Kizazi kipya cha Hispania kitatisha Russia

Muktasari:

  • Naamini kwamba ni timu yenye mchanganyiko mzuri wa kizazi kipya na wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambayo itakuja kushinda Kombe la Dunia. Na moja kati ya timu zenye sifa hiyo ni Hispania. Bila shaka timu ya taifa ya Hispania ni timu ambayo imepata mafanikio makubwa sana. Tangu mwaka 2008 Hispania wameshinda mashindano ya Euro mara mbili na kombe la dunia mara moja.

MSOMAJI, wiki iliyopita vikosi vingi vya awali vya kombe la dunia vilitangazwa na wakati makala hii inatoka huenda Hispania watakuwa wameshatangaza kikosi chao ambacho kitashiriki katika kombe la dunia nchini urusi ndani ya wiki chache. Kwa mtazamo wangu Kombe la Dunia mwaka huu litakuwa na ladha nzuri sana kwa kuwa timu nyingi zipo katika mchakato wa kubadilisha kizazi na hivyo naamini kwamba mastaa wapya watazaliwa Urusi.

Naamini kwamba ni timu yenye mchanganyiko mzuri wa kizazi kipya na wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambayo itakuja kushinda Kombe la Dunia. Na moja kati ya timu zenye sifa hiyo ni Hispania. Bila shaka timu ya taifa ya Hispania ni timu ambayo imepata mafanikio makubwa sana. Tangu mwaka 2008 Hispania wameshinda mashindano ya Euro mara mbili na kombe la dunia mara moja.

Lakini, katika miaka ya hivi karibuni dalili zote zimeonyesha kwamba timu ya taifa ya Hispania inahitaji mabadiliko.

Katika mashindano mawili mfululizo Hispania hawajakuwa karibu kabisa kushinda taji.

Katika Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014, Hispania walitolewa katika hatua ya kwanza na katika mashindano ya Euro mwaka 2016 walitolewa katika hatua ya pili.

Kocha mkongwe wa Hispania, Vincent Del Bosque alijiuzulu baada ya mashindano ya Euro mwaka 2016.

Na Lopetegui aliteuliwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo. Kocha huyu ana jukumu kubwa la kuirudisha timu ya Hispania katika ubora wao.

Sasa ni chini ya mwezi mmoja hadi kufanyika kwa michuano ya fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa nchini Urusi.

Lakini katika mechi za kufuzu mashindano hayo Hispania walionyesha dalili kwamba wapo njiani kurudi katika ubora wao.

Walicheza mpira wa kushambulia na hawakupoteza hata mechi moja.

Ni imani yangu kwamba Hispania wamepata matokeo kutokana na kuwapa kizazi kipya nafasi katika timu ya taifa.

Hakika, wachezaji kama Iniesta, Silva, na Xabi Alonso wameibeba timu ya Taifa ya Hispania kwa muda mrefu.

Lakini, wachezaji hawa wameshafikia umri mkubwa, Xabi Alonso amestafu na fainali za Kombe la Dunia zitakapochezwa nchini Urusi, mchezaji kama Iniesta atakuwa ameshafikia umri wa miaka 34.

Bahati ya timu ya taifa ya Hispania ni kwamba kizazi kipya cha timu hiyo kimeonyesha uwezo wa kuziba pengo la akina Xabi Alonso.

Ni wachezaji kama Isco na Asensio ambao wote wanachezea Real Madrid, pamoja na Thiago Alcantra ambaye anachezea Bayern Munich, na Alvaro Morata kutoka Chelsea.

Hispania wanacheza mfumo wa mpira ambao unatumia viungo wengi wenye kiwango kikubwa. Isco na Thiago Alcantra wote ni viungo wenye umri mdogo lakini wana vipaji vikubwa. Hata hivyo, chini ya kocha wa zamani wa Hispania, Vincent Del Bosque, wachezaji hawa hawakupata nafasi nyingi katika kikosi cha kwanza cha Hispania kutokana kuwepo na upinzani mkubwa.

Lakini, kocha mpya wa Hispania, Lopetegui, anataka kukiendeleza kikosi cha Hispania na kuwapa wachezaji wenye umri mdogo nafasi katika timu ya taifa.

Wachezaji kama Isco na Thiago hawajawahi kushinda taji na timu yao ya taifa na wana njaa ya kupata mafanikio na timu yao ya taifa. Bila shaka Hispania wana kizazi kipya ambacho kina uwezo mkubwa na pamoja na wachezaji wakongwe wa timu hiyo naamini wataipeleka Hispania mbali sana katika Kombe la dunia mwaka huu.