Kumenoga cheki maustadhi hawa wametua rasmi kutikisa Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Wakati sasa, dunia ya wapenda soka duniani kote wakisubiri kushuhudia fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia kuanzia Alhamisi ijayo, jambo zuri ni kwamba fainali hizo zitawakuta mastaa wengi wa Kiislamu wakiwa wamemaliza mfungo, ukiiwaacha wale wa Saudi Arabia watakaocheza na Russia kwenye mechi ya ufunguzi, Juni 14, kwa sababu hiyo itakuwa Ramadhan 29.

MOSCOW, RUSSIA. LEO ni Ramadhan 24. Waislamu duniani kote kwa sasa wapo kwenye idara kutelekeza moja ya Nguzo Tano za Uislamu, Saumu ya Radhamani kwa maana ya kuwa kwenye mfungo.

Wakati sasa, dunia ya wapenda soka duniani kote wakisubiri kushuhudia fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia kuanzia Alhamisi ijayo, jambo zuri ni kwamba fainali hizo zitawakuta mastaa wengi wa Kiislamu wakiwa wamemaliza mfungo, ukiiwaacha wale wa Saudi Arabia watakaocheza na Russia kwenye mechi ya ufunguzi, Juni 14, kwa sababu hiyo itakuwa Ramadhan 29.

Taifa jingine lenye wanasoka wengi waumini wa dini ya Kiislamu, Misri yenye itacheza mechi Juni 15, dhidi ya Uruguay, siku ambayo inaweza kuwa ni Sikukuu ya Eid el Fitr, kama mfungo hautakuwa na 30 kamili.

Soka ni mchezo mmoja unaojumuisha watu wa jamii tofauti dunia, mataifa na dini zilizotofauti.

Wakati fainali hizo za Kombe la Dunia zikitarajia kufika, kuna mastaa matata wa soka waumini wa Kiislamu ambao wanatarajia kwenda kuwa gumzo katika fainali hizo za Russia mwaka huu.

Hawa ndiyo Waislamu wanaotajwa kwamba watakwenda kuitikisa Russia katika fainali hizo za Kombe la Dunia hasa ukizingatia watakuwa wametoka kwenye ibada kubwa ya Mfungo wa Ramadhan, ukiwaweka kando Ilkay Gundogan wa Ujerumani na Benjamin Mendy wa Ufaransa.

Marouane Fellaini - Ubelgiji

Kiungo mwili nyumba wa Manchester United, Marouane Fellaini ni Muislamu. Jina lake linatamkwa ‘Marwaan’ na atakuwapo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia akiwa kwenye kikosi cha Ubelgiji. Ana pacha wake anaitwa Mansour na wote ni Waislamu.

Fellaini alizaliwa na wazazi wa Kiislamu wenye asili ya Morocco na walihamia Brussels, Ubelgiji na kumfanya staa huyo sasa kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo ya Ulaya badala ya Morocco inayopatikana katika Bara la Afrika.

Sadio Mane - Senegal

Supastaa wa Senegal, Sadio Mane ni mmoja wa wachezaji makini sana wanaotamba kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Liverpool na kitu kizuri ni kwamba atakuwapo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia.

Mane ni mwanasoka muumini wa dini ya Kiislamu, ambaye anatazamiwa kwenda kuwa gumzo kwenye fainali hizo za Russia kwa maana ya kupewa nafasi kubwa ya kwenda kuwa mkombozi wa kikosi chake cha Simba wa Teranga katika fainali hizo za kusaka ubabe wa dunia.

Mesut Ozil - Ujerumani

Ujerumani kwa sasa kijasho kinawatoka kuhusu kiungo wao huyo matata kuwa majeruhi katika kipindi hiki ambacho fainali hizo za Kombe la Dunia zimebakiza wiki tu kuanza.

Hakuna ubishi, Ozil ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Ujerumani hasa katika kampeni zao za kutaka kutetea ubingwa wa michuano hiyo ya Russia. Ozil ni muislamu asiyejificha, amekuwa akisoma kuran kabla ya mechi.

Imani yake imemfanya Ozil hata asionekane kuwa mcheza rafu ndani ya uwanja, lakini kubwa ni zile pasi zake ambazo mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kwenye kuzishuhudia huko Russia.

Paul Pogba - Ufaransa

Mmoja wa wanasoka wenye thamani kubwa duniani kwa sasa. Paul Pogba anauzika. Manchester United iliponasa huduma yake kutoka Juventus walilipia Pauni 89 milioni na kumfanya kuwa mchezaji ghali kwenye Ligi Kuu England.

Pogba ni muislamu na amekuwa muumini mzuri wa dini hiyo tangu alipozaliwa.

Akitarajia kwenda kuitumikia Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, Pogba anatazamwa kwamba ni mmoja wa wachezaji watakaokwenda kutikisa kwenye michuano hiyo na hivyo kujitengenezea nafasi nzuri ya kuwapo kwenye wale wachezaji ambao wanafikiriwa watashindana kwenye kuisaka tuzo ya Ballon d’Or siku moja.

Mohamed Salah - Misri

Mo Salah ndilo jina linalotamba kwenye soka kwa sasa. Hakuna cha Cristiano Ronaldo wala Lionel Messi, Mo Salah kwa sasa pengine ndilo jina linalokamatia mchezo wa soka kutokana na huduma yake matata aliyotoa huko Liverpool msimu huu.

Kiwango cha Mo Salah kimekuja wakati mzuri wa fainali za Kombe la Dunia ambapo staa huyo muumini wa Kiislamu, amekuwa kipenzi cha wengi kutokana na utulivu wake ndani ya uwanja hata anapofunga mabao hana mbwembwe za kushangilia kama kimefanyika kitu cha maajabu.

Salah ni mchezaji mwingine ambaye amekuwa akisoma kuran na kuomba dua kabla ya mechi na wakati mwingine amekuwa akisujudu anapofunga mabao. Anasubiriwa kwenda kuziteka fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

N’Golo Kante - Ufaransa

Hakuna ubishi, Kante ni mmoja wa wachezaji bora kabisa kwenye Ligi Kuu England. Kiungo huyo anayefahamu vyema kuitenda kazi yake ya kukaba ndani ya uwanja ni muumini wa Kiislamu na mwaka jana tu hapo mwezi wa Ramadhan alikwenda zake Madina.

Kante atakuwa na Ufaransa kwenye fainali hizo za Russia, lakini mwenyewe ni Muislamu na wazazi wake walihamia Ufaransa wakitokea Mali mwaka 1980.

Kutokana na imani yake kumkolea vyema kabisa, Kante amekuwa mkimya sana ndani ya uwanja si mtu wa kuzungumza sana na hata huwa hapendi vita vya thamani sana kwani hata gari lake analoendeesha ni la kawaida sana tofauti na kiwango chake cha pesa anachovuna kila wiki huko Chelsea.

Essam El-Hadary - Misri

Staa mwingine wa Misri kwenye orodha hii. Kitu kinachosubiriwa kutoka kwa Muislamu Essam El-Hadary ni kuona atakwenda kufanya mambo gani makubwa hasa ukizingatia kwamba yeye ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika fainali hizo za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia.

El-Hadary ana miaka 45 na hakika anakwenda kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza fainali hizo za Kombe la Dunia kihistoria.

Si Waislamu tu au Wamisri, mashabiki wa soka hasa wa Bara la Afrika wanasubiri kwa hamu kuona kipya huyo mkongwe atakapokwenda kuweka jina lake kwenye kitabu cha rekodi tamu kabisa katika historia ya fainali za Kombe la Dunia.