hawa wenzangu (Costa na Sued) wamenizidi uzoefu na uwezo, lakini mimi siku moja nitacheza tu, inshallah. Teacher kaniambia nifanye mazoezi kwa juhudi tu.”

Nilishangaa sana kusikia mchezaji wa Kitanzania anasema hivyo. Na zaidi ya yote nilishangaa kuona ana shangwe na matokeo kama ilivyo kwa wachezaji waliocheza. Wachezaji wengi wanaokaa benchi duniani huwa wanaombea wanaocheza waharibikiwe ili wao waingie katika timu.

Huyu ndiye Nadir ambaye ninamfahamu kitabia. Mmoja kati ya wachezaji waungwana ambao unaweza kukutana nao katika soka. Uungwana wake mkubwa ulianzia katika kujibadili mwenyewe pale Jangwani. Anaondoka Yanga akiwa sio mchezaji aliyeingia Yanga.

Aliingia Yanga akiwa anasifika katika kubutuabutua zaidi. Wakati huo Yanga ikiwa katika Shamba la Bibi. Baadaye alijifunza mpira wa kucheza kuanzia nyuma na kuacha kubutua. Wanaoufahamu mpira watakwambia Nadir alibadilika.

Lakini baadaye akaja kutufundisha mambo mawili. Kwanza kabisa alikuwa bingwa wa kufanya ‘tackling’. Wachezaji wetu wengi hasa wa Tanzania Bara huwa hawawezi kufanya tackling. Lakini pia Nadir alikuwa mzuri sana wa kunusa hatari ya mipira ya juu. Kila ulipokaribia kutua ni yeye ndiye aliyeruka na kuurejesha ulipotoka.

Wakati watu wakiendelea kumuelewa taratibu Nadir wakagundua ndiye mchezaji aliyekuwa kizingiti katika safu ya Yanga. Akiwepo uwanjani walikuwa hawaoni sana mchango wake, akiwa hachezi walikuwa wanaona safu ya Yanga inakuwa nyanya. Wengi walichelewa kuona umuhimu wake.

Mara nyingi nilichokuwa nawaambia watu Nadir alicheza kama beki anayelihami lango. Sio kila beki anayeweza kupewa kipaji kama cha Victor Costa. Kipaji cha kupiga chenga maridadi ndani ya boksi lake na kuuhamisha mpira kwa usalama. Nadir alipewa kipaji cha kulihami lango tu.

Wakati watu wanagundua umuhimu huo pia ndipo walipogundua kuwa ni mchezaji muungwana ndani na nje ya uwanja. Kwa mfano, Nadir hajawahi kuugeukia upande wa mashabiki wa Simba na kutukana. Nadir hajawahi kugombana na wachezaji wa timu pinzani ndani na nje ya uwanja.

Katika kambi ya Taifa Stars, Nadir alikuwa rafiki wa wachezaji wote. Wa Simba, Yanga, Mtibwa na wengineo. Ukikutana na wachezaji wa Taifa Stars waliocheza na Nadir watakwambia hili. Haikushangaza kuona kitambaa chake cha unahodha kilimfiti.

Usingeweza kumsikia nahodha aliyekuwa anaizungumzia timu pinzani vizuri zaidi ya Nadir. Wengi walipenda kumsikia wakati alipokuwa anahojiwa na Azam TV pindi mechi za Yanga zilipomalizika. Alitoa heshima kwa timu pinzani.

Nadir anaondoka huku akiwa ameacha alama halisi ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar katika soka. Hawa wachezaji wa kileo kina Feisal Salum ‘Feyi Toto’ sidhani kama wataweza kufikia mamlaka ya Mzanzibari mwenzao alipofikia katika Timu ya Taifa ya Muungano na moja ya klabu kubwa nchini bila ya upendeleo eti kwa sababu ni Mzanzibari.

Mashabiki wa soka nchini hawakumtazama Nadir kama Mzanzibari. Walimtazama zaidi kama mchezaji mahiri anayestahili kucheza timu kubwa na Timu ya Taifa. Anayestahili pia kupewa unahodha. Hawakumtazama kama Mzanzibari.

Zaidi ya kwamba alikuwa mwanadamu mzuri na mchezaji mzuri, namkumbuka Nadir kwa baadhi ya mabao yake. Kwanza ni bao la kichwa alilofunga dhidi ya Al Ahly katika Uwanja wa Taifa. Katika mipira ya kona alijijenga tabia ya kuchomoka katika kundi la wachezaji wa timu pinzani na kupiga kichwa katika mwamba wa kwanza. Mabeki wengi wanashindwa kutembea na mchezaji wa aina hiyo katika mipira ya kona.

Lakini pia nitamkumbuka kwa penalti ya Panenka aliyopiga katika pambano dhidi ya Aly Ahly kule ugenini Misri. Sijui aliwaza nini? Katika umati kama ule, mechi muhimu kama ile, unakwenda kupiga penalti ya kwanza halafu kabla unaamua kuubetua mpira taratibu kwa masikhara na kumvuka kipa Mwarabu aliyepania. Inataka moyo. Lakini inakuonyesha uwezo wa kujiamini uliokithiri baada ya kuingia Yanga akiwa mchezaji anayebutua mpaka siku ile anapiga Panenka katika Uwanja wa Taifa wa Misri.

Kuna Cannavaro wawili. Lakini kuna Nadir Haroub mmoja tu. akapumzike vema na kazi yake mpya ya umeneja Yanga. Nyakati nguma hazipiti, lakini watu wagumu hupita.