Kumbe Vardy alimpora tonge mdomoni Adi Yussuf Leicester City

Muktasari:

  • Vardy ndiye aliyeifungia Leicester City mabao 24, akizidiwa bao moja tu na aliyekuwa Mfungaji Bora, Harry Kane wa Tottenham Hotspur, alivunja rekodi ya Ruud Van Nistelrooy na kuweka yake ya kufunga kwenye michezo 11 mfululizo ya EPL.

ASIKUAMBIE mtu, Jamie Vardy ni miongoni mwa nyota wa Leicester City waliotingisha msimu wa 2015/16 timu hiyo ilipochukua ndoo ya EPL.

Vardy ndiye aliyeifungia Leicester City mabao 24, akizidiwa bao moja tu na aliyekuwa Mfungaji Bora, Harry Kane wa Tottenham Hotspur, alivunja rekodi ya Ruud Van Nistelrooy na kuweka yake ya kufunga kwenye michezo 11 mfululizo ya EPL.

Nikurudishe nyuma, Vardy aliyeuwatungua makipa wa Chelsea, Arsenal, Liverpool na Manchester United alijiunga na Leicester City, Mei 17 mwaka 2012 kwa dau la Pauni 1 millioni.

Hapa ndipo picha linapoanzia, wakati ambao Vardy alikuwa ametua kwenye klabu hiyo, mwaka mmoja nyuma mshambuliaji wa Kitanzania, Adi Yussuf alitemwa na klabu hiyo mara baada ya mkataba wake kumalizika.

Pengine Adi angekuwa kwenye kiwango kama cha Vardy, lakini kushindwa kwake kuonyesha makali ilikuwa moja ya sababu iliyomfanya kukosa mkataba wa kuendelea kuichezea Leicester City.

Mshambuliaji huyo ambaye ni Mzaliwa wa Zanzibar, aliishia kucheza kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba na mwishowe akatolewa kwa mkopo Tamworth.

Adi alipata mkataba wake wa kwanza kwenye klabu ya Burton Albion ya Ligi Daraja la Pili England baada ya kufanya vizuri majaribio wakati wa maandalizi ya msimu mpya wa 2011/12.

Wakati ambao Vardy alikuwa ameanza maisha mapya Leicester, Adi alikuwa naye ameshaanza kusahau maisha aliyoiishi kwenye timu hiyo ambayo imejipatia umaarufu miaka yaa 2015 2016.

Adi kwa sasa anaichezea Solihull Moors, alijiunga na Lincoln City mara baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu kumalizika wa kuichezea Burton Albion.

Mwaka 2013, mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa Februari 20, 1992 Zanzibar , alicheza Ligi Daraja la Tano England ambalo ni maarufu kama Conference National.

Mshambuliaji huyo wa Kitanzania aliishia kucheza mikchezo miwili tu alivyotua Lincoln na kutolewa kwa mkopo, Adi alifanya vizuri Gainsborough Trinity, Harrogate Town na Histon alipokopeshwa na aliporejea kwenye klabu yake alifunga mabao matatu kwenye michezo 10.

Agosti Mosi 2014, Adi alipata dili la kujiunga na Oxford City, Agosti 9 ndani ya mwaka huo, mshambuliaji huyo alicheza mchezo wake wa kwanza dakika zote dhidi ya Hyde United.

Katika mchezo uliofuata Adi alifunga mara mbili dhidi ya timu anayoichezea sasa ya Solihull Moors.

Mara baada ya kuripotiwa kujiunga na Mansfield Town kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika Oxford City, aliihusishwa kuitwa Timu ya Taifa ya Tanzania.

Alipoanza maisha yake ya soka ndani ya klabu hiyo, alijikuta akipata nafasi ya kuitwa rasmi kwa mara ya kwanza Taifa Stars lakini ilishindikana kupata nafasi ya kucheza baada ya wapinzani kushindwa kutokea kwenye mchezo huo kutokana na kuwa kwao kwenye hali mbaya kiuchumi.

Akizungumzia ukaribu wake na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta , Adi anasema ni mkubwa na akadai bado ana ndoto ya siku moja kuvaa jezi ya timu ya taifa katika mashindano mbalimbali.

“Ile mechi ya hisani nilikuja kucheza kwa sababu ya Samatta, nilifurahia sana kwa sababu inatoa nafasi kwa mashabiki kuwaona wachezaji wao, lakini pia wote kwa pamoja tunapata nafasi ya kuchangia wasiojiweza.

“Tanzania ni taifa langu kwa hiyo nitabaki kuwa shabiki wa nchi yangu hata kama sintopata nafasi ya kucheza,” anasema mshambuliaji huyo ambaye anajiandaa na timu yake kwa ajili ya msimu mpya wa 2018/19.

Timu nyingine ambazo amezichezea Adi kabla ya kutua Solihull Moor ni Crawley Town ambayo alikuwa akiichezea kwa mkopo wa miezi sita na baada ya muda wa mkopo huo kumalizika akajiunga na Grimsby Town Januari mwaka jana na kuichezea kwa makataba wa miezi 18.

Barrow ndiyo timu ya mwisho ambayo Adi ameichezea kabla ya kutua Solihull Januari mwaka huu na kuisaidia timu hiyo kusalia Ligi Daraja la Tano.

Kwa jumla Adi ambaye amecheza Ligi Daraja la Kwanza England ‘Championship’, Ligi Daraja la Tatu ‘League Two’ amefunga jumla ya mabao 55 kwenye uchezaji wake wa soka la ushindani.

Idadi ya mabao 55 ya Adi, inaingia karibu mara tatu ya mabao ya Vardy ambaye amemzidi kete Leicester City kwa kuwa na mabao 151 kwenye uchezaji wake soka.

Mabao ambayo Vardy ameifungia Leiceter tangu amejiunga nayo 2012 alipopishana na Adi ni mabao 82.